Mashirika ya Kiraia Yashambuliwa Duniani Kote Mandeep S.Tiwana
JOHANNESBURG, Mei 28 (IPS) - Mwezi Desemba 2011, serikali na mashirika makubwa ya kimataifa 159
yalitambua jukumu kubwa linalotekelezwa na mashirika ya kiraia katika
kuleta maendeleo na kuahidi kujenga mazingira rafiki ya kuendeshea sekta
isiyokuwa ya kutengeneza faida.
Pamoja na mazungumzo hayo katika Jukwaa la Wakuu wa nchi kuhusu
Ufanisi wa Misaada ya Maendeleo lililofanyika huko Busan, Korea
Kusini, leo hii NGOs, vyama vya wafanyakazi, mashirika ya kiimani,
vuguvugu za kijamii na mashirika yaliyojikita katika jamii yanayofanya
kazi kuibua ukiukwaji wa haki za wengine na rushwa yanabakia kifungoni
katika maeneo mengi ulimwenguni.
Ripoti za maofisa wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia yenye
hadhi kubwa zinaonyesha kuwa mashitaka ya uongo na mashambulizi ya
kuuawa kwa wanaharakati yameongezeka kwa kiasi kikubwa na hivyo
kutishia kurejesha nyuma malengo ya maendeleo ya kimataifa hata wakati
huu wa kujadili mpango mpya wa kuchukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo
ya Milenia ambayo yanamaliza muda wake mwaka 2015.
Katika hali nyingine, harakati zinaendeshwa na serikali kuzuia
ushiriki wa mashirika ya kiraia katika mikutano mikubwa ya Baraza Kuu
la Umoja wa Mataifa kupitia mchakato ambapo mataifa yanaweza kutoa
zuio lenye maslahi ya kisiasa kukataa kuhusishwa kwa baadhi ya NGOs
katika mijadala muhimu.
Kwa bahati mbaya, vikwazo vya kisheria vya uhuru wa kujieleza,
kuanzishwa kwa mashirika ya kiraia na haki ya kuandamana kwa njia ya
amani kunaonekana kuongezeka pamoja na maneno matupu ya kushirikisha
mashirika ya kiraia katika utoaji wa maamuzi kwenye mijadala ya
kimataifa.
Katika nchi nyingi mashirika ya kiraia yanazuiliwa kupata ufadhili
kutoka kwa vyanzo vya kimataifa, kama ilivyoelezwa katika ripoti ya
hivi karibuni ya mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa
kukusanyika na kufanya mikutano ya hadhara.
Nchini Russia, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayopata ufadhili
wa kimataifa yanakabiliwa na ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha
yanazingatia sheria tata ambazo zinataka NGOs kusajiliwa chini ya
sheria kandamizi za mashirika ya kigeni na ama sivyo yanakabiliwa na
adhabu kali.
Rasimu ya sheria ambayo kwa sasa inasubiri kupitishwa nchini
Bangladesh inataka kutekeleza mchakato wa kiurasimu wa kutaka
mashirika ya kiraia yanayopata ufadhili kutoka vyanzo vya kigeni
kupitishwa kwanza kwa mujibu wa sheria, katika hatua ya kutaka kuzuia
kukosolewa kwa serikali.
Misri inafikiria kutunga sheria mpya ambayo itaruhusu vyombo vya
kijasusi na usalama kudhibiti mashirika huru ya kiraia.
Wakati huo huo, mwanamtandao wa blogu maarufu nchini Ethiopia
anatumikia kifungo cha miaka 18 jela kutokana na kuandika taarifa ya
madhara ya Harakati za Kimapinduzi Zinazoendelea katika Ulimwengu wa
Kiarabu kwa nchi yake. Mwanaharakati maarufu nchini Laos amepotea
baada ya kukosoa hatua ya kuhamishwa kwa wananchi ambayo imeendeshwa
na serikali.
Nchini Saudi Arabia, waanzilishi wa Chama cha Haki za Kijamii na
Kisiasa cha Saudia wamehukumiwa kifungo jela cha miaka 10 na 11
kutokana na kuvunja kiapo kwa Mfalme. China inaendelea kuwafunga jela
waandishi wanaokosoa serikali ambao wanataka kupatikana kwa mageuzi ya
kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na Mshindi wa Tuzo ya Nobel Liu Xiobo.
Hali inatisha katika mataifa yenye migogoro. Wakati vita vya wenyewe
kwa wenyewe vikiendelea nchini Syria, idadi kubwa ya wanaharakati wa
amani na waandishi wa habari wanaswekwa jela na kufunguliwa mashitaka,
jambo ambalo ni kinyume na sheria za haki za binadamu za kimataifa.
