Inter Press Service News Agency
Thursday, August 13, 2020   09:15 GMT    

Tanzania:
Imepiga Hatua Katika Kuendeleza Hifadhi na Maeneo Tengefu ya Bahari


Na Marko Gideon


Mara nyingi watu wanaposikia neno hifadhi, mawazo yao moja kwa moja hukimbilia kwenye hifadhi za taifa zilizopo nchi kavu kama vile Mbuga za Wanyama za Serengeti, Ngorongoro, Mikumi na nyinginezo. Lakini ni nadra mno kusikia watu wakitaja hifadhi zinazopatikana katika bahari.

DAR ES SALAAM, Aprili 19 (IPS) -
Wakati hali ikionyesha hifadhi za bahari kutokuwepo akilini na midomoni mwa watu wengi,Tanzania inajulikana kuwa miongoni mwa mataifa duniani ambayo yamejizolea sifa kubwa katika kusimamia vizuri hifadhi za bahari.

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ni nini? Kwa Mujibu wa Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Dk. Adilian Chande, kitengo hicho kilikuwa chini ya Idara ya Uvuvi, kwa mujibu wa sheria ya Maeneo Tengefu ya Bahari Na. 29 ya mwaka 1994. Kutokana na kwamba kwa sasa Sekta ya Uvuvi imegawanyika katika idara mbili Ufugaji wa Samaki na Maendeleo ya Uvuvi, kitengo sasa kipo chini ya Idara ya Maendeleo ya Uvuvi. "Hivyo sheria iliyounda kitengo kwa sasa ipo redundant (imepitwa na wakati), kwani idara ya Maendeleo ya Uvuvi haijatajwa kwenye sheria ya wakati huo, na sasa tupo katika mchakato wa kurekebisha sheria", alisema Dk Chande.

Akizungumza mwaka jana wakati wa kupokea ujumbe wa watendaji wa Mradi wa Kuhifadhi Mazingira ya Ziwa Victoria (LVEMP) uliokuwa kwenye ziara ya kujifunza kutoka kwenye miradi inayotekelezwa kuhifadhi mazingira ya ukanda wa pwani na hasa Mradi wa Pwani wa Mpango wa Kusimamia Mazingira ya Ukanda wa Pwani (TCMP) unaofadhiliwa na USAID, Dk Chande alisema kitengo kilianzishwa baada ya idara kugundua kuwa kulikuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, hasa katika maeneo yenye bayoanuai kubwa na viumbe ambao ni adimu baharini kama vile nguva, pomboo, kasa, papa na wengine ikiwa ni pamoja na uoto wa asili ambapo mikoko ilikatwa ovyo na matumbawe kuharibiwa kwa kupigwa mabomu.

"Matumbawe yalivunjwa ovyo ovyo kwa kutumia mabomu, shida kubwa ni mabomu ambayo yanaangamiza matumbawe ambayo ndiyo uhai wa bahari, hakuna bahari bila matumbawe, hakuna uhai kabisa," alisema Dk Chande.

Ndipo idara ikaona kuna haja ya kuanzisha kitengo kuweza kubainisha maeneo husika ili yaweze kuhifadhiwa kwa njia mbili Hifadhi za Bahari au Maeneo Tengefu.

Kwa kutofautisha, Hifadhi ya Bahari ni eneo kubwa ambalo hata watu wanaishi ndani yake. Shughuli za eneo hilo husimamiwa na Mpango wa Usimamiaji ujulikanao kama General Management Plan, ambao, kwa mujibu wa Dk Chande, maandalizi yake yanashirikisha wadau wote.

Mpango unashirikisha wanajamii ambao wanaishi ndani ya hifadhi, halmashauri husika ambazo ziko ndani ya hifadhi, na wadau wengine ikiwa ni pamoja na wanasayansi kwa kushirikiana na uongozi wa kitengo kukubaliana kuwa baadhi ya maeneo yatengwe kabisa ambapo hakuna uvuvi wowote utakaoruhusiwa, kutenga maeneo ya matumizi ya jumla ambapo uvuvi unaruhusiwa kwa wavuvi wa ndani na nje ya hifadhi na maeneo ya matumizi maalum ambayo pamoja na kwamba wavuvi wa ndani ya hifadhi wanaruhusiwa kuvua kwa kutumia zana maalum zinazoruhusiwa kisheria, wavuvi wa nje hawaruhusiwi kabisa kuvua katika maeneo hayo.

