Inter Press Service News Agency
Thursday, August 13, 2020   09:19 GMT    

:
Jitihada za Mwanamke Kutafuta Njia Sahihi za Uzazi wa Mpango


Na Miriam Gathigah


Beatrice Njeri ndio punde tu amerejea kutoka kazini kwake kama mhudumu katika shule ya msingi mjini Nairobi. Ni mwezi wa Agosti 2009.

NAIROBI, Agosti 30, 2014 (IPS) -
Akiwa amewasili nyumbani mapema kuliko ilivyo kawaida yake, mama mwenye ndoa yake na watoto wawili alimkuta mume wake akimsubiri katika kibanda chao huko Kisumu Ndogo, katika makazi duni ya Kibera.

Mwanaume huyo alikuwa amegundua kuwa anaishi na VVU. Wiki moja baadaye, mwanamke pia alionekana kuwa na VVU.

Wakati huo wote walikuwa na umri wa miaka 29. "Tulikuwa wadogo sana na tulijua mambo machache sana kuhusu VVU," anasema.

Wakiwa na watoto wa kike wawili, ambao wote hawana VVU, walikuwa wanataka kupata mtoto wa kiume, lakini waliamua wasipate mtoto tena.

Wakati huo Njeri alitumia njia ya uzazi wa mpango aina ya Depo-Provera, ambayo ni kwa njia ya sindano na inadumu kwa miezi mitatu, na alihitaji kupiga sindano tena.

Walipogundua kuwa Njeri alikuwa na VVU, manesi walimshawishi kufunga kizazi kabisa jambo ambalo siyo yeye wala mume wake walijiandaa kulifanya.

Ikiwa haijafahamika kwa Njeri, nchi ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya uzazi wa mpango wakati huo. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba kulikuwa na habari zisizokuwa rasmi kwamba wanawake waliotaka kutumia njia ya sindano ya uzazi wa mapango ambayo inatumika zaidi, walipigwa sindano za maji badala yake.

Njeri aliiambia IPS kuwa manesi walisema kuwa walitoa kipaumbele kwa wanawake wengine wenye mahitaji makubwa ya njia za uzazi wa mpango.

"Walisema nilikuwa najipenda mwenyewe kutokana na kukataa kufunga kabisa kizazi," anasema. "Manesi walinishinikiza kuondoa kitu pekee kilichonifanya nijisikie kuwa mwanamke kamili. Sikutaka kitu hicho kutolewa."Alishauriwa kutumia kondomu kuzuia mimba. Lakini kondomu ilikuwa kitu kipya kwao, na haikuwa rahisi.

"Kutumia kondomu wakati wote ilikuwa jambo gumu sana. Ngono ikawa haina mvuto. Niliichukia," anasema.

Bei ilikuwa jambo jingine. "Sote ni wafanyakazi vibarua. Katika makazi haya duni, kupata chakula ni kipaumbele pekee," anasema. Msaada mkubwa unatoka kanisani, kwani viroba vya nguo na chakula huletwa mara kwa mara.

Njeri alielezea tatizo lake kwa mkunga wa jadi, ambaye alimshawishi kufanya ngono tu wakati wa siku salama.

Lakini hakujua kuwa madawa aina ya antibiotics yangeweza kuingilia utaratibu wa siku za hedhi, na wakati huo huo Njeri alikuwa akizitumia kuzuia maambukizi nyemelezi kutokana na VVU. Hii ilifanya njia ya kutumia siku salama kutokufanya kazi ya kuzuia mimba.

Miezi nane baadaye, Njeri alijikuta ana mimba. Alipofika kliniki kwa mara ya kwanza, kinga zake za mwili za CD4 zilikuwa 400. Alipojifungua mtoto wake wa kiume mwaka 2011, kinga zake zilikuwa 180. Alianza kutumia madawa ya kupunguza makali kama ilivyokuwa kwa mume wake.

Lakini mtoto wao huyo wa kiume aliambukizwa VVU.

Pamoja na kwamba Njeri alikuwa akitumia madawa ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika hospitali ya serikali ya Mbagathi karibu na Kibera, alichagua kujifungua kwa mkunga wa jadi kwasababu wana upendo kuliko wafanyakazi wa hospitali.

"Hospitali nyingi za serikali zina msongamano mkubwa; hazina muda wa kuonyesha upendo wala kujali. Unakuwa na bahati kubwa kama nesi anakuhudumia," anasema.

Kati ya mwaka 2012 na 2013, mfululizo wa migomo ya wafanyakazi katika sekta ya afya ulisababisha uhaba wa sindano za uzazi wa mpango. Kwa masikitiko wanandoa hao waliamua kutumia kondomu.

Kuwa na VVU, kuwa na nguvu za kufanya mapenzi na kuwa kijana wa kubeba mimba ni tatizo kubwa, anasema.

"Vituo vingi vya afya haviwezi kutuhudumia kufikia mahitaji yetu," aliiambia IPS.

Baadhi ya kliniki zimetenga siku ya kutoa huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake wenye VVU lakini Njeri hawezi kwenda kutokana na kazi.

Kwa sasa Njeri amerejea katika matumizi ya sindano kuzuia mimba. Anaomba kuwa atakaporejea kliniki miezi miwili ijayo kupiga sindano, huduma hiyo itakuwepo. (END/2014)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2020 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.