Inter Press Service News Agency
Wednesday, December 19, 2018   00:13 GMT    

:
Kuhakikisha Ng’ombe na Mbuzi Wanaboresha Maisha ya Wakenya


Na Miriam Gathigah


"Hiyo ni sauti ninayoipenda zaidi katika dunia," Hussein Ahmed anasema wakati kengele iliyofungwa kwenye ng’ombe ikianza kugonga wakati wakirejea nyumbani. Ahmed, mfugaji katika wilaya ya Marsabit katika eneo kame kaskazini mwa Kenya, alipoteza wanyama wake wote mwaka 2011 wakati wa moja ya ukame mkubwa kuwahi kutokea katika ukanda huo katika kipindi cha miaka 60.

NAIROBI, Jan 13, 2014 (IPS) -
Wakati huo, Ahmed alisafiri kwenda nchi jirani ya Ethiopia kutafuta maji na malisho kwa ajili ya ng’ombe wake. "Nilikuwa nawakimbia wezi wa ng’ombe wenye silaha ambao walifika na kuiba wanyama ambao waliachwa na ukame. Wakati wa safari ya umbali wa kilomita 250 kutoka Marsabit hadi Ethiopia nilipoteza ng’ombe wangu wote kutokana na kukosa malisho na maji. Alirejea Marsabit mwezi mmoja baadaye, akiwa hana kitu. Lakini kiongozi wa ukoo, ambaye alisaini bima ya wanyama, alimpatia Ahmed mbuzi watano na ng’ombe mmoja ili kuanza tena. Maisha ni tofauti sasa. Ahmed amerejesha wanyama wake na ana ulinzi, hata kukiwa na ukame na wezi wa wanyama. Mwaka uliopita alisaini bima ya mifugo kama aliyokuwa nayo mkuu wa ukoo wake – bima ya kwanza kuwahusu wafugaji nchini Kenya, ambayo inatolewa na NGO ya International Livestock Research Institute (ILRI). "Nilijiunga mwaka 2012, na tangu kipindi hicho nimekuwa nikilipwa kutokana na kupoteza mifugo mara mbili, ikiwa ni pamoja na Machi mwaka jana," Ahmed anasema. Bima hiyo imepatiwa ruzuku na washirika wa ILRI: Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza, Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Australia. Katika kipindi cha kwanza bima ilikuwepo katika wilaya ya Marsabit pekee. Lakini mwezi Agosti ilianza kutekelezwa kaskazni mwa nchi katika maeneo ya Isiolo na Wajir. Na kutokana na mafanikio yake katika taifa la Afrika mashariki, kwa sasa inafanyiwa majaribio katika eneo la Borana, na maeneo ya ukame kusini mwa Ethiopia. Kwa ILRI, wafugaji 4,000 au nusu yao kaskazini mwa Kenya wamepatiwa bima. Hata hivyo, ni vigumu kuthibitisha idadi ya jumla ya wafugaji katika ukanda huo. Teresia Njeri, ofisa mazingira kaskazini mwa Kenya, aliiambia IPS hii inatokana na "wafugaji kutokukaa katika eneo moja kwa muda mrefu, wanasafiri mara kwa mara." Wafugaji wana jukumu kubwa katika ukanda. Kwa mujibu wa wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi ya Kenya, wastani wa thamani ya sekta ya mifugo nchini ni dola milioni 800. Benki ya Dunia inaonyesha kuwa Kenya ina pato la taifa la jumla ya dola bilioni 37. Na Mamlaka ya Maendeleo ya Serikali za Mashariki mwa Afrika, inakadiria kuwa zaidi ya asilimia 90 ya nyama inayotumiwa Afrika Mashariki inatokana na jumuiya ya wafugaji. Lakini siku zote maisha ya wafugaji yamekuwa magumu. Issa Salesa, mfugaji huko Isiolo, anaiambia kwa IPS kuwa mara zote wana maisha duni. "Mara nyingi ukame unatupiga kaskazini mwa Kenya kuanzia Juni hadi Disemba na unazidi kati ya mwezi Januari hadi Aprili, kwa hiyo kimsingi wafugaji na wanyama wao wanakuwa hatarini kufa njaa na kushambuliwa na wezi wa ng’ombe mwaka mzima," Salesa