Inter Press Service News Agency
Saturday, June 23, 2018   07:16 GMT    

KENYA:
Ufugaji wa Vipepeo Waleta Chakula Mezani


Ntandoyenkosi Ncube


Kwa miaka 10, Roselyne Shikami, alikuwa akiuza mayai ya kuchemsha katika kituo cha mabasi nje ya msitu mnene wa Kakamega magharibi mwa Kenya, karibu na mpakani mwa Uganda. Kwa sasa anauza vipepeo.

MSITU WA KAKAMEGA, Kenya, Apr 24 (IPS) -
"Ilikuwa ni vigumu mno kwangu mimi kuuza mayai ya kutosha kwa siku," mwanamke mwenye umri wa miaka 35 aliiambia IPS. "Kuna wakati nakaa hapo kwa zaidi ya masaa kumi na moja. Lakini ni mara chache naingiza shilingi 200 za Kenya (kama dola za Kimarekani 2.60). Kwa sasa nikiuza tu vipepeo viwili naingiza fedha nyingi zaidi."

Shikami ni mmoja wa wanavikundi vidogo ambavyo wanachama wake wengi ni wanawake, ambao wamenza ufugaji wa vipepeo kwa ajili ya kuviuza nchini Kenya na mahali pengine barani Afrika. Wanatarajia kupata wateja barani Ulaya na Amerika ya Kaskazini, masoko mawili yenye faida kwa biashara ya vipepeo. Mume wake, Joel, ni sehemu ya kikundi hicho. Kama ilivyo kwa wengi wanaoishi kuzunguka msitu wa Kakamega, alikuwa akiingiza kipato chake kutokana na kukata miti msituni na kuiuza kama kuni.

Kulingana na Mpango wa Elimu ya Mazingira Kakamega (KEEP), kikundi cha kuhifadhi mazingira ambacho hutoa mafunzo kwa wanawake juu ya ufugaji wa vipepeo, msitu wa Kakamega umepungua kutoka zaidi ya hekta 240,000 mwaka 1820 hadi hekta 23,000 tu leo hii. Kwa ujumla msitu huo unaonekana unaofanana zaidi na misitu ya tambarare ya Kongo katika Afrika ya Kati. Ukataji mkubwa wa miti kwa kiasi kikubwa umetokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na uhaba wa ajira na kusababisha kusafisha ardhi kwa ajili ya kilimo na kuchoma mkaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kuuza.

Serikali imefanya kazi kuwafanya wakataji miti na wakulima kuondoka kutoka katika msitu huo na sasa inahamasisha miradi ya jamii kama vile ufugaji wa vipepeo, kama njia ya kuzalisha kipato mbadala.

Msitu wa Kakamega una zaidi ya asilimia 70 ya vipepeo nchini Kenya na zaidi ya aina 500 tofauti za vipepeo hao. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, ufugaji wa vipepeo umegeuka kuwa njia ya kuingiza fedha kwa wanajumuiya wanaozunguka misitu, na kuwaingizia wakulima sawa na zaidi ya dola za Kimarekani 100,000 kwa mwaka linasema shirika la Huduma za Misitu Kenya katika ripoti yake ya mwaka.

Mkurugenzi wa KEEP Benjamin Okalo anaunga mkono. "Biashara ya vipepeo inakua. "Mkulima anahitaji tu vipepeo wawili kupata mayai elfu moja na hayo yatazalisha zaidi ya shilingi za Kenya 75,000 (dola 950) kwa mwezi fedha nyingi zaidi ikilinganishwa na ambazo mtu angeweza kuingiza kwa kuuza kuku au mayai."

Okalo alielezea kuwa watu wanataka kununua aina mbalimbali za vipepeo kadri inavyowezekana kwa ajili ya kuwakusanya na kutengeneza mapambo mazuri. Vipepeo pia wananunuliwa kwa ajili ya utafiti.

