Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:38 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Klabu za Vijana, Ufumbuzi wa Changamoto za Watu, Afya na Mazingira
Na Marko Gideon

PANGANI, May 6 (IPS) - Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2002 ilionyesha kwamba idadi ya watu Tanzania iliongezeka kutoka milioni 23.1 mnamo 1988 hadi milioni 34.4 mnamo 2002, ikiwa ni wastani wa kiwango cha ukuaji cha asilimia 2.9 kwa mwaka. Sehemu ya watu wenye umri chini ya miaka 15 ilikuwa karibu asilimia 44, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu 2006.

Akiandika katika makala yake ya "Matokeo ya kidato cha nne 2012, mataifa mawili katika nchi moja" kwenye tovuti yake ya http://zittokabwe.wordpress.com Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mhe. Zitto Kabwe anasema "Ni vema ifahamike kwamba Tanzania ni Taifa la vijana na watoto. Kwa mujibu wa taarifa za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, hivi sasa Tanzania ina jumla ya vijana 38 milioni wa chini ya umri wa miaka 35, hii ni sawa na idadi ya watu waliokuwepo Tanzania mwaka 2003. Asilimia 78 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 35 na nusu ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 17".

Muundo huu wa kuwepo watu wengi vijana una maana ya ukuaji mkubwa wa idadi ya watu katika siku zijazo, pale vijana wanapoingia katika maisha yao ya uzazi bila kutilia maanani kama uwezo wa kuzaa unapungua au la, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu.

"Ukuaji haraka wa idadi ya vijana unahitaji ongezeko la matumizi yaliyolengwa kwenye huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na makazi. Ukuaji wa haraka wa nguvukazi unahitaji uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya rasilimali watu, na vilevile mikakati ya maendeleo inayohakikisha fursa za uundaji wa ajira katika siku zijazo," inasema Sera hiyo, ikiongeza kuwa "Ukuaji wa haraka wa idadi ya watu katika muktadha wa kuondoa umaskini hupunguza uwezekano wa kufikia ukuaji endelevu wa uchumi."

Sera inatoa wito wa kuongezeka kwa idadi na uwezo wa Asasi Zisizo za Serikali (AZISE) na mashirika ya dini yanayojihusisha na shughuli zinazohusiana na idadi ya watu ikiwa ni pamoja na utetezi, uhamasishaji wa jamii, utoaji wa huduma na kujenga uwezo ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa Mkakati wa Afya ya Uzazi kwa Vijana wadogo.

Sera inataka kuongezeka kwa mwamko kwa viongozi na jumuiya kuhusu uhusiano kati ya idadi ya watu, rasilimali, mazingira, kuondoa umaskini, na maendeleo endelevu.

Lakini ni kwa nini vijana ni kundi muhimu?

Kundi la vijana linaangaliwa sana katika jamii kutokana na kuwa na ushawishi kisiasa, kiuchumi na hata kijamii. Kutokana na kulitambua hili, Mradi wa TCMP Pwani kupitia shughuli zake za watu, afya na mazingira (PHE) limeamua kuunda klabu za vijana wilayani Pangani ili kuwa chachu ya kuhamasisha masuala ya watu, afya na mazingira. Akizungumza wakati wa mjadala wa kuanzisha klabu hizo katika kata ya Mkalamo hivi karibuni, Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Pangani na mtaalam wa masuala ya watu, afya na mazingira, Dk. Ole Sepere alisema klabu hizo zitakuwa majukwaa ya vijana ya kujadili masuala ya uzazi wa mpango, afya ya mama na mtoto, maambukizi ya VVU/UKIMWI na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

"Kwa kuwa na klabu zinazowaleta pamoja, vijana wataweza kujadili na kuanzisha shughuli za maendeleo zinazoweza kuwaingizia vipato kama vile ufugaji wa nyuki, kuku, mbuzi, ng’ombe wa kisasa au shughuli za kilimo cha kisasa ambazo ni endelevu," alisema Dk. Sepere.

Alisema uharibifu wa mazingira umeleta changamoto kubwa za kiafya, kiuchumi na kijamii katika maeneo mengi ya vijijini na mijini. Kwa hiyo klabu zitakazoanzishwa zitatoa fursa kwa vijana kwa kuwapatia nafasi ya kuanzisha mjadala juu ya shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira, athari za uharibifu huo na kutafuta njia za kukabiliana na uharibifu huo.