anasema. Lakini kwa sasa Ahmed na Salesa, kama ilivyo kwa maelfu ya wafugaji katika wilaya zao ambao wamesaini bima, wanatambua kuwa kama wanyama wao watakufa na ukame, watapata fidia. Na hii ina maana kuwa familia ya Ahmed itapata chakula mwaka mzima na watoto wake wanaweza sasa kwenda shule. Yusuf Aden, mfugaji wa Marsabit na mmoja wa wanaofadika na bima, aliiambia IPS kuwa wafugaji wanapaswa kuhakikisha angalau moja ya kumi ya mifugo yao imechanganya wanyama mbalimbali. "Kwa mfano, mbuzi 10 na unalipa bima ya kiasi cha dola 20 kwa mwaka. Hii gharama inawezekana kwasababu tunauza mbuzi mmoja tu kupata fedha za kuhakikisha unawekea bima mbuzi 10," Aden alisema. "Bima ina lengo la kutoa fidia kama kutatokea kupoteza mifugo, lakini ikilinganishwa na bima za kawaida, ambazo zinalipa kutokana na kiasi mtu ambacho amepoteza, bima hii ya mifugo inalipa watu kulingana na viashiria vya nje, kama vile upatikanaji wa malisho," Andrew Mude, ambaye anahusika na bima ya mifugo katika mradi wa ILRI, aliiambia IPS. Alielezea kuwa takwimu za satelaiti zinatoa wastani wa upatikanaji wa malisho na kuna sera ya malipo wakati uhaba wa malisho unapotabiriwa kusababisha vifo vya wanyama katika eneo fulani. Mifugo iliyowekewa bima inalipiwa fidia ya zaidi ya asilimia 15 ya hasara ya mifugo. Lakini faida kwa maisha yao ni kubwa mno. "Kaya zilizowekewa bima zilishuhudia kushuka kwa asilimia 33 katika uwezekano wa kupunguza lishe zao, asilimia 50 ya kushuka kwa uuzaji mifugo wa bei nafuu na asilimia 33 ya kutegemea chakula cha misaada," Mude alisema. Hata hivyo, hakuna uhakika kama aina hii ya bima itaenea katika maeneo mengine ya Kenya. Mtaalam wa bima Beatrice Wambui anasema kuwa "kuwekea bima mifugo hakuna faida kibiashara." "Kuweka bima za majanga ya asili ni biashara hatari sana, huna udhibiti wa hali ya hewa … Lakini katika maeneo ambayo bima ya mifugo inafanya kazi, na kama makampuni yanaweza kupata njia za shinda nishinde na wafugaji, aina hii ya bima inaweza kubadili maisha," Wambui aliiambia IPS, akiongeza kuwa kama makampuni ya bima hayatashirikiana na NGOs hayataweza kufikia wafugaji. Alisema kuwa wakati makampuni ya bima yalikuwa yakianza kuzingatia kuanzisha bima za namna hiyo, walikuwa wakiingia huko kwa "kiwango cha chini sana na hawako tayari kujitangaza." "Baadhi wanafanya kazi na wateja wachache kama vile 50 tu kuona kama inafanya vizuri katika kipindi cha mwaka," Wambui anasema. Njeri anasema kuwa wakati bima ya ILRI ilikua ikiboresha maisha na usalama, inapaswa kufikia watu wengi zaidi. Wafugaji kutoka wilaya za Samburu, Turkana, Pokot na Marakwet kaskazini mwa Kenya bado wanabakia katika hatari ya kupoteza vyanzo vya riziki zao kutokana na wezi wa ng’ombe – lakini bado bima haipo katika maeneo hayo. Moses Lentoimaga ni mfugaji toka Samburu na anaishi kwa hofu kutokana na wezi wenye bastola. Wezi walishambulia kijiji Oktoba 18 na kuua majirani zake watano na kuiba ng’ombe 1,000. Yeye pia anahitaji usalama ambao wanao Ahmed na Aden. "Kabla ya kwenda kwa majirani zetu nchini Ethiopia, kwanza wanatakiwa kuja kutuokoa," Lentoimaga aliiambia IPS (END/2014)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2018 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.