Inter Press Service News Agency
Tuesday, February 20, 2018   03:37 GMT    

Matumaini kwa Vijana Wanaoishi na VVU Kaskazini mwa Ghana :


Na Albert Oppong-Ansah


Ikiwa machozi yanamtiririka shavuni mwake, Zainab Salifu alipanga foleni katika kitengo cha tiba ya homa katika Hospitali ya Mafunzo ya Tamale kaskazini mwa Ghana. Mapema siku hii, kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 alishaonekana kuwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

TAMALE, Machi 13, 2014 (IPS) -
Pamoja na aina ya ushauri nasaha alioupata kutoka kwa nesi Felicity Bampo, Salifu aliuona ulimwengu wake ukimwangukia. Alifikiria afadhali angekufa tu. Salifu aliiambia IPS, alianza kutetemeka na kuanguka sakafuni. Watu walimwangalia. Halafu mwanaume mwenye umri wa makamo, alimchukua na kumpeleka katika kona moja ya hospitali hiyo kimyakimya. Sulemana Sulley alimwambia Salifu kuwa yeye mwenyewe aliambukizwa VVU miaka 10 iliyopita baada ya kuwa na wapenzi wengi na bila kujua alimwambukiza pia mke wake. Lakini wanandoa hao waliendelea kuishi pamoja, na wote wanatumia madawa ya kurefusha maisha (ARV), na wameshapata watoto wawili ambao hawajaambukizwa VVU. "Huu siyo wakati wa kulia," alimwambia Salifu. "Kubali hali uliyo nayo. VVU siyo kibali cha kifo. Elekeza nguvu zako katika kutumia ARVs, kula chakula bora na fanya sana mazoezi." "Wewe hauko peke yako, kila mmoja wetu anaweza kuambukizwa virusi. Hebu ona mimi nilivyo," aliongeza. Sulley anafanya kazi katika kikundi cha kujitolea cha "Model of Hope", ambacho kilianzishwa na shirika la "Catholic Relief Services". Kikundi hicho kina wanachama 19 katika eneo la Tamale na wana mafunzo kama washauri nasaha wa kujitolea wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi ya Ghana. Mji huo ukiwa na wakazi 540,000, Tamale, iliyopo takribani kilomita 600 kaskazini mwa mji mkuu wa Ghana wa Accra, unakuwa mji wa nne kwa ukubwa na makao makuu ya ukanda wa kaskazini. Kila Jumanne na Ijumaa, siku maalum katika Hospitali ya Tamale kwa ajili ya kupima VVU na kuchukua ARV, wafanyakazi wa kujitolea wanakuwepo hapo kusaidia watu wapambane vema na matokeo mapya ya vipimo na kuangalia ni jinsi gani wagonjwa wanaotumia tiba wanakabiliana na ugonjwa. Kwa mujibu wa Bampo, upimaji na utoaji wa huduma za ushauri nasaha huwafikia wastani wa vijana sita hadi 10 kwa siku, mara nyingi kupitia madaktari wa rufani. Wachache wanafika hapo kwa kupenda wao wenyewe, aliiambia IPS. "Upimaji wa virusi kwa hiari siyo jambo linalofanyika mara kwa mara miongoni mwa vijana kwasababu wanahofia unyanyapaa", alisema. Miongoni mwa vijana wenye umri wa kufanya mapenzi kati ya miaka 15-24, ni wanne tu kati ya 10 miongoni mwa watoto wa kike na wawili kati ya kumi miongoni mwa watoto wa kiume wamepima afya zao, kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria Vingi Ghana (MICS) wa mwaka 2011.

"Watu wengi wanatambua VVU ni nini na baadhi ya dlili zake lakini wachache wanajua kuwa ARVs inaweza kuongeza mfumo wa kinga mwilini na mtu anaweza kuishi maisha marefu," alisema Bampo.