Kwa upande wao, vijana walielezea kuwa na ufahamu wa uhusiano uliopo kati ya watu, afya na mazingira. Walisema mtu akiwa na watoto wengi ambao amewazaa bila mpangilio, atashindwa kumudu kuwalea kama vile kuwapatia elimu ya kutosha na hatimaye kuendelea kubaki kijijini wakitegemea zaidi rasilimali chache zilizopo kama vile misitu na bahari. Ni vijana hawa wasiokuwa na elimu ambao hugeuka kuwa wachomaji wakuu wa mkaa, washiriki wakuu katika uvuvi haramu na usiokuwa endelevu na kilimo kinachoharibu mazingira.

Hivyo, vijana hao walikubali kuanzisha klabu za vijana zitakazoongoza katika usambazaji wa ujumbe wa uzazi wa mpango, masuala ya afya na kuhifadhi mazingira. Walisema mara nyingi, pamoja na kuwa wengi nchini, vijana hawapati fursa ya kushiriki kikamilifu katika mijadala ya utoaji wa maamuzi katika ngazi ya kijiji hadi taifa. Walisema klabu zitakuwa jukwaa muhimu la kujadili masuala ya maendeleo na kuyafikisha kwa watoaji wa maamuzi.

Hata hivyo, Dk. Sepere aliwapa vijana hao angalizo juu ya changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kuanzisha klabu za vijana. "Kuanzisha kikundi ni kazi ngumu, lakini kukiua ni kazi rahisi sana," aliwaasa. "Vikundi vingi vinakufa kutokana na kukosekana kwa nidhamu ndani ya kikundi."

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ubinafsi. "Mara nyingi vikundi vinakufa kutokana na ubinafsi wa wachache katika kikundi, umimi uliopitiliza na kutaka kufaidika na kikundi haraka haraka bila kujali uendelevu wake".

Kukosekana kwa mtaji ni changamoto nyingine za kuanzisha vikundi. "Mara nyingi vikundi vinakufa kutokana na waanzilishi kuhisi hawana nguvu za kiuchumi," alisema.

Aliwaasa vijana kuwa mtaji mkubwa wa awali ni nguvu zao, muda wao na moyo wa kujitolea. "Kama mkiwa mmeshaanza kuonyesha jitihada, mfano, mkiwa mmeanzisha bustani za mbogamboga, ni rahisi wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuwasaidia," alisema.

Klabu hizo kwa kuanzia zitaanzishwa katika vijiji vya Mkalamo, Mbulizaga, Mkwaja, Buyuni, Sange na Kwakibuyu. Zinaanzishwa kama sehemu ya jitihada ya TCMP Pwani inayofadhiliwa na USAID na kupata msaada wa kiufundi kutoka Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Rhode nchini Marekani za kuhakikisha mazingira na rasilimali za pwani yanahifadhiwa na kutunzwa.

Mradi wa TCMP Pwani unaendesha shughuli zake za kuhifadhi na kutunza mazingira ya pwani kwa kushirikisha wananchi katika shughuli za uzalishaji mali, uzazi wa mpango, afya, kuhifadhi viumbe waliopo katika hatari ya kutoweka, kufuatilia mwenendo wa tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa ajili ya kuhamasisha kuwepo kwa matumizi sahihi ya ardhi, kuisimamia na kuhifadhi na kutunza mazingira na mapitio ya wanyama, kutenga miamba ya bahari kuhamasisha uvuvi endelevu, kuongeza elimu ya ufahamu wa mabadiliko ya tabia nchi na jinsi ya kukabiliana nayo na kuhamasisha ufugaji wa viumbe bahari katika mwambao wa Bahari ya Hindi. Katika nchi ambapo vijana ndiyo sehemu kubwa ya wakazi, ni muhimu kwa sauti zao na maoni kusikika na kujenga mustakabali wa baadaye ambao wataurithi. "Kupitia klabu hizi vijana wanatarajiwa kuja kuonekana kama viongozi na mabalozi wa jamii zao katika kukabiliana na changamoto za watu, afya na mazingira," anasema Juma Dyegula, Mratibu wa Mradi wa Watu, Afya na Mazingira katika TCMP. (END/2013)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>