Inter Press Service News Agency
Monday, June 18, 2018   10:56 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
SACCOS Zasaidia Kuinua Kilimo Bagamoyo
Na Marko Gideon

BAGAMOYO, Mei 28 (IPS) - "Kilimo Kwanza" ni mkakati mzuri kama utatekelezwa kwa ufanisi", alisema Salum Shamte, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kilimo Tanzania wakati wa mahojiano maalum kwa njia ya simu na mwandishi wa makala haya.

Akifafanua kuhusu mkakati huo, alisema unalenga katika kuwafanya wananchi kuendesha kilimo chenye faida na tija. Alisema Kutokana na serikali kujitoa kuendesha kilimo, itapata fursa kuwezesha kilimo kupitia kwa wananchi.

"Hivyo, kama mkakati utatekelezwa wakulima watafaidika kwa kupata mbolea kutoka serikalini, kupata mikopo ya kifedha kutoka Benki ya Kilimo itakayoanzishwa na pia kuweza kukopa pembejeo kama vile matrekta. Pia masoko yatapatikana, kwani mkakati huo pia utahamasisha sekta binafsi kufungua viwanda vitakavyotumia malighafi kutoka mashambani". Alisema Shamte.

Alisema jambo zuri la mkakati huo ni kwamba Baraza lake limeshirikisha wananchi tangu dhana yenyewe ilipoanza mwaka 2006 hadi ripoti ilipowasilishwa serikalini Juni 2009.

"Tulifanya kazi ya kukusanya maoni ya wakulima nchini kote. Tulifanya warsha kuanzia Kigoma hadi Mtwara kuchukua maoni ya wananchi," alisema akiongeza kuwa Baraza lilikuwa sehemu ya kikundi kazi ambacho kiliundwa kwa pamoja kati ya serikali na sekta binafsi kufanikisha dhana na hatimaye mkakati huo.

"Kushirikishwa kwa wananchi kunasaidia kwasababu katika mijadala walipata fursa kujua matatizo ya kilimo wanachoendesha sasa na faida ya kilimo watakachoendesha baada ya mkakati kuanza kufanya kazi," alisema na kuongeza kuwa "Kilimo cha sasa hakina faida kubwa kwao wala tija. Mkakati unasisitiza kilimo cha kisasa na chenye tija.""Ni mkakati mzuri kama utatekelezwa, utekelezaji ni msingi mkuu na pia lazima kuwepo kwa ufuatiliaji wa utekelezaji huo."

Mkakati wa "Kilimo Kwanza" ulikuwa kaulimbiu ya mwaka wa fedha 2009/2010. Akifafanua maana ya kaulimbiu hiyo wakati wa hotuba yake bungeni Juni 11, 2009, Waziri wa Fedha na Uchumi wa wakati huo, Mustafa Mkulo alisema "Hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa kilimo kinapatiwa rasilimali zaidi ikiwemo pembejeo na zana za kilimo".

Kulingana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Peter Pinda, "Ili kuutoa Uchumi wetu kutoka kwenye uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuuingiza kwenye uchumi imara, wa kisasa na endelevu tunahitaji kufanya mapinduzi katika sekta ya kilimo na viwanda. Mapinduzi haya yataongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi," alisema katika hotuba yake ya Juni 22, ya mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge mwaka 2009/20010, na kuongeza kuwa "uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka, mavuno yataongezeka na hivyo ongezeko hilo litawawezesha wakulima kunufaika kupata kipato kutokana na kuuza mazao mengi zaidi nje. Hii pia, inavutia wawekezaji kujenga viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani kutokana na mazao ya kilimo.

"Tukifanya mapinduzi hayo, tutakuwa tumetekeleza ahadi yetu ya maisha bora kwa kila Mtanzania", alisema Waziri Mkuu.

Kauli ya Waziri Mkuu iliungwa mkono na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. "Tumeamua kuzindua ‘Kilimo Kwanza’ kama azma maalum ya kitaifa ya kuongeza kasi ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini," alisema katika Tamko la Rais kwenye kijitabu cha ‘Kilimo Kwanza, Mapinduzi ya Kijani’.

