Inter Press Service News Agency
Monday, June 18, 2018   10:46 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions


Wakulima wa Kigeni Wadhoofisha Usalama wa Chakula Nchini Zambia
Na Nebert Mulenga

LUSAKA, Desemba 3 (IPS) - Ongezeko la maendeleo ya kilimo nchini Zambia litaathiri usalama wa chakula nchini humo kwani wakulima wadogo wadogo wanaendelea kuondolewa katika ardhi zao za kimila kupisha wakulima wakubwa wa ndani na nje ya nchi wanaotaka kuendesha kilimo cha biashara, kwa mujibu wa mkuu wa shule ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Zambia, Dk. Mickey Mwala.

"Wakulima wadogo wadogo ni watu ambao wanahusika na usalama wa chakula nchini Zambia. Kwa hiyo, kuwaondoa katika maeneo yao kunaweza kuathiri kwa kipindi kirefu hali ya usalama wa chakula, kama hali itazidi kuendelea," aliiambnia IPS.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, kaya nyingi nchini Zambia kwa sasa zina usalama wa chakula, huku kaya 62,842 kati ya watu wanaokadiriwa kuwa milioni 13.4 nchini humo wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

"Kuchukuliwa kwa ardhi kunaongeza matukio na kiwango cha umaskini nchini kwa kuongeza idadi ya watu ambao hawawezi kupanda chakula chao wenyewe, na ambao hawawezi kupeleka watoto wao shuleni," Mwala alisema.

Kuondolewa kwa wakulima kutoka katika ardhi zao za kimila kulianza miaka 12 iliyopita lakini kulipata umaarufu mwaka 2005 baada ya serikali kuwaita wawekezaji wa kigeni, kwa mujibu wa Umoja wa Ardhi Zambia, shirika linalotetea haki za kumiliki ardhi.

Kuchukuliwa kwa ardhi kunakofanywa na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi kwa sasa kunaonekana kuwa suala la kawaida katika taifa hilo la kusini mwa Afrika. Katika wilaya ya Masaiti, katika jimbo tajiri wa madini la Copperbelt, zaidi ya wakulima 2,000 walisemekana kuhamishwa kutoka katika ardhi yao mwaka 2011 kufuatia kuchukuliwa kwa hekta zaidi ya 200 na kampuni ya uzalishaji wa saruji ya Nigeria. Baadaye walilipwa dola 250 kwa kila hekta kama fidia.

Kuanzishwa kwa biashara ya madini katika majimbo ya North-Western, Copperbelt na Luapula pia kumewaacha maelfu ya wakulima wadogo wadogo bila makazi.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2011 ya GRAIN, shirika lisilokuwa la kiserikali la kimataifa ambalo linakuza usimamizi endelevu na matumizi ya baoanuwai ya kilimo, wenye jina la "Kuchukuliwa kwa ardhi na mgogoro wa chakula duniani", asilimia tatu ya ardhi ya kilimo nchini Zambia inadhibitiwa na wageni wanaoendesha kilimo cha chakula cha biashara.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Oakland , shirika la utafiti huru wa sera, uwekezaji wa kilimo hapa unazidi kuongezeka wakati serikali "inazidi kuuza kimyakimya na kuandaa kuendeleza kwa uchache hekta milioni 1.5 za ardhi yake."

Pamoja na kwamba hakuna utafiti umefanyika kuangalia idadi halisi ya wakulima waliohamishwa kutokana na kuchukuliwa kwa ardhi yao, Chama cha Wakulima cha Taifa cha Zambia chenye kifupi chake kwa lugha ya Kiingereza kama ZNFU kilisema wakulima walioathirika wanaweza kufikia maelfu.

Kwa mujibu wa makamu wa rais wa ZNFU Graham Rae, kuhamishwa kwa wakulima kutoka katika ardhi yao ya jadi ni suala la kuangaliwa. "Limekuwa likiendelea kwa muda sasa na wakulima wetu wengi, hasa katika maeneo ya kijijini wameathirika.

"Hali ya usalama wa chakula inaweza kuwaathirika kwasababu pengine tunazungumzia wakulima kwa maelfu ambao hawazalishi. Katika nchi kama Afrika Kusini, usalama wa chakula umejikita katika wakulima wakubwa, wakati kwa upande wetu sekta ya wakulima wadogo wadgo ina jukumu kubwa la usalama wa chakula. Hivyo usalama wa chakula unaweza kuathirika kwa kiasi kikubwa, siyo tu katika ngazi ya kaya lakini pia ngazi ya taifa," Rae alisema.

Wakulima wadogo wadogo ni asilimia 70 ya jamii ya wakulima ya Zambia, kwa mujibu wa ZNFU. Umoja una wanachama 600,000 ambao ni pamoja na wakulima wadogo wadogo, wakulima wa dharula, na wakulima wa biashara. Kati ya idadi hiyo, theluthi mbili au 400,000 ni wakulima wadogo wadogo. Lakini idadi ya wakulima wadogo wadogo nchini wanaweza kuwa mara mbili ya idadi hiyo na hata mara tatu kwani wengi wao hawajajiunga na chama.

