Inter Press Service News Agency
Wednesday, April 25, 2018   07:51 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions


Kukuza Kilimo cha Migomba Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi
Na Marko Gideon

PANGANI, Oktoba 31 (IPS) - Haki ya chakula ni moja ya haki za msingi kabisa kwa mwanadamu. Hata hivyo, njaa inaendelea kuwakumba watu wengi duniani huku Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiongoza kwa kuwa na wakazi wengi wanaokabiliwa na njaa kila mwaka. Mabadiliko ya tabia nchi yamezidisha kuenea kwa janga hili kutokana na kusababisha uzalishaji wa chakula kutokuwa endelevu.

Pamoja na takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa kuonyesha kuwepo kwa mafanikio ya kupunguza njaa kwa wakazi wa dunia, hata hivyo, bado mtu mmoja katika kila watu nane wanatajwa kukabiliwa na njaa.

Idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa imepungua kwa watu milioni 130 tangu mwaka 1990, kutoka watu bilioni moja hadi milioni 868. Idadi kubwa ya watu hawa, milioni 852, wanaishi katika nchi zinazoendelea, jambo ambalo lina maana kuwa asilimia 15 ya watu katika nchi zinazoendelea wanaishi katika njaa, wakati ni watu milioni 16 tu wanakabiliwa na njaa katika nchi zilizoendelea.

Ripoti ya Hali ya Kukosekana Kwa Usalama wa Chakula Duniani Mwaka 2012 (SOFI), ambayo imetolewa kwa pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), inasema kuwa kama "hatua stahiki" hazijachukuliwa kulisha watu wenye njaa na kupunguza kasi ya kupungua kwa uzalishaji wa chakula, lengo la kupunguza nusu ya watu wenye njaa katika ulimwengu unaoendelea ifikapo mwaka 2015 halitafikiwa.

"Habari njema ni kuwa tuna baadhi ya mafanikio lakini bado inaonyesha kuwa mtu mmoja katika kila watu nane anaishi na njaa. Jambo hili halikubaliki," Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya FAO siku za karibuni. "Katika FAO namba inayokubalika ya watu wenye njaa ni sifuri tu."

"Hata kama tunapunguza nusu ya watu wenye njaa ifikapo mwaka 2015, ni muhimu kuangalia mbele na kufikia kutokomeza kabisa njaa, na hivyo kujibu wito wa mkutano wa kilele wa Rio+20 wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wa ‘Changamoto ya Namba Sifuri ya Njaa’," alisema Graziano da Silva.

Hali ni mbaya zaidi barani Afrika, ambapo idadi ya watu wenye njaa imeongezeka katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita kutoka watu milioni 175 hadi milioni 239. Katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, njaa imekuwa ikiongezeka kwa asilimia mbili kwa mwaka tangu mwaka 2007, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Takwimu za hivi karibuni nchini Tanzania zinaonyesha kuwa asilimia 42 ya watoto wa chini ya umri wa miaka 5 wanapata lishe duni na wamedumaa na zaidi ya asilimia 50 ya watoto hao wana upungufu wa damu.

Kuna mambo mengi yanayochangia kuenea kwa njaa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao pia unaongoza kwa umaskini duniani. Moja ya sababu hizo ni kuzidi kuenea kwa mabadiliko ya tabia nchi.

Ili kujua athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa jamii, Mradi wa TCMP- Pwani unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) ulifanya utafiti wake hivi karibuni katika baadhi ya vijiji wilayani Pangani. Matokeo ya utafiti katika kijiji cha Mwembeni kata ya Madanga yalionyesha kilimo kuathirika na hivyo kuwakosesha wananci wa kijiji hicho vyanzo muhimu vya chakula na mapato.

"Matokeo ya utafiti shirikishi uliofanyika katika kijiji cha Mwembeni juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na namna jamii inavyoweza kukabiliana nayo ulionyesha kuwa kijiji kimekumbwa na athari za mabadiliko hayo kutokana na historia ya matukio ya majanga ya ukame unaojitokeza mara kwa mara na kunyesha kwa mvua kubwa za el nino mwishoni mwa miaka ya 1990", anasema Jairos Mahenge, mratibu wa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi katika TCMP-Pwani.

Kwa mujibu wa Mboni Salehe, katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Tabia Nchi ya kijiji cha Mwembeni, kutokana na hali ya ukame iliyojitokeza katika miaka ya hivi karibuni, mashamba ya mpunga hayakuweza kutoa mazao hata kidogo kutokana na ukame kuathiri kilimo cha mpunga ikiwa ni pamoja na mazao mengine ya chakula.

Amesema zamani wakulima kijijini humo waliweza kupata mvua za kutosha na kuendesha kilimo mara nne kwa mwaka na kuvuna katika misimu yote, lakini sasa hali ni mbaya na uzalishaji wa chakula umepungua kwa kiasi kikubwa.

"Tulikuwa na uwezo wa kuvuna mpunga, mihogo na miwa ambayo pia iliweza kutusaidia kuingiza kipato kutokana na kuuza ziada na hata kusafirisha kwenda Zanzibar," alisema Bi. Salehe hivi karibuni. "Lakini sasa mvua ni chache, mto Mzia umekauka, hauna maji tena. Chumvi imeongezeka katika Mto Pangani, mabonde ya mpunga yamevamiwa na chumvi na badala ya kuendesha kilimo cha mpunga na miwa, sasa mabonde hayo yamejaa miti aina ya mikoko."