Kwa upande mwingine, maeneo tengefu ni maeneo madogo madogo ya visiwa ambayo yanazungukwa na matumbawe. Katika maeneo haya watu hawaruhusiwi kuishi wala matumizi ya rasilimali hayaruhusiwi. Shughuli zinazoruhusiwa katika maeneo hayo ni zile zinazohusiana na utalii tu. Kwa mujibu wa Dk Chande, maeneo hayo ni pamoja na visiwa vya Bongoyo na Mbudya mjini Dar es Salaam ambapo ndani yake kitengo kimetengeneza njia vinjari (nature trails) kwa ajili ya watalii kupita.

Je Unazijua Hifadhi za Bahari Tanzania?

Kwa mujibu wa Dk. Chande, ni mpango wa dunia nzima kuwa asilimia 10 ya maji ya bahari na maziwa yanakuwa chini ya hifadhi, na Tanzania ina asilimia 4.5 tu ya hifadhi. Alisema kama kitengo chake kitaingia katika kuanzisha hifadhi kwenye maji ya ziwa, anatarajia asilimia hiyo itaongezeka hadi 7 na hivyo nchi kupiga hatua kubwa.

Asilimia hiyo 4.5 inahusisha hifadhi za bahari 3 na maeneo tengefu 15. "Tuna Hifaddhi za Bahari 3 nchini Tanzania," alisema Dk Chande.

Akizitaja kwa majina, alisema hifadhi ya kwanza ni ile ya kisiwa cha Mafia katika mkoa wa Pwani ambayo ilianzishwa kati ya mwaka 1995/96. Hifadhi hii ina ukubwa wa kilomita za mraba 822.

"Katika hifadhi hii huwezi kusikia bomu linalia kwani tumeshadhibiti hali na wananchi wengi wameshakuwa na uelewa na hivyo kusaidia katika kazi za uhifadhi," alisema, na kuongeza kuwa pia wananchi wanafaidika kutokana na kuongezeka kwa utalii katika eneo hilo.

"Kuna geti la kuingilia kwenye hifadhi na kiingilio ni dola 20. Kila mwaka wanakijiji wanapata asilimia 20 na halmashauri asilimia 10 ya mapato yatokanayo na utalii", alibainisha, na kuongeza kuwa kila mwaka wanakijiji wanaandaa mpango wao wa shughuli za maendeleo ambao unapitishwa na halmashauri husika. Mpango huo unabainisha vijiji vya kufaidika na fedha za hifadhi mwaka hadi mwaka na unaweza kuhusisha shughuli za uchimbaji visima, kujenga zahanati, madarasa na shughuli nyingine.

Pia kitengo hicho kinasomesha baadhi ya watoto wa wanajamii katika hifadhi katika kiwango cha elimu ya sekondari ili kuhamasisha jamii hizo kupenda kupeleka watoto wao shule.

"Kwa hiyo wameona faida ya hifadhi, ila hapo kabla walikuwa hawajaelewa," alisema Dk Chande. "Wameona umuhimu wa kutunza hizi rasilimali. Hakuna mwananchi wa Mafia ndani ya hifadhi ambaye sasa anapenda kusikia bomu."

Hata hivyo, kwa mujibu wa Dk Chande, kuna aina ya uvuvi wa kutumia nyavu za mitando ambazo haziruhusiwi kutokana na kuwa na macho madogo. Uvuvi huu bado unatumika katika vijiji viwili kwenye hifadhi ya Mafia. Lakini, alisema kitengo chake kinafanya jitihada za kudhibiti uvuvi huo. Hifadhi ya pili ni ya Mnazi Bay ambayo imeanzishwa mwaka 2000. Hifadhi hii inahusisha eneo lenye gesi la Mnazi Bay na ina ukubwa wa kilomita za mraba 650. Hapa uvuvi haramu ni mkubwa kutokana na kuwepo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji katika mkoa wa Mtwara.