Henry Machina, mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa Ardhi Zambia, kikundi cha utetezi, analaumu kuhamishwa kwa wakulima kuwa kunatokana na taratibu mbovu na ngumu za kupata hati miliki na sheria za "kizamani" ambazo hazitambui haki za kimila kama aina ya umiliki wa ardhi. Chini ya sheria nchini Zambia, hati miliki ndiyo uthibitisho pekee kuwa unamiliki ardhi hiyo.

"Ili kupata hati miliki, inaweza kukuchukua kati ya miezi miwili hadi miaka 10. Mfumo ni wa kizamani mno na umejikita katika serikali kuu – kwani unaweza kupata hati miliki kutoka kwa Wizara ya Ardhi pekee mjini Lusaka," Machina aliiambia IPS.

"Kwa wakulima katika maeneo ya vijijini, kupata hati miliki ni gharama kubwa. Inabidi kulipia usafiri ikiwa ni pamoja na chakula na malazi kila wakati wanaposafiri kufuatilia. Na inaweza kuwagharimu hadi kwacha milioni 10 (kama dola 2,000) katika mchakato huo. Matokeo yake, wengi wanaona afadhali waachane na mchakato na hivyo kuendelea na kilimo," alisema Machina.

Kwa sasa asilimia 59 ya Wazambia wanaishi chini ya mstari wa umaskini, huku asilimia 65 ya wakazi wakiishi katika maeneo ya kijijini.

Pretorious Nkhata, kutoka wilaya ya Mpongwe kwenye jimbo la Copperbelt, ni mmoja wa wakulima hao. Akiwa na umri wa miaka 68-anadai kuwa alihamishwa kutoka hekta zake 21 za ardhi ya jadi, ambazo amekuwa akilima kwa miaka 10 na zaidi, na kampuni ya kilimo cha biashara ya Afrika Kusini mwaka 2008.

Nkhata ambaye pamoja na wakulima wengine walihamishwa kutoka hekta 46,876 za shamba la biashara aliiambia IPS kuwa walipata ardhi yao kutoka kwa kiongozi wa jadi lakini hawakupata hati miliki kutoka serikalini.

"Walituambia kuwa sisi ni watumiaji wasiokuwa rasmi na ni wavamizi wa ardhi. Nilikuwa na hekta 21 … nilizipoteza zote …

"Wakulima wa kilimo cha biashara kutoka Afrika Kusini walifika na bunduki na kutishia kumpiga yeyote ambaye angekaidi amri ya kuondoka. Walichoma moto mali zetu zote za kaya zetu bila kutuambia. Tulikuwa karibu kaya 200. Walichoma moto maghala yangu ya kuhifadhia chakula, nguo, mablanketi, vitanda, televisheni – walichoma hata mashamba yangu," alisema.

Hata hivyo kampuni hiyo imeshauza ardhi na kufunga biashara zake nchini Zambia. Jitihada za IPS za kutafuta maoni ya kampuni hiyo hazikuafanikiwa.

Mwanasheria mashuhuri ambaye anawakilisha wakulima waliohamishwa na ambaye hakutaka kutajwa, aliiambia IPS kuwa watu wenye kumiliki ardhi kijadi nchini Zambia hawana ulinzi wa kisheria, na hata fidia zao zinatolewa kwa misingi ya kibinadamu tu.

"Vifungu vya 33 na 34 vya Sheria ya Ardhi na Utoaji wa Hati Miliki vinasema kuwa hati miliki ni ushahidi wa kisheria kuwa namiliki ardhi. Kanuni ya msingi ni kwamba mtu mwenye hati miliki ya ardhi anamiliki kila kitu katika ardhi hiyo. Haijalishi ni maendeleo gani umefanya katika ardhi hiyo kama huna hati miliki siyo yako," alisema mwanasheria huyo.

"Tunachopigania tunapowawakilisha wateja wetu ambao ardhi yao imechukuliwa ni kupewa fidia kutokana na kufanya maendeleo katika ardhi – lakini wamiliki wapya wa ardhi hawana kifungo chochote cha sheria kinachowataka kulipa fidia."

Katibu mkuu katika Wizara ya Ardhi Daizy Ng’ambi aliiambia IPS kuwa kwa sasa serikali inaandaa waraka wa kazi kuwapatia usalama wamiliki wa jadi.

"Kwa sasa, hakuna kifungu kinachowalinda wamiliki wa jadi ambao hawana hati miliki. Lakini inaonekana kuwa waraka utakapokamilika juu ya usalama wa wamiliki wa jadi na kupata maoni kutoka kwa wadau wote, masuala ya umiliki wa jadi na ulipaji sahihi wa fidia yatazingatiwa," Ng’ambi alisema.

Pia alisema wizara yake inafanya kazi kuboresha teknolojia katika kuandaa hati miliki, ambayo inatarajiwa kupunguza taratibu zinazochosha na ambazo zinachukua muda mrefu.

Pamoja na mabadiliko haya, Nkhata hatapata ardhi ambayo aliwahi kuimiliki. Kwa sasa Nkhata anaishi katika kijiji kidogo kilichozungukwa na mashamba ya wakulima wa biashara yaliyozungukwa na fensi ya nyaya, baadhi ya kilomita 40 kutoka katika shamba lake la zamani. "Kwa sasa nimekwama. Hawajanipatia fidia yoyote au ardhi mbadala," alisema (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The element 'html' is used but not declared in the DTD/Schema.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>