Vitendo vya makundi ya kijeshi yenye msimamo wa mrengo wa kulia nchini
Colombia vimesababisha mauaji makubwa na kuifanya nchi hiyo kwa sasa
kuwa mbaya zaidi duniani kwa wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi.
Wanaharakati wa haki za wanawake wanaopinga misimamo mikali ya mfumo
dume na ya kidini nchini Pakistan wanapigwa risasi na kutishiwa mara
kwa mara, wakati wanaharakati nchini Sri Lanka na Bahrain wanaotoa
sauti zao katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini
Geneva mara nyingi wanakabiliwa na kulipiziwa kisasi wanaporejea
nyumbani kwao.
Nchini Cameroon na Uganda wanaharakati wanaopigania haki za mashoga
siyo tu kwamba wanatengwa na jamii lakini pia kukabiliwa na vitisho
vya kuuawa vya mara kwa mara ili kuwanyamazisha wasifanye kazi yao.
Hata katika mataifa yanayoonekana kuwa na demokrasia iliyokomaa, kuwa
mpinzani kunabakia kuwa kazi inayokabiliwa na hatua hasi. Sehemu ya
kikundi cha wanamazingira cha Forest Ethics Canada iliamua kuachana na
shughuli zake za kutoa misaada, ili kujizuia na kuingiliwa na
kukaguliwa kwa mara kwa mara baada ya kulaumiwa na serikali ya
kihafidhina kuwa wanazuia maendeleo ya kiuchumi nchini humo.
Julian Assange, mwanzilishi wa tovuti ya harakati ya WikiLeaks,
anaendelea kusakwa kutokana na kuanika kwake taarifa za siri kutoka
kwenye mitandao ya kidiplomasia ya Marekani na kudai kuwa anafanya
kazi kama inayofanywa na waandishi wa habari za uchunguzi.
Nchini Uingereza, tabia ya polisi wa upelelezi kujipenyeza katika
vikundi vya harakati za kimazingira kumesababisha Umoja wa Mataifa
kukemea hali hiyo, ambapo mtaalam wake wa uhuru wa kukusanyika na
kufanya mikutano ya hadhara, Maina Kiai, alielezea "kusikitishwa kwake
kwa kiasi kikubwa" mwezi Januari juu ya maofisa wa polisi kujipenyeza
katika mashirika yasiyotumia nguvu yoyote na yasiyofanya shughuli za
kiuhalifu.
Kama ambavyo inaonekana katika Ripoti ya Hali ya Mashirika ya Kijamii
ya CIVICUS ya mwaka 2013, ahadi zilizotolewa huko Busan kuhusu
mazingira rafiki kwa CSOs zimepuuzwa mara tu matamshi hayo
yalipotoweka masikioni mwa watu.
Kutokana na mijadala juu ya mkakati wa maendeleo baada ya mwaka 2015
kuendelea, mashirika maarufu ya kiraia yanaomba Jopo la Watu Maarufu
la Umoja wa Mataifa kutambua umuhimu wa mazingira rafiki kwa mashirika
ya kiraia katika uanzishwaji wowote ule upya wa malengo ya maendeleo
yanayokubaliwa kimataifa.
Wakati vichwa vya wanasiasa kwa sasa vinawaza tu kuanza vizuri au
kuendeleza maendeleo ya kiuchumi waliyonayo, kuna hatari ya kweli kuwa
haki za mashirika ya kiraia na uwezo wa kushiriki kama watoaji wa
maamuzi katika majukwaa mbalimbali zitaendelea kukandamizwa.
Kama malengo ya maendeleo kimataifa yanataka kufanikiwa, mashirika ya
kiraia yanapaswa kuwa na uwezo wa kufanya kazi zao kwa uhuru bila ya
hofu ya kulipiziwa kisasi kutokana na kuendeleza madai halali.
Mashirika ya kiraia yana mchango mkubwa katika mikakati ya maendeleo
na yanasaidia kupata ufumbuzi wa kiubunifu wa changamoto ngumu za
kimaendeleo.
Jambo la msingi zaidi, yanasaidia kuhakikisha kuwa kuna uwakilishi wa
sauti mbalimbali, hasa zile za wanyonge katika mijadala ya maendeleo.
Pengine hii ndiyo sababu ya kukandamizwa kwao.
(END/2013)
|
|
|
|
|
Latest
News from Africa |
|
XML error: The element 'html' is used but not declared in the DTD/Schema.
|
|
|
|
|
|