Inter Press Service News Agency
Tuesday, December 18, 2018   23:57 GMT    

:
Uzuri na Ubaya wa Dawa Mpya ya ARV kwa Wajawazito Nchini Uganda


Na Wambi Michael


Uganda inapata sifa nyingi lakini pia kuna baadhi ya wakosoaji juu ya kuanza kwake kutumika kwa dawa mpya ya kupunguza makali ya VVU kwa wanawake wajawazito na watoto wao, ijulikanayo zaidi kama Option B +.

KAMPALA, Jan 13, 2014 (IPS) -
Ikipendekezwa na Shirika la Afya Ulimwenguni Juni 2012, Option B+ inaweza kurefusha maisha kwa wanawake wajawazito bila kujali idadi ya kinga mwilini mwao (yaani CD4 count). Kabla ya hapo, kwa kutumia dawa aina ya Option A na B, mama na mtoto walipatiwa ARVs wakati wakiwa wajawazito au wakinyonyesha. Ni wanawake tu ambao kiasi cha CD4 kilikuwa chini ya 350 walipewa ARVs kwa maisha yao yote lakini mashine za kuhesabu kiasi cha CD4 ni za gharama kubwa na hazipatikani kiurahisi barani Afrika. Uganda imefanya kazi nzuri. Zaidi ya asilimia 70 ya vituo vyote vya afya vinatoa dawa aina ya Option B+ na ilivuka lengo na kufikia wanawake 35,000 katika mwaka wa kwanza na kufikia wanawake 50,000 ilipofika Oktoba mwaka 2013. "Tumefanya vizuri sana katika kuanza kutumia dawa hii," alisema Godfrey Esiru, mratibu wa kitaifa wa mpango wa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) katika Wizara ya Afya. "Ni mpango wa gharama nafuu kwa nchi ambayo ina uhaba wa rasilimali katika sekta ya afya." Kiwango cha maambukizi ya VVU nchini Uganda ni asilimia saba, au watu wapatao milioni 1.5, kwa mujibu wa Shirika la Kupambana na UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS).

Wanaharakati wa masuala ya UKIMWI wamekaribisha kuanza kwa mpango huo lakini wameonyesha wasiwasi wao. "Option B+ inanyima wanawake wajawazito haki ya kuamua kama wanapenda kujiunga na huduma hiyo au hapana," alisema Dorothy Namutamba wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanawake Wanaoishi na VVU/UKIMWI katika mashariki mwa Afrika (ICWEA). Ukosoaji huo ulitolewa zaidi katika mjadala wa vikundi maalum ulioandaliwa na ICWEA mwaka 2012 kujadili uzoefu wa wanawake katika matumizi ya dawa aina ya Option B+ nchini Uganda na Malawi. "Majina ya Option A, B na B+ yana maanisha kuwa wanawake wajawazito ambao wanakutwa na VVU wanapatiwa madawa aina mbalimbali ya kuchagua, wakati katika uhalisia ni serikali ambayo inachagua aina gani ya dawa ya kuitekeleza," inasomekana ripoti ya mjadala wa vikundi ya ICWEA.

