Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:48 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Utafiti wa Kisayansi Kusaidia Kupambana na Ujangili, Kuhifadhi Mazingira
Na Marko Gideon

DAR ES SALAAM, TANZANIA, Agosti 23, 2012 (IPS) - Jitihada za Tanzania za kupambana na ujangili na kuhifadhi mazingira katika mbuga na mapori yake ya hifadhi zinaweza kuimarika kufuatia utafiti wa njia ya satelaiti wa kufuatilia mwenendo wa tembo katika Mbuga ya Taifa ya Saadani na Pori la Hifadhi la Wami Mbiki.

Utafiti huo ambao ulianza mwaka 2010 kwa udhamini wa Mradi wa Pwani wa Mpango wa Kusimamia Mazingira ya Ukanda wa Pwani (TCMP-Pwani) unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) na kupata msaada wa Kiufundi kutoka Kituo cha Rasilimali za Bahari cha Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Rhode, umefikia hatua ya pili ya utekelezaji, ambayo kwa mujibu wa mtaalam wa masuala ya Tembo nchini Tanzania, Dk. Alfred Kikoti, inahusu kuwavua kola tembo waliovishwa kola kwa ajili ya kuwafuatilia kwa njia ya satelaiti.

"Hivi majuzi tumewavua kola tembo nane katika pori la Hifadhi la Wami Mbiki," alisema Dk. Kikoti wakati akizungumza na mwandishi wa makala hii hivi karibuni mjini Dar es Salaam.

"Matokeo ya utafiti bado yanaandaliwa, lakini moja ya matokeo ya awali tumegundua kwamba bado ujangili ni tatizo katika mbuga na mapori ya hifadhi nchini," alibainisha Dk. Kikoti ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Tembo Duniani (World Elephant Centre) kilichopo mjini Arusha. Baadhi ya picha za zoezi la kuvua tembo kola zinapatikana katika blog ya http://tcmppwani.blogspot.com/.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma Agosti 8, 2012, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alifafanua juu ya ukubwa wa vitendo vya uhalifu/ujangili nchini. "Kumekuwa na ongezeko la vitendo/wimbi la uhalifu/ujangili wa nyara za serikali ambao unaathiri rasilimali za taifa hususani wanyamapori tembo, viboko, twiga, nyati na wanyama wengine pamoja na uvunaji haramu wa mazao ya misitu," alisema Waziri Kagasheki.

Mkutano wa Waziri ulikuwa na lengo la kuwafahamisha waandishi wa habari juu ya operesheni ya kupambana na uhalifu/ujangili iliyoanza Julai 22, 2012 wilayani Liwale katika mkoa wa Lindi kukabiliana na ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Selous.

Kwa mujibu wa Waziri, maofisa wakuu waandamizi, maofisa wa kati, wakaguzi na askari wa kawaida kutoka Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Uhalifu Mkubwa Nchini ambacho kinavishirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini waliendesha operesheni hiyo.

Matokeo ya awali ya utekelezaji wa operesheni yanatisha. Kwa mujibu wa Waziri Kagasheki, meno ya tembo 14 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 164 na meno ya kiboko 80 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18.8 yalikamatwa.

Nyara nyingine ni pamoja na bangili moja ya usinga wa mkia wa tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 23.6, ngozi 2 za simba zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 15.4, ngozi ya chui yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5.5, mikia miwili ya ngedere yenye thamani ya shilingi laki 378, kichwa cha nyati chenye pembe mbili chenye thamani ya karibu shilingi milioni 3, nyama ya nyati yenye thamani ya karibu shilingi milioni 3 na kichwa cha pofu chenye pembe 2 chenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 2.6.

Kwa mujibu ya taarifa ya Waziri Kagasheki, jumla ya thamani ya nyara za serikali zilizokamatwa ni karibu shilingi milioni 213.

Fedha hizi ni nyingi mno kupatikana katika operesheni ya eneo moja tu katika nchi ambayo ina hifadhi nyingi za taifa kutoka mashariki hadi magharibi, kaskazini hadi kusini.

Pia kiasi hiki cha fedha ni kikubwa mno katika nchi ambayo wakazi wake wengi wanaishi katika umaskini mkubwa na kukabiliwa na changamoto nyingi za huduma za jamii kama vile maji, afya na elimu.

Kwa mujibu wa Dk. Kikoti, utafiti wa kisayansi wa kufuatilia mwenendo wa tembo kwa kutumia satelaiti unaweza kutoa taarifa za kutosha kwa watunga sera zitakazowawezesha kutunga sera, sheria na mikakati ya kutokomeza ujangili na kuhifadhi mazingira ya hifadhi zetu nchini.

Alisema taarifa za utafiti huo zikitumiwa vizuri na watunga sera zinaweza kupunguza kiwango cha ujangili, kuvutia watalii, kuhifadhi mazingira, kupunguza migongano kati ya jamii na wanyama, kuanzisha na kujua mapitio ya wanyama kwa nia ya kuyahifadhi, kuyalinda na kufuatilia majangili.

Hadi tembo 17 katika Mbuga ya Taifa ya Saadani na pori la Hifadhi la Wami Mbiki takribani kilomita 100 kutoka Saadani walivikwa kola tangu kuanza kwa mradi huo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mpango wa Kuhifadhi Mazingira ya Ukanda wa Pwani (TCMP), Jeremiah Daffa, ufuatiliaji wa mwenendo wa tembo pia hutumika kujua mwenendo wa wanyama wengine katika hifadhi.

"Katika zoezi la juzi la kuwavua tembo kola, tuligundua kuwa tembo mmoja aliyekuwa na kola alikuwa na jeraha la risasi," alisema Dk. Kikoti huku akionyesha picha ya tembo mwenye jeraha la risasi sikioni mwake. "Lakini nina imani atapona".

Pamoja na ujangili, utafiti huo umegundua changamoto nyingine zinazokabili Mbuga ya Saadani na pori la Hifadhi la Wami Mbiki ikiwa ni pamoja na mwingiliano wa shughuli za binadamu kama vile kilimo kisichokuwa na mpangilio, kilimo cha kuhama hama na makazi ya watu kuwepo katika maeneo ambayo yangepaswa kuwa makazi au mapitio ya tembo, ukataji miti kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa na kukata mikoko katika eneo ambapo Mto Wami unaingia baharini.

Pia changamoto nyingine zilizoonyeshwa na taarifa za awali za utafiti huo ni kuwepo kwa ujangili wa kasa wa kijani, uchimbaji wa chumvi na barabara za umma na reli kukatiza katikati ya Mbuga ya Saadani.

Ugunduzi kama huu unaweza kusaidia serikali kwa kiasi kikubwa kujua ni wapi katika hifadhi kuna vitendo vya ujangili na hivyo kuwa rahisi kuvifuatilia na kuvidhibiti. Pia kutokana na utafiti kufanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi wanaoishi ndani au kuzunguka hifadhi, unaweza kutumika kama njia mojawapo ya kuwahamasisha kujua umuhimu wa kuhifadhi rasilimali za nchi na kukabiliana na changamoto zinazokabili hifadhi ikiwa ni pamoja na ujangili. (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>