Inter Press Service News Agency
Thursday, August 13, 2020   07:46 GMT    

:
Nini Muhimu Zaidi, Vita juu ya UKIMWI au Vita tu?


Na Kanya D'Almeida na Mercedes Sayagues


Wanasema kuna vita na inalenga Virusi vya Ukimwi (VVU).

JOHANNESBURG/NEW YORK, Agosti 29, 2014 (IPS) -
Vita hii inafanyika duniani kote lakini uwanja wake wa vita ni Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako watu saba kati ya 10 wana VVU duniani watu milioni 24.7 mwaka 2013. Ukanda huo ulipatwa na vifo vilivyohusiana na UKIMWI milioni 1.3 mwaka huo, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.Askari wa sungusungu wanapambana na vita dhidi ya UKIMWI. Mara nyingi jeshi hilo linakuwa na maafisa wa misaada waliovalia vizuri wakiwa wamekaa katika vyumba vya mikutano wakitoa fedha. Wakati mwingine, wanatumia askari waliovalia nguo chafu wanaotembea kwa miguu ambao ni watoa huduma za afya katika jamii na wanaharakati wa UKIMWI wakiwa katika maeneo ya vijijini yaliyojitenga na ambayo hayana hata maji ya bomba, wala madawa ya kurefusha maisha.

Huku kukiwa na matatizo mengi ya afya yanayoshindana pamoja, ufadhili wa masuala ya UKIMWI unazidi kuwa tatizo. Hata hivyo ukiangalia katika bajeti ya ulinzi ya nchi kadhaa zenye VVU inaonyesha picha inayoshangaza ya vipaumbele vya serikali, huku kukiwa na matumizi makubwa ya jeshi huku wakitoa sababu kuwa kikwazo kikubwa cha kushinda vita dhidi ya UKIMWI ni uhaba wa fedha.

Na wakati mwaka wa mwisho wa 2015 kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa ukikaribia huku nchi wafadhili wakizidisha kukaza uzi wataalam wa afya wana hofu kuhusu ufadhili wa kuzuia VVU na utoaji wa tiba ya UKIMWI baada ya mwaka 2015.

Fedha mpya za kufadhili UKIMWI katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati zilipungua kwa asilimia tatu mwaka 2012 hadi dola bilioni 8.1 mwaka 2013, inasema ripoti ya pamoja ya Mfuko wa Familia ya Kaiser na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na VVU/UKIMWI (UNAIDS) iliyotolewa Juni.

Nchi kubwa wahisani tano kati ya 14 Marekani, Canada, Italia, Japan na Uholanzi zilipunguza matumizi yake katika UKIMWI mwaka jana.

Na hata hivyo, wakati serikali zikisema zina matatizo makubwa ya kifedha kupambana na UKIMWI, fedha kwa ajili ya kupigana katika vita vingine zinaonekana zinapatikana kiurahisi.

Matumizi katika vita na katika UKIMWI

Afrika itahitaji kufanya kazi kubwa zaidi kwa kiasi kidogo ilichonacho katika kukabiliana na UKIMWI, inahitimisha ripoti ya UNAIDS ya 2013 inayojulikana kama Smart Investments.

Nchini Kenya, kushuka kwa matumizi kunatarajiwa hivi karibuni, kutokana na kwamba fedha zinazotolewa na Benki ya Dunia jumla ya dola milioni 115 kupambana na UKIMWI zilimaliza muda wake mwezi uliopita.

Wakati huo huo, bajeti ya ulinzi ya taifa hilo inatarajiwa kuongezeka kutoka dola bilioni 4.3 mwaka 2012-2014 hadi dola bilioni 5.5 mwaka 2018, wakati nchi ikiwa inafanya manunuzi ya helikopta, ndege za kijeshi zisizotumia rubani, na vifaa vya kufanya doria katika mipaka ya nchi, kwa mujibu wa tovuti ya DefenceWeb.

Ni kweli Kenya inakabiliwa na mashambulizi ya magaidi wa Al-Shabaab. Lakini bado wanawake wajawazito watano kati ya 10 nchini Kenya wanaoishi na VVU hawapati madawa aina ya ARVs kulinda watoto wao.

Ndege za Kivita Nchini Msumbiji

Nchini Mzumbiji, kukosekana kwa fedha kumeweka matumizi ya nchi katika ulinzi na jeshi katika mwanga.

