Inter Press Service News Agency
Thursday, April 26, 2018   10:38 GMT    

KENYA:
Walimu Wa Shule za Msingi Wapata Matokeo Mabaya Kwenye Hisabati


Na David Njagi


Kama ilivyo kwa walimu wengi wa shule zote za msingi nchini Kenya, Nemwel Mokua amechanganyikiwa. Anatakiwa kufundisha kwa uchche masomo sita kwa siku, ambayo ni pamoja na mchanganyiko wa masomo ya sanaa na sayansi.

NAIROBI, Sep 14, 2010 (IPS) -
Ana muda mchache wa kuendeleza uelewa wake wa masomo magumu ya hisabati na sayansi. Na matokeo yake, wanafunzi wake wanapata alama za chini katika masomo hayo.

Na mwalimu wa Shule ya Misngi Le Pic huko Riruta, Nairobi, anaishi kwa hofu ya kukaguliwa kwa shule yake na wakaguzi, ambao mara nyingi wanamkaba koo yeye na wafanyakazi wenzake kuhusu matokeo mabaya ya shule yake katika masomo ya hisabati na sayansi. Mwaka 2008, wanafunzi wa shule anayofundisha Mokua walipata wastani wa daraja D+ katika mitihani yao. Hata hivyo, kulingana na matokeo ya Cheti ya Elimu ya Msingi Kenya 2008 huu pia ni wastani wa wanafunzi wengine katika nchi nzima.

Kama ilivyo kwa walimu wengi wa shule za msingi nchini Kenya, Mokua anahusisha matokeo hayo mabaya ya wanafunzi wake na muda mdogo anaopata kuwekeza katika hisabati na masomo ya sayansi.

"Pamoja na kwamba wanafunzi wangu wameboreka zaidi katika hisabati katika miaka miwili iliyopita, lazima nikubali kuwa mfumo wa elimu nchini Kenya unaweka kazi kubwa kwa walimu. Hana muda wa kuwekezaji katika masomo ya kiufundi," alisema Mokua.

Lakini wizara ya elimu inasisitiza kuwa walimu wa shule ya msingi ni lazima kufundisha kwa uchache masomo sita kwa siku. Lakini wataalam wa elimu wanasema hii inapingana na ubora wa elimu katika shule za msingi Kenya. Na utafiti uliotolewa Agosti 25 unaunga mkono maoni ya wataalam.

Utafiti wa "Classroom Observation" mjini Nairobi uliotolewa na Kituo cha Utafiti wa Wakazi wa Afrika, unaonyesha kuwa walimu wa hisabati katika shule za msingi nchini Kenya wana uelewa mdogo wa somo hilo. Na watafiti wamehoji ubora wa mfumo wa elimu ya msingi nchini humo.

Matokeo ya ripoti hiyo yalishtua Wakenya baada ya walimu kupata wastani wa asilimia 60.5 katika matokeo ya majaribio ya hisabati.

Watafiti walisema wangetarajia walimu walioshiriki katika utafiti kupata zaidi ya asilimia 90 katika somo hilo, lakini ni kiasi cha asilimia 13 tu kiliweza kutofautisha ufaulu wa walimu na wanafunzi.

Katika tukio moja, mwalimu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka mitano alipata asilimia 17 katika majaribio. Mtafiti mwandamizi wa APHRC, Dk. Moses Oketch, alielezea matokeo hayo kama ‘ya aibu’.

"Matokeo yalitushtua mno," alisema Oketch. "Tulitarajia walimu kupata maksi zaidi ya asilimia 90, lakini matokeo yao yanakaribiana kufanana na ya wanafunzi, ambao wastani wao ni asilimia 46.89. Kuna jambo ambalo linahitaji kufanyika hapa."

Kulingana na watafiti, matokeo mabaya pia yanaweza kuelezea ni kwa nini wanafunzi wanafanya vibaya katika somo hilo.

Lakini Peter Githinji, mwalimu wa hisabati katika Shule ya Msingi ya Gikandu katikati mwa Kenya alisema walimu wanatakiwa wasilaumiwe kwani serikali imeshindwa kuwapatia vifaa vya kufundishia ambavyo vingeweza kurahisisha masomo ya hisabati na sayansi.

"Kuna mtizamo uliojengeka nchi nzima kuwa hisabati na sayansi ni masomo magumu," alisema Githinji. "Nadhani serikali haijafanya kazi ya kutosha kuhamasisha Wakenya kukubali masomo hayo."

Lakini ripoti imesababisha mjadala unaoendelea, huku vyama vya walimu vikilaumu serikali kutokana na kushindwa kufundisha walimu wa kutosha waliobobea katika masomo ya hisabati na sayansi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Msingi Njeru Kanyamba alisema wakati Kenya ilipozindua mpango wa elimu ya msingi kwa wote mwaka 2003, pia iliufanya bila ya kuwa na mpango sahihi wa rasilimali.

Wakati elimu ya msingi kwa wote ilipoanzishwa mwaka 2003, zaidi ya wanafunzi wapya milioni 1.3 waliandikishwa katika wiki ya kwanza. Na bado walimu walibakia kuwa wachache, Kanyamba alisema.

"Walimu wa shule ya msingi wamezidiwa na wanafunzi waliojiandikisha katika darasa moja kutokana na uhaba wa wafanyakazi," alisema Kanyamba. "Kutokana na wajibu mkubwa waliokuwa nao, hawawezi kupata fursa za kuendelea na masomo yao."

Anakubaliana kuwa matokeo ya ripoti hiyo yataathiri maendeleo ya sayansi na teknolojia ya baadaye.

Katibu Mkuu wa wizara ya elimu, Profesa James Ole Kiyiapi, alitetea mpango wa elimu kwa wote akiongeza kuwa mfumo wa elimu ya juu nchini Kenya umejikita katika mfumo wa ongezeko la thamani ambapo wanafunzi wameweza kuonyesha mafanikio katika sayansi na teknolojia katika ngazi hii. (END/2010)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2018 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.