Inter Press Service News Agency
Wednesday, September 19, 2018   22:14 GMT    

:
Hofu ya Kupima Virusi vya Ukimwi kwa Vijana wa Zimbabwe


Na Jeffrey Moyo


Natalie Mlambo* mwenye umri wa miaka kumi na saba ana sababu mbili muhimu za kupima Virusi vya Ukimwi (VVU). Ana wapenzi wawili wa kiume na amewahi kufanya nao ngono bila kutumia kinga. Mmoja ni mwanafunzi mwenzake katika darasa la sekondari. Mwingine ni mtu mzima, anafanya kazi benki na ana uwezo wa kumpatia Mlambo zawadi ndogo ndogo na fedha.

HARARE, Jan 13, 2014 (IPS) -
"Ndiyo, huwa nalala nao wote wawili," Mlambo anaiambia IPS. Na, tangu aanze kufanya nao ngono, wameshaacha kutumia kondomu. Lakini Mlambo ana wasiwasi anaweza kuwa ameambukizwa na hivyo kuhofia kupima VVU. "Naogopa," alisema. "Ni vema kubakia gizani kuliko kujua kuwa nakabiliwa na kifo; tiba haiondoi ugonjwa huo." Mlambo, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho sekondari kutoka kitongoji cha watu wengi mjini Harare cha Kuwadzana, siyo kwamba yupo peke yake katika kufanya mapenzi na wanaume wengi au kufanya mapenzi ili kupewa kitu, wala ambaye anaogopa kupima VVU. Felicia Chingundu, mwanaharakati katika shirika la kutoa misaada ya Ukimwi la Shingai-Batanai mjini Masvingo, mji uliopo kilomita 300 kusini mashariki mwa Harare, anaona vijana wengi wakikataa kupima kila siku. "Vijana wanashiriki katika tabia hatarishi za kufanya ngono lakini ni vigumu mno kuona wanakwenda kwenye vituo vya upimaji," Chingundu aliiambia IPS. Zimbabwe ilianzisha programu kabambe ya kuzuia maambukizi mapema miaka ya 1990 ambayo inasifiwa kwa kupunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 24 mwaka 2001 moja ya viwango vya juu kabisa duniani hadi chini ya asilimia 15 mwaka 2012, kwa mujibu wa Shirika la UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS). Pamoja na kwamba mlolongo wa migogoro ya kiuchumi na kisiasa baada ya mwaka 2000 ilizorotesha mipango mingi, uelewa wa Ukimwi umeenea. Moja ya matokeo ni kwamba zaidi ya nusu ya vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 wana ufahamu wa kutosha wa Ukimwi, kwa mujibu wa Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (DHS) wa mwaka 2011 kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya wastani. Hata hivyo, maarifa peke yake hayawezi kutafsiriwa katika vitendo. Wizara ya Afya imeanzisha miundombinu ya kupima inayohama hama ambayo inatembelea shule na vituo vya kupima katika kliniki. Lakini vijana wanasema vituo hivyo siyo rafiki kwa vijana. "Vijana wengi hawaji maeneo haya, wanasema yamejaa watu wazima," alisema Mavis Chigara, mratibu wa Mtandao wa Ukimwi wa Vijana katika wilaya ya Mwenezi katika jimbo la Masvingo nchini Zimbabwe. Mwaka 2012, shirika lake lilifanya utafiti wa vijana 12,500 katika wilaya; na ni asilimia tano tu walikuwa wamepima VVU.

"Kupima VVU ni sawa na kutafuta kibali cha kifo, na kutumia ARVs ni mzigo wa maisha yote," alisema Terrence Changara, 19, kutoka kitongoji cha kipato cha chini mjini Harare cha Highfield. Unyanyapaa nao unachangia. Pamoja na kuenea kwa ugonjwa na programu nyingi za tiba na kampeni za kusambaza taarifa, bado ubaguzi unaendelea. "Wapenzi wangu wawili wa kiume wanatania watu wanaoishi na VVU/Ukimwi," alisema Mlambo. Mtizamo wao unaonyesha kuwa wenyewe hawawezi kupata ugonjwa huo, alielezea.

Utafiti wa mwaka 2011 wa DHS ulikuta kuwa kiwango cha maambukizi cha karibu asilimia nne kwa vijana wa kiume na asilimia sita kwa vijana wa kike. Sensa inakadiria kuwa kuna vijana milioni 3.1 wenye umri kati ya miaka 15-24 nchini. Faida za kupima Kupima kunaweza kuogopesha, na kuelezea kwa mshauri nasaha kuwa nilifanya ngono isiyokuwa salama kunaweza kumfanya mtu kuhisi vibaya, lakini faida zake ni nyingi. "Ni muhimu kwa vijana kujua hali zao za VVU kwasababu kutawawezesha kuanza tiba mapema na kuboresha afya zao," alisema Judith Sherman, mtaalam wa VVU/Ukimwi katika Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa nchini Zimbabwe. "Kwa vijana wenye umri mkubwa kidogo, itaondoa hatari ya kuambukiza virusi kwa mtu mwingine," aliongeza. "Mwisho wake, inasaidia vijana ambao hawana VVU kujilinda wasiambukizwe." Pamoja na hofu, wanne kati ya watoto wa kike 10 katika umri wa kufanya ngono kati ya miaka 15-19 wameripoti kupima VVU katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, kwa mujibu wa DHS. Lakini sababu moja kubwa ya mara kwa mara ya kupima ni kwamba watoto wa kike walipata mimba na wanahudhuria kliniki. "Kujipeleka kupima kwa vijana ni jambo la nadra sana," alisema Mandy Chiwawa, mshauri nasaha wa masuala ya Ukimwi mjini Harare. "Kwa kweli wanahitaji msaada." Hata hivyo, watu wengi wenye umri kati ya miaka 15-24 wanapima, ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2006 za DHS. Asilimia ya vijana wa kiume wanaofanya ngono ambao walipima iliongezeka mara tatu hadi asilimia 23, wakati wanawake iliongezeka mara tano hadi asilimia 45. Hii ni idadi kubwa kuliko wastani wa ukanda wa asilimia 22 kwa wanawake na asilimia 14 kwa wanaume. Bado kuna safari ndefu kusaidia akina Mlambo ambao wanahitaji kuondokana na hofu, lakini hali inatia tumaini. *Siyo jina halisi. (END/2014)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2018 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.