Inter Press Service News Agency
Friday, February 22, 2019   20:40 GMT    

:
Nigeria Yaamka Kukabiliana na Tishio la UKIMWI


Na Sam Olukoya


Ndoa ya Tope Tayo ilivunjika miaka 11 iliyopita baada ya kugundulika alikuwa na VVU. Mume wake aliyekuwa na hasira alimchukua mtoto wao wa pekee. Miezi mitatu baadaye, wakati mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja alipogundulika kuwa na virusi, mwanaume huyo alikwenda kumtupia Tayo na kumtelekeza.

Lagos, Nigeria, Agosti 25, 2014 (IPS) -
"Alitutelekeza kana kwamba tulifanya uhalifu lakini nilimwambia kupata maambukizi ya VVU siyo uhalifu," Tayo aliiambia IPS.

Mwanamke huyo alikuwa hana ajira na mume wake hakulipia chochote cha matunzo ya mtoto. "Nilitebea mtaani na kuanza kulia, niliishi kwa kutegemea msaada," Tayo anakumbuka.

Mwanaume kutelekeza mke mwenye VVU na watoto ni suala la kawaida nchini Nigeria, anasema Rosemary Hua, mratibu wa shirika la kutetea haki za watoto la "First Step Action for Children".

"Akina baba wanaondoa msaada wao kwa familia kwasababu wanahisi hakuna haja ya kuendelea kuwekeza kwa mtoto ambaye ana uwezekano wa kufariki dunia akiwa bado mdogo," Hua aliiambia IPS.

Kiwango cha maambukizi cha asilimia 3.2 nchini Nigeria kinaonekana kuwa cha chini ikilinganishwa na kusini mwa Afrika, lakini ikiwa na idadi ya watu milioni 173, asilimia hiyo inatafsiriwa kuwa idadi kubwa ya watu milioni 3.4 ya Wanigeria walikuwa na VVU mwaka 2013.

Miongoni mwa hawa, watoto wa chini ya umri wa miaka 14 ni 430,000, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Kupambana na UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS). Nigeria inabeba theluthi moja ya maambukizi yote mapya kwa watoto katika nchi 20 zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo katika Afrika Kusini mwa Jngwa la Sahara.

Ripoti hiyo inasema Nigeria inakabiliwa "na vitisho vitatu ambavyo ni mzigo mkubwa wa VVU, kutokupungua au kupungua kidogo sana kwa maambukizi mapya ya VVU na utoaji wa tiba kwa idadi ndogo ya waathirika."

Hata hivyo, kiwango cha VVU kitaifa kinaonyesha tofauti kubwa iliyopo miongoni mwa majimbo 36 nchini humo: katika majimbo manne, kiwango cha maambukizi kinatofautiana kati ya asilimia nane hadi 15.

Kwa nini wanawake hawataki kupima

Tayo na mtoto wake wamekuwa wakitumia madawa ya kurefusha maisha kwa miaka 11 iliyopita sasa. Hawa wana bahati. Chini ya Wanigeria 600,000 wanatumia madawa hayo, au asilimia 20 tu ya wale wanaoyahitaji.

Utoaji tiba kwa wachache unasababisha kuwepo kwa imani potofu na unyanyapaa, kama ambavyo habari ya Tayo inavyoelezea.

Kutelekezwa mara nyingi kuna maana kuwa kujiingiza katika ugumu wa maisha kiuchumi. Nusu ya wanawake nchini Nigeria hawana ajira.

"Hofu ya kuendesha maisha yake peke yake au pamoja na kutunza mtoto wake kunasababisha wanawake wenye VVU kujitumbukiza katika ngono ili kupata fedha za kujikimu na hii inaweza sababisha kusambaza virusi zaidi," anasema Lucy Attah, mwanaharakati wa jinsia ambaye anaishi na VVU. Yeye ni mkurugenzi wa shirika la kusaidia wanawake wanaoishi na VVU la "Women and Children of Hope Foundation", ambako IPS ilikutana na Tayo.

Tayo aliiambia IPS kuwa alikataa kupima alipokuwa na mimba. Hospitali za umma nchini Nigeria zinapima mara kwa mara wanawake wajawazito lakini hofu ya kubaguliwa kama ukikutwa una virusi kulisababisha Tayo kwenda kwenye hospitali za binafsi ambako siyo lazima kupima.

"Ni jambo kubwa ninalolijutia katika maisha yangu," aliiambia IPS.

Sababu moja ambapo wanawake wenye mimba wanakataa kupima, anasema Hua, ni kutokana na wafanyakazi wa afya "kukosa weledi kwa kushindwa kutunza siri za matokeo ya wagonjwa wanaokutwa na VVU."

"Kuna wakati inatubidi kupeleka wagonjwa katika hospitali ambazo ziko mbali na mahali tunapoishi kwasababu ya kuenezwa kwa taarifa zao juu ya kuwa na virusi," aliiambia IPS.

Baadhi ya wafanyakazi wa afya hawataki kugusana na wanawake wenye VVU kwasababu wana imani kuwa wanaweza kuambukizwa virusi kwa kuwagusa, anasema Attah."Kwa juu juu inaonekana kuwa kuna uelewa mkubwa miongoni mwa wafanyakazi wa afya lakini katika uhalisia kuna unyanyapaa mkubwa," anasema Attah.

Sheria dhidi ya ubaguzi na kutunza siri za wagonjwa imeshapitishwa na bunge na sasa inasubiri kutiwa saini na Rais Goodluck Jonathan.

Lakini Nigeria inahitaji zaidi ya kuwa na sheria kukabiliana na ugonjwa huo.

Mwaka 2012, UNAIDS ilielezea kuwa taifa hilo limesimama katika kuchukua hatua stahiki na zinazohitajika kupambana na ugonjwa huo."

Nigeria ina asilimia 13 ya watu wanaoishi na VVU na asilimia 19 ya vifo vinavyohusiana na VVU katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa mujibu wa UNAIDS.

Ni taifa la Chad pekee lipo chini ya Nigeria katika utoaji wa tiba kwa wanawake wajawazito wanaishi na VVU.

Habari njema

Tangu kutolewa kwa taarifa hizo, serikali imechukua hatua kali kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) miongoni mwa majimbo 12 yaliyoathirika zaidi.

Huduma za utoaji wa madawa kwa PMTCT zilifika asilimia 27 mwaka 2013, kiwango kikubwa ikilinganishwa na asilimia 19 mwaka 2012, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).

Baadhi ya majimbo yaliongeza mara mbili au tatu idadi ya kliniki zinazotoa huduma za VVU, na hivyo kufikisha idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma za PMTCT kufikia 2,216 pamoja na kwamba bado ni idadi ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya vituo 16,400.

Maambukizi ya kila mwaka kwa watoto yalishuka kutoka 60,000 mwaka 2012 hadi 51,000 mwaka 2013.

Lakini, hali ikionyesha kuwa wanawake wawili katika kila watatu wenye mimba hukataa kutumia huduma za kliniki, changamoto inayobakia ni jinsi ya kuwafikia kwa kuboresha huduma na kuwapatia taarifa.

"Lazima tuwafikie badala ya kusubiri waje kwetu katika vituo vya afya," Arjan de Wagt, mkuu wa VVU na watoto katika UNICEF nchini Nigeria, aliiambia IPS. "Tusipofanya hivyo watoto wataendelea kufariki dunia kutokana na gonjwa la UKIMWI." (END/2014)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2019 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.