Rais alifafanua zaidi kuwa kilimo kwanza kinajumuisha sera na mikakati inayolenga katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili kilimo na pia kutumia fursa lukuki zilizopo nchini. "Kwa hiyo kilimo kwanza itakua mhimili muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na itaweka msukumo zaidi katika kufanikisha malengo yetu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii".

Pamoja na maneno mazuri ya viongozi wetu je kuna rasilimali za kutosha kutekeleza mkakati wa kilimo kwanza nchini Tanzania? Jibu la swali hili linajibiwa na Rais Kikwete. "Nchi yetu yenye wakazi wapatao milioni 40 imejaaliwa kuwa na hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo lakini ni asilimia 23 tu ndiyo inayotumika."

Kwa kutambua fursa iliyopo katika kilimo, baadhi ya wanachama wa SACCOS ya Mkange ya UWAMKE (Umoja wa Wanawake Mkange) wilayani Bagamoyo wamejiingiza kwenye shughuli za kilimo baada ya kupata mtaji kutoka katika SACCOS hiyo.

"Najivunia uzuri wa shamba langu, hata nikipeleka mgeni atajua kweli nimefanya kazi yenye tija," anasema Mwanahamisi Ramadhani Kitivo. "Nilikopa shilingi milioni 2 kutoka katika SACCOS, nikalima ekari 5 za mahindi kwa kutumia trekta, na ekari nyingine 3 za ufuta," anaongeza Kitivo, mmoja wa wanawake wanaofaidika na kuwepo kwa SACCOS ya UWAMKE.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na uongozi wa SACCOS hiyo hivi karibuni, kikundi hicho kilianzishwa na wanawake wachache wa Mkange mwaka 2009 ambao walianza kama mchezo wa kibati wa kupeana pesa. Mchezo uliendelea hadi waliposikia juu ya Mradi wa Pwani wa Mpango wa Kuhifadhi Mazingira na Rasilimali za Pwani (TCMP) kuwa inasaidia kutoa misaada ya kiuchumi na elimu ya uhifadhi wa mazingira, ujasiriamali na ongezeko la kipato.

TCMP ni mpango unaofadhiliwa na Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID) na kupata msaada wa kiufundi kutoka Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Rhode, ambacho pia kipo nchini Marekani.

"TCMP kwa kushirikiana na idara ya ushirika ya wilaya ya Bagamoyo ilianza kusaidia kwa kutoa elimu ya mazingira, ujasiriamali na kujiingizia kipato kwa kikundi hicho cha wanawake," anasema Patrick Kajubili, mratibu wa kitengo cha kukuza uchumi na kujiingizia kipato katika TCMP.

Mashavu Ali, mwenyekiti wa UWAMKE na Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi katika kata ya Mkange na mmoja wa waanzilishi wa SACCOS hiyo anasema walianza na mtaji wa shilingi 100,000 ambapo walikuwa wakikopeshana watu 5 kwa awamu hadi mzunguko wa wajumbe 20 unapokamilika.

Anasema waliendelea na mpango huo ambao haukuwa rasmi ambao ulivutia zaidi idadi ya wanachama hadi kufikia 50 na fedha walizokuwa wakiweka kufika shs milioni 3.

"Tulipokutana na TCMP baada ya kutupatia elimu ya ujasiriamali na hifadhi ya mazingira, walitupatia pia ruzuku ya shs milioni 1 kwa masharti kuwa tukifanya vizuri wangetuongezea kiasi kingine cha fedha. Waliweza kutuongezea tena ruzuku ya shs milioni 1.5 baada ya kuridhishwa na maendeleo ya kikundi chetu," anasema.

Mwenyekiti huyo anasema kwa sasa SACCOS hiyo ina jumla ya wanachama 74 ambapo wanawake ni 65 na wanaume ni 9, fedha kiasi cha shs millioni 14, shamba la ufuta la ekari 4 na eneo jingine la ekari 50 ambalo wamepewa na serikali ya kijiji kwa ajili ya kupanda miti na kuanzisha ufugaji wa nyuki katika msitu wa miti ya kupanda.

