:
Uhusiano Dhaifu Kati ya Kuzuia VVU Barani Afrika na Matumizi ya Njia za Uzazi wa Mpango
Na Miriam Gathigah
Katika kukimbilia kuokoa watoto wachanga kutokana na maambukizi ya
VVU na kutibu mama
zao, wataalam wanaonya kuwa suala la msingi katika kuzuia VVU
linapuuzwa barani Afrika –
matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa wanawake wanaoishi na
VVU/UKIMWI.
NAIROBI, Agosti 30, 2014 (IPS) - Wakati huo huo inajulikana kuwa uzazi wa mpango ni nguzo ya pili
ya kuzuia kwa
mafanikio maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
(PMTCT), ikiwa ni
pamoja na kuzuia maambukizi miongoni mwa wanawake na watoto na
kutoa matunzo kwa
wale walioambukziwa.
"Mahitaji ya uzazi wa mpango kwa wanawake wanaoishi na VVU mara
nyingi yanawekwa
nyuma ya pazia, na shabaha kuu ikiwa ni kumfanya mama na mtoto
kuwa na afya nzuri,"
Florence Ngobeni-Allen, msemaji wa Elizabeth Glaser Paediatric
AIDS Foundation, aliiambia
IPS. Akiwa ni raia wa Afrika Kusini, alikutwa na VVU mwaka 1996,
akapoteza mtoto wake
kutokana na ugonjwa wa UKIMWI na kwa sasa ana watoto wa kiume
wawili wenye afya
nzuri.
Uzazi wa mpango ni muhimu katika Afrika Mashariki na Kusini,
ambako maambukizi ya
VVU pamoja na kiwango kikubwa cha kutokufikiwa kwa mahitaji ya
uzazi wa mpango, na
ambako wanawake nane kati ya 10 wenye VVU wana umri wa kuzaa, kwa
mujibu wa Shirika
la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA).
Tafiti zinasema kuwa wanawake wanaoishi na VVU wana matamanio sawa
kama siyo zaidi
ya kujipatia watoto ikilinganishwa na wale wasiokuwa na VVU.
Kupunguza kiwango cha
uhaba wa huduma za uzazi wa mpango miongoni mwa wanawake hawa ni
jambo muhimu
ili kufikia lengo la kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa watoto
kwa asilimia 90,"
inasema ripoti ya Umoja wa Mataifa ijulikanayo kama Women Out
Loud.
Tafiti za wanawake wanaoishi na VVU nchini Kenya na Malawi
zinaonyesha kuwa karibu
robo tatu hawataki kupata watoto tena katika kipindi cha miaka
miwili ijayo au milele,
lakini ni robo tu walitumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.
Udhaifu wa mipango
Utafiti wa shirika la Family Health International miongoni mwa
wanawake wanaoishi na VVU
nchini Rwanda, Kenya na Afrika Kusini ulionyesha kuwa zaidi ya
nusu hawakupanga kubeba
mimba zao walizo nazo sasa au hivi karibuni.
Pamoja na kuwa wanawake hao walitaka njia za uzazi wa mpango,
upatikanaji wake
ulikuwa mgumu. Moja ya kikwazo ilikuwa ni wafanyakazi wa afya:
walikuwa hawana ujuzi
wa kutoa aina mbalimbali ya njia za uzazi wa mpango kwa wanawake
wanaoishi na VVU;
walikuwa na imani potofu kuhusu usalama wa njia za uzazi wa
mpango; wengi wao walitoa
kondomu za kiume tu, pamoja na kwamba wanawake walipendelea
vipandikizi na sindano,
na wengi walikuwa wakitoa hukumu juu ya maisha ya kujamiiana ya
wanawake hao.
"Mara nyingine manesi walisahau kuwa wanawake bado wana hamu ya
kujamiiana hata
kama wanaishi na VVU," anasema Ngobeni-Allen.
Kutokufikiwa kwa mahitaji ya huduma za uzazi wa mpango nchini
Kenya kunafikia asilimia
25 nchini kote lakini kunafika asilimia 60 miongoni mwa wanawake
wanaishi na VVU, Dk
John Ong’ech, mkurugenzi msaidizi katika Hospitali ya Kenyatta
aliiambia IPS.
