Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:37 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Uzazi wa Mpango Muhimu Kuhifadhi Mazingira, Kuimarisha Afya ya Mama na Mtoto.
Na Marko Gideon

DAR ES SALAAM, Septemba 6 (IPS) - Tangazo linalorushwa katika kituo cha redio ya jamii cha Pangani FM ambalo limeandaliwa kwa mtindo wa mchezo wa kuigiza linasisitiza mambo makuu matatu – idadi ya watu, afya na mazingira.

Tangazo linaanzia mchana nyumbani kwa mama wawili ambapo mama Sauda anagonga hodi ambayo inachelewa kuitikiwa kutokana na kelele za sauti ya mtoto anayelia. Baada ya muda mlango unafunguliwa huku sauti ya mtoto mchanga ikiendelea kusikika akilia.

Mama Sauda anashangaa "He! mama Wawili, mimba nyingine tena hata hawa mapacha hawajatimiza mwaka? Mama Wawili anajibu huku akiendelea kubembeleza mtoto. "Loh! nifanyeje mama Sauda na huyo shemeji yako ndivyo anavyotaka."

Mama Sauda anahamaki. "Jamani mbona shemeji anafanya mambo ya kizamani- siku hizi kuna njia za kisasa za uzazi wa mpango ili kujikinga na mimba zisizotarajiwa." Mama Wawili hakukosa cha kujibu. "Mmwenzangu hizo njia tunasikia zina madhara….!?" Mama Sauda anamhakikishia usalama "Hapana njia zote ni salama, mbona mimi na mume wangu tunatumi miaka yote…kwanza baba wawili yuko?" Mama Wawili anajibu kwa unyonge "Yupo shamba".

Mama Sauda anaahidi kumfuata huko huko shamba ili kwenda kumpatia dozi yake, lakini wakati huo huo anaanza kumpatia mama wawili ujumbe wa uelewa wa njia za uzazi wa mpango.

"Uzazi wa mpango, utawafanya mpange idadi ya watoto mnaowataka na mtaweza kuwalea na kuwasomesha, utakuwezesha kujikinga na mimba zisizotarajiwa, mtaweza kuboresha afya ya mama na mtoto na kumuwezesha mama kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi."

Anaendelea kutoa ufafanuzi. "Njia zote za uzazi wa mpango ni salama, fika kwa mhudumu wa afya upate taarifa sahihi."

Anaongeza "tukipanga uzazi tutaweza hata kutunza vyema rasilimali zetu na zitatutosha…na tutaweza kupiga hatua katika kuleta maendeleo endelevu…. Umenipata mama Wawili."

Baada ya tangazo unakuja ujumbe "Tumia njia za kisasa za uzazi wa mpango. Panga uzazi na tunza mazingira kwa maisha bora ya sasa na ya baadaye".

Tangazo hili ni moja ya kazi za Mpango wa Kuhifadhi Mazingira na Rasilimali za Ukanda wa Pwani (TCMP-Pwani) unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) na kupatiwa msaada wa kiufundi na Kituo cha Rasilimali za Bahari cha Chuo Kikuu cha Rhode Island katika wilaya za Pangani na Bagamoyo.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Kitengo cha Idadi ya Watu, Afya na Mazingira (PHE) wa TCMP-Pwani, Juma Dyegula, mradi unatumia dhana ya kisasa kabisa ya hifadhi ya mazingira kwa kujenga uelewa wa jamii za pwani juu ya suala zima la uhusiano uliopo kati ya idadi ya watu, afya na mazingira. Na hapa ndipo suala zima la uzazi wa mpango linapokuja.

"Dhana ya idadi ya watu, afya na mazingira ambayo pia inatekelezwa katika mradi tofauti ujulikanao kama BALANCED (Building Actors and Leaders for Community Excellence in Development) ina lengo la kukuza uelewa wa mwingiliano uliopo kati ya idadi ya watu, afya na mazingira katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa bioanuwai," anasema Dyegula.

"Pia dhana hii inajengwa katika ukweli kwamba uzazi wa mpango ni muhimu katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana ya kuhifadhi mazingira katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa bioanuwai na katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi. Inajengwa katika ukweli kwamba usimamiaji wa maliasili unakwenda vizuri kama kuna uelewa mzuri wa umuhimu wa kudhibiti ukubwa wa familia."

Kwa mujibu wa tafiti za BALANCED, jinsi idadi ya watu inavyozidi kuongezeka ndivyo umaskini unavyozidi kuongezeka ambao husababishwa na fursa chache za kujiingizia kipato, migogoro katika familia na hata katika ngazi ya jamii na kukosekana kwa usawa wa kijinsia, miongoni mwa mamabo mengine. Hali hii inaweza kuchangia kuenea kwa magonjwa kama ya VVU/UKIMWI, utapiamlo na hivyo usimamiaji duni wa maliasili na kusababisha uharibifu wa mazingira kama vile ukataji miti kupita kiasi.

Tanzania ni mojawapo ya mataifa yanayokabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaohusiana na dhana ya idadi ya watu, afya na mazingira. Kwa mujibu wa mradi wa BALANCED, idadi ya watu nchini Tanzania ni zaidi ya milioni 40, kiwango cha ongezeko la idadi ya watu ni asilimia 2.3, kiwango cha uwezo wa kuzaa watoto ni asilimia 5.3 na idadi ya watu chini ya miaka 15 ni asilimia 44. Takwimu pia zinaonyesha kuwa maambukizi ya VVU ni asilimia 5.7, idadi ya watu wanaoishi chini ya dola 2 kwa siku ni asilimia 90 na kiwango cha ukataji wa miti ni asilimia 40.

"Hali hii inatisha kama itaachwa kuendelea bila kudhibitiwa, kwani maliasili na mazingira vitaendelea kutumika kwa kiasi cha kupitiliza na hivyo kuendelea kuharibiwa kwa mazingira ambayo yanapaswa kutunzwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho," anasema Dyegula.

Mradi ambao unatekelezwa kwa miaka minne na sasa upo katika mwaka wa tatu wa utekelezaji, pamoja na mambo mengine, unafanya kazi ya kueneza elimu ya uzazi wa mpango kwa jamii za pwani hususani katika wilaya ya Pangani kupitia kwa wasambazaji wa huduma za uzazi wa mpango katika jamii (CBDs), waelimishaji rika na wamiliki wa maduka yanayouza kondomu.

Pia mradi unahamasisha matumizi ya majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo, wanajamii kujiunga na Vikundi vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na kutoa ushauri nasaha juu ya VVU/UKIMWI na kusambaza kondomu.

"Shughuli zote hizi zina matokeo makubwa katika kuhifadhi mazingira ya pwani na kuimarisha afya ya mama na mtoto na ya jamii nzima kwa ujumla," anasema Dyegula. (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>