"Doria imekuwa ngumu kutokana na kuwa wavuvi haramu wanapofukuzwa upande mmoja wa nchi wanakimbilia upande mwingine," alisema Dk Chande, akiongeza kuwa, hata hivyo hali imeweza kudhibitiwa baada ya kuongeza nguvu ya doria katika hifadhi hiyo.

"Kwa sasa hali imekuwa nzuri, ilibidi usimamiaji wa sheria uwe mkali zaidi ili kupunguza upigaji wa baruti na wavuvi haramu wamepungua kwa kiasi kikubwa," kwa mujibu wa Dk. Chande.

Hata hivyo, anasema bado kuna vijiji viwili ambavyo vinasumbua katika kuendesha uvuvi haramu kwenye hifadhi hiyo. "Lakini wamekuja wenyewe na kujisalimisha kwa Mkuu wa Wilaya na kula kiapo mbele ya mwanasheria mkuu wa serikali wakiahidi kuwa hawatarudia tena vitendo vyao vya uvuvi haramu," alisema Dk Chande. "Pia tumewaanzishia vikundi vyao vya doria ili wao wenyewe washiriki katika kusimamia hifadhi".

Akifafanua zaidi juu ya hifadhi hiyo, Dk Chande alisema ina rasilimali nyingi na vivutio viko vingi ikiwa ni pamoja na msitu mkubwa wa mikoko ambao usingekuwa katika maji hata wanyama wakubwa wangeweza kuishi humo. Pia kuna maingilio ya Mto Ruvuma ambayo yana viboko wengi na kuanzia mwezi wa nane kuna mapitio ya nyangumi. Watu wanavutiwa kuangalia nyangumi wakipita. Na ili kukuza utalii wa kuangalia nyangumi, ofisi ya hifadhi sasa imejengwa katika mapitio ya nyangumi. Ni kivutio kikubwa.

Pia kuna viota vya kasa ambavyo vinavutia watalii wengi wakati wa kuanguliwa kwa kasa na kuna vivutio vya matumbawe.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Dk. Chande, utalii wa eneo hilo unakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa miundombinu. "Vivutio viko vingi lakini utalii bado haujakua kutokana na kukosekana kwa miundombinu. Barabara yetu ya Kibiti hadi Lindi haijaisha, hata usafiri wa kutoka (Mtwara) mjini kwenda eneo tulilojenga ofisi kilomita 45 ni barabara mbaya ambayo inahitaji uwekezaji," alielezea Dk Chande.

Hata hivyo, kuna watalii ambao wanapita vikwazo hivyo vyote kutokana na kupenda kufikia vivutio adimu vinavyopatikana katika hifadhi hiyo.

Hifadhi ya tatu ni ile ya Tanga Coelacanth ambayo ilianzishwa mwaka 2009 ambayo ina ukubwa wa kilomita za mraba 552. Ilianzishwa kwa shinikizo la Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na umuhimu wake wa kuwepo kwa samaki adimu duniani aina ya silikanti (Coelacanth). Pia ni kutokana na wananchi wenyewe wa Tanga ambao tayari wamehamasika kutunza mazingira na hivyo kuwasukuma kufika kwenye kitengo kuomba kuanzishwa kwa hifadhi.

Mbali na samaki aina ya silikanti, vivutio vingine vinavyopatikana katika hifadhi ya Tanga ni pamoja na matumbawe, kasa na ni eneo lenye samaki wengi.

"Kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa hivi wananchi wenyewe wameanza kushuhudia kuwa samaki wameongezeka kwa kiasi kikubwa," alisema Dk Chande.