Upatikanaji duni wa huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake wenye
VVU ambao wana
uwezekano wa kufa mara sita hadi nane kutokana na matatizo ya
mimba ikilinganishwa na
wale wasiokuwa na VVU, "ni udhaifu katika mipango ya afya,"
aliiambia IPS, pamoja na
kwamba ni rahisi na inafanya kazi kutoa huduma za uzazi wa mpango
kuliko PMTCT.
Wanaume na mama wakwe
Mary Naliaka, ambaye anafanya kazi katika kitengo cha UKIMWI kwa
watoto katika wizara
ya afya nchini Kenya aliiambia IPS kuwa uzazi wa mpango unapaswa
uwe sehemu ya tiba ya
VVU na kutoa aina mbalimbali za njia za kupanga uzazi.
Lakini mifumo ya afya katika Mashariki na Kusini mwa Afrika mara
nyingi inakabiliwa na
uhaba wa vifaa na kliniki nyingi hazina miundombinu ya kutosha.
"Kutumbukiza kipandikizi kwa mwanamke kunahitaji mazingira mazuri
yenye vifaa vya
kuua vijidudu," Ong’ech anasema.
Sindano ni njia inayotumiwa zaidi na wanawake kwasababu wanaweza
kutumia bila waume
zao kujua, anaongeza.
Kukosekana kwa usawa wa kijinsia na wanawake kukosa ushawishi
kunasababisha
matumizi duni ya njia za uzazi wa mpango. Naliaka anasema kuwa
katika utamaduni wa
Kiafrika, "mama mkwe anaweza kusababisha kuvunja ndoa kama hakuna
mtoto
anayezaliwa."
Dorothy Namutamba, kutoka Jumuiya ya Kimataifa ya Wanawake
Wanaoishi na VVU katika
Afrika Mashariki (ICWEA), ambaye ofisi yake ipo Kampala, Uganda,
aliiambia IPS kuwa
wanawake wameumbwa kuwafurahisha waume zao.
"Kama mwanaume anadai anataka kuwa na watoto kumi ni lazima
kukubali na kama hutaki
atawatafuta kutoka kwingine," anasema. "Wanaume wengi hawataki
wanawake kutumia
uzazi wa mpango, hilo ni tatizo kubwa."
Unyanyapaa na unyanyasaji wa majumbani unazidisha tatizo.
"Wanawake wanahofia kutaja
kuwa wameambukizwa VVU kutokana na kuwa wanaweza kukabiliwa na
unyanyasaji wa
kijinsia, na hii inazuia kupata njia za uzazi wa mpango," Anthony
Mbonye, kamishina wa
Huduma za Afya nchini Uganda, aliiambia IPS.
Kutokana na nguvu za wanaume katika utoaji wa maamuzi kuhusu
mimba, huduma za afya
ya uzazi zinazoshirikisha wanandoa wawili ni muhimu, lakini "vituo
vya afya vina
msongamano mkubwa mno kuweza kuhudumia wanandoa wa kiume," Naliaka
aliiambia
IPS.
Ushinikizaji wa kufunga kizazi kwa wanawake wanaoishi na VVU
nchini Kenya, Malawi,
Namibia, Afrika Kusini na Zambia, huku kukiwepo na kesi
mahakamani, kunazidisha utata
wa suala la haki na mahitaji ya uzazi na VVU.
"Hii inaaibisha sekta ya afya," anasema Naliaka. Hata hivyo,
anaongeza, "kupitia kesi hizi,
sekta ya afya na umma umeelewa kuwa wanawake hawa wana mahitaji ya
uzazi kama ilivyo
kwa wenzao wasiokuwa na virusi."
Eneo moja la kutolea huduma
Ili kusonga mbele, wataalam wanapendekeza kuunganisha VVU, uzazi
wa mpango na
huduma za uzazi na watoto wachanga ili kuokoa muda kwa watumiaji
na wafanyakazi wa
afya.
Nchi saba za Kusini mwa Afrika zimeshaanzisha eneo moja la kutolea
huduma ambapo
wanawake wanaweza kupata ARVs, kupima kansa ya kizazi, ushauri wa
kunyonyesha na
uzazi wa mpango kwa wakati mmoja, chini ya jengo moja, mara
nyingine katika chumba
kimoja chenye mhudumu wa afya.
Kuunganisha huduma kunaokoa gharama na kunaleta ufanisi, inasema
UNFPA. (END/2014)