Inter Press Service News Agency
Monday, June 18, 2018   10:49 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions


TANZANIA: Vyombo vya Habari na Siku 16 za Kupinga Unyanyasaji Dhidi ya Wanawake Duniani
Na Marko Gideon

DAR ES SALAAM, Desemba 6 (IPS) - Kifungu cha 29 cha Itifaki ya Jinsia na Maendeleo kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kinataja umuhimu wa vyombo vya habari kuzingatia masuala ya jinsia kwa kuhakikisha wanawake wanakuwa na sauti sawa na wanaume katika maudhui ya habari na idadi ya wafanyakazi wa vyombo vya havari.

Kwa mujibu wa kifungu hicho "Wanawake wanapaswa kuwa na uwakilishi sawa katika maeneo yote na katika ngazi zote zinazohusu kazi za uandishi wa habari".

Umoja wa Mataifa pia unatambua umuhimu wa wanawake katika kuwa na sauti sawa kwenye vyombo vya habari. Kwa mujibu wa maazimio ya Mkutano wa Nne wa Wanawake wa Beijing wa Umoja huo wa mwaka 1995, wanawake wanapaswa kuwa na ushiriki kamili na wa usawa katika vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na menejimenti, uandaaji wa vipindi, elimu, mafunzo na utafiti. Kwa mujibu wa maazimio hayo, kuendelea kuandika au kuonyesha mambo mabaya ya wanawake na picha zinazowadhalilisha katika vyombo vya habari kunapaswa kukomeshwa.

Hata hivyo, hali bado ni tofauti katika ukanda mzima wa Kusini mwa Afrika ikiwa ni pamoja na nchini Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Jinsia na Vyombo vya Habari ya mwaka 2010 iliyofadhiliwa na shirika la Gender Links la Afrika Kusini, masuala ya jinsia hayapatiwi nafasi kubwa katika vyombo vya habari vya Tanzania ambapo ni asilimia 0.3% ya habari zinahusu jinsia.

Utafiti pia unasema wanaume wanaongoza kutoa sauti zao katika vyombo vya habari vya Tanzania, wakiwa ni asilimia 79 ya vyanzo vyote vya habari huku wanawake wakishika asilimia 21 tu. Katika suala la ajira katika vyombo vya habari, utafiti unaonyesha kuwa wanawake ni asilimia 36 ya wafanyakazi katika vyombo vya habari, lakini wanashika asilimia 30 tu ya nafasi za juu za utoaji wa maamuzi.

Pia kuna taarifa za unyanyasaji wa kijinsia katika vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na masuala kama vile rushwa ya ngono, mishahara duni na kufanya kazi hadi miaka mitatu bila kupatiwa mikataba ya ajira.

Akizungumza wakati wa warsha ya waandishi wa habari na mashirika ya kiraia ya kujiandaa na kampeni ya siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia mapema mwezi wa Novemba, Mratibu wa warsha hiyo Gladness Munuo alisema kuna haja kubwa ya kujenga uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia kama vile uvunjaji wa haki za binadamu kijamii, kitaifa, kikanda na kimataifa.

Alisema katika kipindi cha siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia kuna haja ya kuimarisha kazi za kupinga ukatili dhidi ya wanawake katika ngazi za chini na kuunganisha kazi za maeneo mbalimbali yanayoshughulikia ukatili dhidi ya wanawake. Pia kipindi hiki ni muhimu katika kujenga njia ya kubadilishana taarifa na uzoefu kuhusu ukatili dhidi ya wanawake kati ya wadau mbalimbali, kuonyesha mshikamano ulimwenguni kote kupinga ukatili dhidi ya wanawake na pia kutumia siku 16 kupaza sauti ili wadau wote waweze kutekeleza wajibu wao katika kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake.

Aliongeza kuwa kampeni hiyo pia inafanyika nchini kwa kuwa Tanzania, kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika, vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiendelea, huku unyanyaswaji huo ukijitokeza katika sura mbali mbali kama vipigo, ukeketaji, ubakaji, mauaji ya wanawake na watoto wa kike, kurithi wajane, ukatili nyumbani n.k.

Alisema ni muhimu vyombo vya habari na mashirika ya kiraia kushirikiana kwa kiasi kikubwa katika kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwani vyombo hivyo ni chachu kubwa ya kuleta mabadiliko katika jamii kama vikifanya kazi pamoja.

Ili vyombo hivi viweze kufanya kazi kwa pamoja, kuna haja ya kukaa pamoja na kujuana. "Ni muhimu mashirika ya kiraia kujua jinsi vyombo vya habari vinavyofanya kazi, na wakati huo huo vyombo vya habari kujua jinsi mashirika ya kiraia yanavyofanya kazi," alisema Munuo.

Hata hivyo, wadau mbalimbali waliohudhuria warsha hiyo walipendekeza kuwepo mafunzo ya jinsi vyombo vya habari vinavyofanya kazi kwa viongozi wanawake kwani wengi wao wanashindwa kuongea na vyombo vya habari bila kujua kuwa wanajinyima wenyewe haki yao ya kutoa maoni.

Walisema mifumo ya maisha katika jamii na tamaduni mbalimbali barani Afrika zimewafanya wanawake siku zote kuwa nyuma na kutegemea kila jambo kutoka kwa wanaume. "Kuna wakati hata wanawake wa vijijini hawataki kuongea na waandishi wa habari hadi wapate idhini ya kuongea kutoka kwa waume zao," alitoa maoni Rose Mwalongo, mmoja wa washiriki wa warsha hiyo.

Waadishi wa habari nchini walitakiwa kutumia fani yao kwa bidii kuhakikisha kuwa katika kila habari wanazoandika wanazingatia kuwepo kwa sauti za wanawake ili kufikisha ujumbe ambao unatokana na maoni ya jamii nzima na wala siyo kuegemea upande wa jinsia moja tu ya wanaume. (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The element 'html' is used but not declared in the DTD/Schema.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>