Maeneo tengefu

Kuna maeneo tengefu 15 nchini Tanzania huku Dar es Salaam pekee ikiwa na maeneo tengefu 7 ambayo yanapatikana upande wa kaskazini na kusini. Kwa upande wa kaskazini kuna kisiwa cha Bongoyo, Mbudya na eneo tengefu la fungu la mchanga lijulikanalo kama Fungu Yasin na Pangamin. Maeneo haya tengefu yalianzishwa kabla ya kitengo hakijaanza mwaka 1975 wakati Idara ya Uvuvi ilipokuwa inaanza. Maeneo hayo yalipitishwa kwa kutumia sheria ya Idara ya Uvuvi. Visiwa vya kusini ni pamoja na kisiwa cha Finda, Kenda na Makatobe ambavyo vimeanzishwa na Kitengo cha Hifadhi za Bahari.

Ukiacha Hifadhi ya Bahari, Mafia pia ina maeneo tengefu katika visiwa vya Shungimbili, Nyororo na Mbarakuni.

Kwa upande wa Tanga, kuna kisiwa cha Maziwe katika wilaya ya Pangani. Hiki kilipitishwa mwaka 1975 kuwa eneo tengefu ambapo wakati huo kilikuwa ni kisiwa. Lakini sasa kutokana na uharibifu wa mazingira, kimegeuka na kuwa fungu la mchanga. Kisiwa hiki kina mazalia makubwa ya kasa ambapo kuna utalii mkubwa unaoendelea wa kushuhudia jinsi kasa wanavyoanguliwa katika fukwe za Ushongo na Kikokwe.

Maeneo mengine tengefu yanaanzia Tanga mjini kwenda mpakani mwa Kenya. Maeneo hayo ni pamoja na Mwewe, Kilui, Ulenge na Kwale. Kisiwa cha Kilui kiko mpakani kabisa mwa Kenya. Hali hii imesababisha kitengo kuona haja ya kuanzisha usimamiaji wa pamoja wa maeneo tengefu na nchi za jirani. Hii itasaidia kudhibiti uvuvi haramu na kuhifadhi viumbe wanaohama kama vile kasa.

Tofauti ya Hifadhi za Bahari na Hifaddhi za Taifa

Kuna tofauti kati ya Hifadhi za Bahari na Hifadhi za Taifa zilizopo chini ya Mamlaka ya Kusimamia Mbuga za Taifa Tanzania (TANAPA).

Wakati hifadhi zinazosimamiwa na TANAPA haziruhusu wanajamii kuishi katika hifadhi za taifa, kitengo cha kusimamia hifadhi za bahari kinaruhusu wanajamii kuishi ndani ya hifadhi.

Kwa mujibu wa Dk. Chande, mpangilio huu unafanya kazi ya kuwashirikisha wanajamii katika uhifadhi kuwa rahisi zaidi. Mafanikio ya Hifadhi na Maeneo Tengefu ya Bahari

Moja ya mafanikio ni kuongezeka kwa akiba ya samaki baharini na kuhifadhiwa kwa rasilimali na viumbe bahari walio katika hatari ya kutoweka kama vile mikoko, matumbawe, kasa, nguva, silikanti n.k.

Pia kuna ongezeko la utalii katika maeneo ya hifadhi. "Tunajaribu kuhamasisha utalii," alisema Dk Chande.

"Pamoja na kuwa lengo letu la msingi ni kuhifadhi mazingira, lakini baada ya kuhifadhi, mahitaji ya uwekezaji katika utalii yanazidi kuongezeka."

Changamoto za kuendeleza Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu

Changamoto kubwa ya kusimamia Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ni ulipuaji wa mabomu kutokana na kuongezeka kwa samaki katika maeneo hayo.

"Tunapata shida sana na uvuvi haramu katika maeneo hayo, baada ya kuyatunza samaki wamekuwa wengi wengi sana, kwa hiyo wahalifu wakilipua bomu na samaki kuelea wanachota samaki wengi. Kazi kubwa ni kusukuma utekelezaji wa sheria kwa kufanya doria za mara kwa mara ambazo ni za gharama kubwa. Hii kwa kiasi kikubwa imepunguza uvuvi haramu," alisema Dk. Chande. (END/2012)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2020 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.