Ili kukabiliana na hali hiyo, mradi wa TCMP-Pwani ulishauriana na wananchi na wadau wengine juu ya njia za kukabiliana na ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Katika hali ya kuweza kuelimishana na wananchi juu ya mabadiliko ya tabia nchi, tuliwaambia kuwa ufumbuzi siyo kukimbia kijiji, lakini namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo," anasema Mahenge, na kusema kuwa moja ya ufumbuzi wa kukabiliana na ukame ni kupanda mazao yanayohimili ukame huo.

Kilimo cha migomba ufumbuzi wa kukabiliana na athari za ukame

Kwa mujibu wa Mahenge, kutokana na kiijiji cha Mwembeni kuwa na historia ya watu kupenda kupanda migomba, ambayo walisema inawasaidia wakati wa ukame, "tulishauriana na wanakijiji hao kupanda zao hilo ambalo angalau wana asili na uzoefu nalo ili kukabiliana na ukame badala ya kuchagua mbinu ambayo ni mpya kabisa kwao".

"Kwa kushirikiana na wataalam wa kilimo wa wilaya ya Pangani tuligundua kuna taasisi za kilimo ambazo zimefanya utafiti wa aina ya migomba inayoweza kuhimili ukame, magonjwa na kuzaa katika kipindi cha muda mfupi. Tukaona mazao hayo yatakuwa ni suluhisho kwa eneo la Mwembeni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hasa suala zima la ukame," anasema.

Migomba kutoka kituo cha utafiti wa kilimo Tengeru mkoani Arusha iligawiwa kwa wanakijiji 20, ambao kila mmoja alipata miche 10 ya kupanda katika kipande chake cha shamba kwa kutumia mbinu za kitaalam. Akifafanua zaidi, Mahenge anasema mbinu hizo ni pamoja na kuzingatia kuwa nafasi kutoka mche hadi mche ni lazima kuwa mita 5, na shimo lenye upana wa futi 3 na urefu futi 3 na kina futi 3. Shimo linatakiwa kuchanganywa na mbolea ya kutosha na kuacha nafasi ya futi moja kutoka juu kwa ajili ya kuacha nafasi ya maji kutuama kwa muda mrefu.

Aina 5 za mbegu za migomba ziligawiwa kwa wananchi. Aina hizo ni pamoja na mkono wa tembo, mzuzu, williams, grandenine na Chinese Cavendish. Kila mkulima alipewa kwa mchanganyiko kuhakikisha kila mmoja anakuwa na aina zote za mbegu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mahenge, mwitikio wa wananchi juu ya mradi huo ulikuwa ni mkubwa kwani "jamii iliona ile miche 200 iliyoenda pale kijijini ni sawa na tone la maji katikati mwa Bahari, kwani karibu wananchi wote kutoka kijijini hapo walikuwa na hamu ya kupanda migomba hiyo".

Mradi endelevu

Kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kudumu kwa miaka mingi, TCMP-Pwani ilihakikisha kuwa inaandaa mradi utakaoendeshwa na wananchi wenyewe na utakaohakikisha unadumu kwa miaka mingi hata kama mradi huo wa Pwani utakua umeshamaliza wakati wake wa utekelezaji.

"Tumehakikisha mradi unakuwa endelevu kwa kuweka makubaliano na serikali ya kijiji kuwa watu 20 waliopatiwa mbegu za migomba watakuwa ni chachu ya kusambaa kwa migomba hiyo katika kijiji kizima na kwingineko na tukakubaliana na serikali ya kijiji kuwa machipukizi yote yatakayotokana na migomba hiyo yatasambazwa kwa wananchi wengine," anafafanua Mahenge.

Pia mradi unahakikisha uendelevu kwa kufanya kazi karibu na halmashauri ya wilaya, ambapo bwanashamba wa tarafa ya Madanga hufuatilia kwa karibu kuwasaidia wananchi katika masuala ya kitaalam kutokana na kuwa mmoja wa waanzilishi na wabunifu wa mradi wakati wote tangu mwanzo. Pia kikundi cha watu ishirini kilichopewa mbegu za Migomba kina uongozi wao ambao unafanya ufuatiliaji wa maendeleo ya mradi pamoja na kuwa kila mmoja ana shamba lake binafsi analolihudumia.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Pangani, Neneka Rashid, anaunga mkono suala la uendelevu wa mradi huo kwa kusema kuwa mbegu hizo za migomba zinatarajiwa kusambaa kwa wananchi wengine na baadaye kutapakaa kwa haraka katika kijiji kizima na vijiji vingine.

Mahenge anasema kwa sasa jukumu la TCMP-Pwani ni kuendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha kwamba hiyo migomba inatoa matarajio yaliyotarajiwa. "Kwa mujibu wa sifa ya hiyo migomba endapo itapatiwa matunzo mazuri ina uwezekano wa kutoa zao la kwanza ndani ya miezi 10 tu. Ni matarajio yetu kuwa muda siyo mrefu tutaanza kuona matunda," alisema. (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The element 'html' is used but not declared in the DTD/Schema.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>