"Aina ya vipepeo wanaopatikana hapa ni wazuri mno. Hoteli kubwa na watalii wanawanunua. Wafanyabiashara matajiri wameshaanza kuwanunua pia ili kupamba nyumba zao wakati wa siku maalum kama vile harusi na kwa ajili ya elimu ya watoto wao," Okalo anasema.

Anne Moraah, mfugaji mwingine wa vipepeo aliiambia IPS baadhi ya wabunifu kutoka Ulaya hutumia vipepeo kuja na ubunifu wa aina mbalimbali.

Ufugaji wa vipepeo

"Kwa biashara hii hauhitaji shamba kubwa; hauhitaji chumba kikubwa. Kila mmoja anaweza kushiriki katika biashara hii kwani unahitaji kontena dogo tu," anasema Roselyne Shikami.

Mpango mzima unahusu ujenzi wa kibanda kidogo chenye nyavu na kuweka chakula cha mimea ndani yake ili kuvutia aina mbalimbali za vipepeo. Kipepeo jike hukamatwa na kuwekwa kwenye kibanda cha kuzaliana ili kutaga mayai yake kwenye majani. Mayai huvunwa na kutunzwa hadi yanapozalisha kipepeo mchakato ambao huchukua takribani mwezi mmoja.

Ni lazima mfugaji kuwa na leseni inayotolewa na taasisi za Wanyama Pori Kenya kuuza wadudu aina ya vipepeo na wadudu wengine hai nchini Kenya na mahali pengine Afrika.

Kulingana na KEEP na viongozi wa mradi mwingine wa jamii ujulikanao kama Kipepeo, , leseni nyingine inahitajika kusafirisha nje ya nchi kwenda Ulaya na Amerika ya Kaskazini.

"Tatizo kubwa ni kwamba taasisi ya wanyamapori husita kutoa leseni kwa wafanyabiashara wa vipepeo wanaoibukia aidha kwa ajili ya uuzaji wa ndani ya nchi au kimataifa," anasema Okala.

Katika Mkutano wa Pili wa Mawaziri kuhusu Athari za Majanga na Jinsi ya Kuzipunguza uliofanyika nchini Kenya mapema mwezi huu, Afisa Mawasiliano Mkuu wa Wizara ya Misitu na Wanyamapori Kenya, Mary Ngaruma aliiambia IPS kuwa wafugaji vipepeo wanawake wanapaswa kuanzisha vyama vya ushirika na kusajili mashirika yao kabla ya kuomba leseni.

"Serikali inafaidika kutokana nao," alisema Ngaruma. "Wafugaji wa vipepeo wanahifadhi misitu yetu na kukuza uchumi wa ndani hivyo hakuna sababu ni kwa nini tusiwapatie leseni za biashara."

Faida za kimazingira

Wale wanaoshiriki katika ufugaji wa vipepeo wanasisitiza kuwa wakati biashara nyingine zinazohusiana na misitu ni za kinyonyaji, ufugaji wa vipepeo una faida kwa mazingira.

"Unapokuwa na idadi nzuri ya vipepeo ina maana kuwa mazingira ni mazuri. Kwa kuwa na vipepeo wachache ina maana kuwa kuna uchafuzi wa mazingira. Vipepeo pia huweza kuwa mwongozo wa mabadiliko ya hali ya hewa," anasema Joel Shikami.

Afisa Mtafiti Mwandamizi wa Kituo cha Kimataifa cha Saikolojia ya Wadudu na Mazingira, Lamberts Morek, anasema vipepeo ni muhimu kwa mazingira na viumbe hai kwasababu huchangia katika mazingira kutokana na kusaidia kuchanua kwa maua.

"Kama wanasayansi ndoto yetu ni kuwa na mazingira yenye afya na utajiri. Inafikiwa kwa kuwezesha wanawake hawa wafugaji wa vipepeo." (END/2010)

 
Contact Us | About Us | Subscription | Help us Improve | News in RSS
Copyright © 2018 IPS-Inter Press Service. All rights reserved.