Wanawake vijana ambao wana VVU wanaweza wasipende kuanza kutumia ARV kurefusha maisha yao wakati bado wanajiona kuwa na afya, pamoja na kwamba dozi ya dawa hiyo ni kidonge kimoja kwa siku. Katika kipindi kirefu, watu wawili kati ya kumi waliotumia dawa wanakuwa na usugu wa ARVs na hivyo kulazimika kugeukia dawa ya mstari wa tatu ambayo ni ya ghali zaidi. Mwanaharakati Mulani Birimumaso na mke wake wameishi na VVU kwa miaka 15. Mabinti zao wawili hawana VVU kutokana na kutumia huduma za PMTCT ambazo zinapatikana nchini Uganda tangu mwaka 2001. Ana wasiwasi kwa wanandoa kuanza kutumia dawa hiyo pamoja majumbani mwao. "Wameanzisha dawa aina ya Option B+ bila kuzingatia kuwa kuna watu wengine wenye VVU majumbani ukiachia mama wajawazito na wanaonyonyesha," aliiambia IPS. "Wanaume pia wanahitaji dawa hizo." Vikundi vya majadiliano vilibainisha hatari ya kuanza kwa unyanyasaji majumbani kutokana na kukosekana kwa usawa wa tiba. Wasiwasi mwingine ni kuwa madawa ya ARV yanaisha katika akiba na yanategemea wafadhili zaidi. Uganda ina mipango ya kuhakikisha watu wapatao 240,000 wanapata tiba ifikapo mwaka 2014, Musa Bugundu, mratibu wa UNAIDS nchini humo aliiambia IPS. "Kati ya hawa, watu 190,000 watapata madawa kutokana na msaada wa kifedha kutoka Marekani na wanaobaki 50,000 kutoka Mfuko wa Kimataifa," alisema. "Je hiyo ndiyo njia ya kufuata? Tuna tatizo kubwa." Proscovia Ayo, wa Jukwaa la Mitandao ya Watu Wanaoishi na VVU Tororo mashariki mwa Uganda, anasema kuwa kuanza kutumika kwa dawa hiyo kunapuuzia matakwa ya uzazi wa mpango kama sehemu ya PMTCT. "Unamkuta mwanamke anajifungua mtoto kila baada ya miaka miwili, wakati huo huo anatumia tiba ya ARV. Tulidhani Option B+ ingetatua tatizo hilo, lakini haijatatua," alisema. Baadhi ya wakosoaji wanasema Option B+ inaweza kuwa kichocheo cha kupata mimba ili kupata madawa matatu kwa ajili ya tiba ya kila siku. Shafik Malende, mtafiti katika utekelezaji wa Option B+ katika wilaya ya kaskazini ya Gulu, aligundua kuwa inahitaji ushirikiano mkubwa wa kifamilia.

"Ushirikishwaji wa wanajamii utaweza kwa kiasi kikubwa kukuza Option B+ kwasababu watahakikisha wanazingatia matumizi na kufuatilia dozi," alisema Malende. Utafiti uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mulago mjini Kampala mwishoni mwa mwaka 2012 uligundua kuwa kati ya wanawake 190 wanaotumia Option B+, ni asilimia 20 walichukua matokeo ya vipimo vya hesabu za CD4 zao. "Kiwango kikubbwa cha kutokufuatilia kuna maana kuwa kuongezeka kwa hatari ya kushindwa kwa tiba, usugu wa dawa na kuendelea kwa ugonjwa kwa wanawake," Namutamba alielezea. Madai haya yanashughulikiwa wakati mpango huo ukitekelezwa nchini kote, Godfrey Esiru aliiambia IPS. Kwa sasa, kila kliniki inapewa simu ya kiganjani kufuatilia wanawake waliopo katika tiba. Alikubaliana na baadhi ya madhaifu ya ushiriki wa wanaume, lakini aliongeza kuwa kuendelea kutumika kwa timu za afya za vijiji na vikundi vya wanawake kutahamasisha wanaume kuunga mkono wake zao. Moja ya faida za Option B+ ni kuwa wanawake wajawazito wenye VVU wanaingizwa katika tiba bila kuhesabiwa CD4. "Tusingeweza kwenda kwa kasi kwa kupima idadi ya CD4 kwani hatuna mashine za kutosha," Esiru alielezea.

Hata hivyo, ukiangalia zaidi ya kuzaliwa kwa watoto, wanawake wanaotumia tiba hiyo watahitaji kupimwa mara kwa mara CD4 ili kufuatilia afya zao. Mwanaharakati Augustine Sebuma, ambaye ameishi na VVU kwa miaka 20, alishangaa jinsi wafanyakazi wa afya watafuatilia wanawake wanaotumia Option B+ wakati kliniki hazina mashine za kupima idadi ya CD4. "Tunaunga mkono kwa kiasi kikubwa dawa ya Option B+," inasomeka taarifa ya ICWEA. "Lakini tuna mashaka makubwa kuhusu changamoto mbili za mapema, kushindwa kufuatilia na ushirikishwaji mdogo wa jamii, kitu ambacho kitapelekea uhitaji mdogo wa huduma hii." (END/2014)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2018 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.