"Tumepanda ufuta mwaka huu ambapo mavuno yatakayopatikana yatatuwezesha kuendeleza malengo ya SACCOS yetu," anasema Ali. "Malengo hayo ni pamoja na kujenga ofisi ya kikundi chetu".

Mashavu Ali pia ni mmoja wa wanachama wanaofaidika na SACCOS. Anasema kiasi cha fedha alichokopa kwenye SACCOS ametumia kuboresha nyumba yake ya kuishi, kununua jiko la Oven kwa ajili ya kuoka mikate ya biashara na kusomesha mtoto wake sekondari huko Zanzibar. Mama huyu ambaye ni mjane pia amepata fursa ya kutumia mkopo kuanzisha shamba la ufuta la ekari 3 ambalo pia linaendelea vizuri.

Shaban Ramadhan, mweka hazina wa SACCOS hiyo pia ameweza kulima shamba la ufuta la ekari 8 baada ya kupata mkopo kutoka SACCOS. "Pia kuwepo katika kikundi kumetupatia fursa ya kupata mafunzo ya watu, afya na mazingira. Kikundi hiki hakiruhusu kuingiza watu wanaoendeshaa shughuli za kuharibu mazingira – hatuingizi watu wanaokata mkaa, mbao wala wakataji miti ovyo" anasema Ramadhan. "Mwanachama anayeacha shughuli za utunzaji wa mazingira na kufanya zinazoharibu mazingira tunamfukuza katika chama".

Kwa upande wake, Kitivo anajivunia kuwa na mazao mazuri ya ufuta na mahindi ambayo ameweza kulima kwa kutumia trekta kutokana na mkopo alioupata kutoka SACCOS. Anasema SACCOS imekuwa mkombozi wa kweli kwani sasa anaweza kuendesha kilimo cha kisasa na pia amewekeza katika biashara ndogondogo za kuuza chakula katika kata ya Miono.

"SACCOS imenipatia mtaji wa kuendesha kilimo cha kisasa," anasema. "Rai yangu kwa serikali ni kwamba kilimo cha kutumia jembe la mkono hakiwezi hata kidogo kumkomboa mkulima wa kijijini kujinasua kutoka katika dimbwi la umaskini. Serikali itafute njia ya kuwezesha wakulima wadogo wadogo kupata huduma ya trekta ili waweze kuendesha kilimo chenye tija."

Anasema pamoja na mpango wa Kilimo Kwanza kuwa na mikakati mizuri ya kuboresha kilimo na maisha ya Watanzania hasa wanaoishi vijijini, baadhi ya mikakati ya mpango huo haina mafanikio makubwa kwa wakulima wa vijijini. Mfano mzuri ni matrekta aina ya power tiller ambayo yamesambazwa kupitia mpango wa Kilimo Kwanza. "Mashamba mengi yana visiki ambavyo siyo rahisi kuving’oa kwa kutumia power tiller. Trekta pekee ndilo lenye uwezo wa kutifua ardhi vizuri na kuchimba visiki," anasema.

Kwa mujibu wa wakulima hao, ekari 3 za ufuta zina uwezo wa kuzalisha takribani kilo 2000 ambapo kilo inauzwa kwa shs 1500 katika soko linalopatikana kiurahisi katika mazingira ya kijijini. Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa hasa kwa wananchi wa vijijini ambao wengi wao wanaishi katika umaskini mkubwa wa chini ya dola mbili kwa siku.

"Najivunia kilimo cha ufuta kwani kitaniwezesha kurejesha mkopo na kuongeza akiba yangu katika SACCOS kwa kiasi kikubwa," anasema Kitivo.

Picha za makala haya zinaweza kupatikana katika tovuti ya https://tcmppwani.blogspot.com/ (END/2013)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The element 'html' is used but not declared in the DTD/Schema.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>