Daniel Kertesz, mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni nchini Msumbiji, aliiambia IPS kuwa mpango wa afya wa miaka sita nchini humo una pengo la dola milioni 200 kwa mwaka.

Kutokana na Msumbiji kuwa nchi maskini sana, huwezi kuona ni jinsi gani nchi yenye watu milioni 1.6 ambao wameambukizwa VVU, taifa la nane kwa mzigo wa ugonjwa huo itaweza kufikia mahitaji yake ya ndani.

"Leo hii, Msumbiji inatumia kati ya dola 30 na 35 kwa kila mtu katika afya. WHO inapendekeza kiwango cha chini kuwa dola 55-60 kwa kila mtu kwa mwaka," Kertesz alisema.

Wiki hiyo hiyo, serikali ilitangaza imetengeneza ndege za kivita sita ambazo ilizitelekeza miaka 15 iliyopita, nchini Romania, na inategemea kupata ndege za kijeshi tatu aina ya Embraer Tucano kutoka Brazili bure, huku kukiwa na uelewa kuwa ununuzi wa ndege za kivita tatu utafuata.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ya Kitengo cha Uchunguzi wa Kiuchumi, matumizi ya Msumbiji katika usalama wa nchi yanatarajiwa kuongezeka kwa kasi, hasa kutokana na manunuzi ya wizara ya ulinzi, ya boti 24 za uvuvi na meli sita za doria na meli za kivita kwa gharama ya dola milioni 300 sawa na nusu ya bajeti ya afya ya taifa ya mwaka 2014 iliyokuwa dola milioni 635.8.

Wiki hiyo hiyo ambayo ndege za kivita zilizofanyiwa matengenezo zilipotua mjini Maputo, vyombo vya habari viliripoti kuwa hospitali kuu katika jimbo la kaskazini magharibi na lenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe la Tete ilikaa kwa siku tano bila maji.

Ni hali isiyopingika kuwa mfumo wa afya ya umma nchini humo upo katika hali mbaya ambapo Mpango wa Msaada wa Dharula wa Rais wa Marekani (PEPFAR) unachangia asilimia 90 ya bajeti ya mwaka ya UKIMWI katika wizara ya afya."Bajeti ya nchi katika masuala ya kijamii haiongezeki kama ambavyo bajeti ya jeshi, ulinzi na usalama inavyoongezeka," Jorge Matine, mtafiti katika Kituo cha Public Integrity (CIP) nchini Msumbiji, aliiambia IPS.

"Tumekuwa tukishinikiza kuwepo kwa uwajibikaji katika manunuzi ya meli za kibiashara na kijeshi ambazo zinagharimu mamilioni ya dola," alisema.

Muungano wa NGOs umeomba serikali kujieleza juu ya "uamuzi wake wa kutumia fedha hizo bila ya kupata kibali kutoka Bungeni wakati nchi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi na vifaa katika sekta ya afya," Matine alielezea.Umoja huo unasema kuwa kama matumizi katika ulinzi yangebakia kama ilivyokuwa mwaka 2011, nchi ingeokoa dola milioni 70, ambazo zingenunua magari ya wagonjwa 1,400 (ambayo ni sawa na magari 11 kwa kila wilaya, wakati wilaya nyingi zina gari moja au mawili tu) au kuagiza asilimia 21 ya madawa zaidi.

Hali kama hiyo inajitokeza katika bara zima ambapo, kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Kimataifa wa Amani ya Stockholm (SIPRI), matumizi katika jeshi yalifikia wastani wa dola bilioni 44.4 mwaka 2013, ongezeko la asilimia 8.3 kutoka mwaka uliopita. Nchini Angola na Algeria, mapato makubwa ya mafuta yalichochea manunuzi hayo.

Kampeni yenye makao yake nchini Afrika Kusini inayojulikana kama Ceasefire Campaign iliripoti kuwa manunuzi ya silaha yaliyofanywa na makampuni binafsi yanazidi kuongezeka barani Afrika, huku serikali zikitarajiwa kusaini mipango hiyo na makampuni ya ulinzi ya kimataifa yenye thamani ya jumla ya dola bilioni 20 katika muongo ujao. (END/2014)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2020 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.