Maambukizi madogo, unyanyapaa mkubwa Kwa wastani Ghana ina maambukizi ya chini ya VVU kwa asilimia 1.4, kutoka asilimia 2.3 ya mwaka 2001. Lakini maambukizi ya chini yanaleta matatizo yake: kukosekana kwa uelewa wa jinsi ya kuusimamia ugonjwa, viwango vya juu vya unyanyapaa na viwango vya chini vya kuvumiliana. Ni asilimia sita tu ya wanawake na asilimia 15 ya wanaume wenye umri kati ya miaka 15 na kuendelea wanakubaliana na suala la kuishi na VVU, kwa mujibu wa MICS. Salifu, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika chuo cha ufundi, aliiambia IPS kuwa aliambukizwa virusi na rafiki yake wa kiume. Waliachana naye lakini bado hajaweza kukubali kumwambia yeye wala familia yake kuhusu suala lake la kuonekana na VVU mwezi Disemba 2013. Kama ilivyo kwa Salifu, wanawake saba kati ya 10 wangeweza kuficha kuwa mwanafamilia ameambukizwa virusi vya Ukimwi. Sulley anakosoa kuenea kwa wingi kwa mtizamo kuwa virusi hivyo ni kifo na kwamba mtu anaweza kuambikizwa VVU kwa kuwa karibu na mtu ambaye ameambukizwa. "Tumeachana na upimaji wa bure kwasababu upimaji wote sasa umeelekezwa kwa wanawake wajawazito." kwa mujibu wa Nuhu Musah, mratibu wa VVU na Kitengo cha Kusaidia wenye Ukimwi. Mwaka 2013, Sulley aliwapatia ushauri nasaha vijana 200 ambao waliambukizwa, huku wengi wao wakiwa wanafunzi. Wengi waliwaza kujiua, na Sulley na wafanyakazi wenzake wanatoa elimu juu ya kuishi maisha chanya na yenye furaha. Sulley aliiambia IPS kuwa vijana kadhaa wameshajiua miaka ya karibuni baada ya kutambulika kuwa wanaishi na VVU. Nuhu Musah, mratibu wa VVU na Kitengo cha Kusaidia wenye Ukimwi kaskazini mwa Ghana, anasikitika kuwa Kampeni ya Tambua Hali Yako iliyoelekezwa kwa vijana ilisitishwa kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kupimia. "Tumeshaachana na kazi zote za kupima bure kutokana na kukosekana kwa vifaa kwasababu kwa sasa vimeelekezwa kwa wanawake wajawazito,"aliiambia IPS. Kampeni hiyo ilifanya programu za elimu kila mwezi katika jamii wakati wa matukio ya kitaifa, kama vile Siku ya Uhuru, kushawishi upimaji. Kwa mujibu wa Musah, ukanda wa kaskazini una vituo vinne kwa ajili ya vijana kupima VVU na afya ya kujamiiana lakini kutokana na kukosekana kwa rasilimali hadi sasa havifanyi kazi. Hii haitaondoa takwimu za wachache wanaopima VVU na kuongeza ufahamu miongoni mwa vijana. Katika hali ya kitaifa, ni vijana wa kiume na vijana wa kike wanne tu kati ya 10 wenye umri kati ya miaka 15-24 wana ufahamu wa kutosha kuhusu Ukimwi , MICS iligundua.

Kaskazini mwa Ghana kuna ufahamu wa chini zaidi wa wanaume na wanawake juu ya Ukimwi, ambao ni asilimia 17 ikilinganishwa na asilimia 47 katika Accra Kuu. Takwimu za MICS zinaonyesha kuwa Ghana imeshindwa kufikia lengo lake la kuwezesha asilimia 95 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 wana ufahamu wa kutosha juu ya VVU ifikapo mwaka 2015.

"Ufahamu wa kutosha wa kuzuia VVU na maamukizi bado ni mdogo nchini Ghana, pamoja na kuwa na miaka mingi ya uhamasishaji wa umma," ulihitimisha utafiti huo. "Nguvu za pamoja zinafaa kuelekezwa kwa vijana kwani wengi wao wanaambukizwa kutokana na ufahamu wao mdogo wa VVU." (END/2014)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2018 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.