Biashara Baina ya Mataifa ya Afrika au Muungano wa Kimataifa: Utata wa Kuku na Yai? Na Isolda Agazzi
GENEVA, Juni 5 (IPS) - Pamoja na kuwa Shirika la Fedha Ulimwenguni (WTO) kwa muda mrefu limewahi kusema biashara baina ya mataifa ya Afrika iko chini mno, wataalam katika Kituo cha Kusini, chombo cha serikali mbalimbali kinachofanya tafiti katika nchi zinazoendelea, kinasema biashara miongoni mwa mataifa ya Kiafrika tayari ni muhimu katika utengenezaji wa bidhaa na inaonyesha njia mpya ya kuelekea kwenye mapinduzi ya viwanda.
"Biashara baina ya mataifa ya Kiafrika iko chini mno. Mwaka jana, ilikuwa asilimia 10 tu ya biashara katika bara hilo," Valentine Rugwabiza, naibu mkurugenzi mkuu wa WTO, ambayo inataka kupunguza vizingiti vya kukuza biashara na pia kukuza misaada kwa ajili ya biashara, aliiambia IPS.
"Pamoja na gawio la Afrika katika biashara ya kimataifa kuwa dogo mno chini ya asilimia tatu mwaka 2011 – linazidi kuongezeka kwa kasi, hususan katika nchi zenye uchumi unaoibukia; wakati biashara ndani ya Afrika zinazidi kuwa muhimu."
Kutokana na kutokubadilika kwa mgawanyo wa nguvukazi kulikorithiwa kutoka enzi za ukoloni, Afrika inaendelea kutegemea kiasi kidogo cha bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje ambazo ni malighafi: mwaka 2010, uchimbaji wa mafuta na madini uliwakilisha asilimia 66 ya jumla ya bidhaa zilizosafirishwa nje.
Kwa mujibu wa Rugwabiza, kukosekana kwa miundombinu ya uwekezaji na vizingiti visivyokuwa vya ushuru vya kila aina kunafanya biashara kati ya mataifa 54 ya Afrika kuwa ngumu.
"Wakati inachukua siku 18 kusafirisha bidhaa nje kwenda mataifa ya Amerika Kusini na Caribbean, karibu inachukua siku 33 kufanya biashara kutoka taifa moja la Afrika kwenda jingine," aliongeza, akibainisha kuwa pia ni gharama kubwa kusafirisha kontena kutoka taifa moja la Afrika kwenda jingine ikilinganishwa na kusafirisha katika mataifa mengine yaliyoendelea.
Kwa mfano, kusafirisha kontena kutoka kusini mashariki mwa bara la Asia kunagharimu dola 900, ikilinganishwa na kusafirisha kwa dola 2,000 kutoka taifa moja kwenda jingine barani Afrika; vile vile inagharimu dola 935 kuagiza kontena kutoka kusini mashariki mwa Asia, na karibu dola 2,500 kufanya hivyo ndani mwa bara la Afrika. Hata hivyo, Kituo cha Kusini kilichopo mjini Geneva kina matumaini zaidi.
"Kwa kuangalia hali kwa undani, biashara ndani ya Afrika ni ya chini," Aileen Kwa, afisa biashara wa Kituo cha Kusini, aliiambia IPS. "Katika suala la kusafirisha nje mazao yasiyokuwa ya mafuta biashara ya ndani barani Afrika iko juu huku ikisafirisha bidhaa nyingi kwenda mataifa ya EU. Zaidi ya hapo, kiwango cha ukuaji wa biashara ndani mwa Afrika ni cha pili kwa ukubwa baada ya China na mbele ya Marekani na EU. Hivyo, inaleta matumaini makubwa, pia katika suala zima la ubora wa bidhaa zinazosafirishwa nje."
Anaelezea kuwa ukiondoa Afrika Kusini, ni asilimia 10 tu ya bidhaa zinazosafirishwa nje katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinazokwenda EU zinatoka viwandani, kiwango ambacho kimeongezeka hadi asilimia 27 katika biashara kati ya kanda na kanda barani Afrika.
"Bidhaa nyingi za viwandani barani Afrika zinakwenda katika nchi za Afrika. Hivyo kama bara linataka kuwa na viwanda vingi, soko linalotoa fursa nzuri kwa Afrika siyo China, Marekani wala EU."
Kwa upande wa Rugwabiza, hata hivyo, ukuaji wa viwanda barani Afrika unahitaji siyo tu kuimarisha soko la ndani, lakini pia kuunganisha soko la dunia.
"Leo hii, sehemu za kifaa kimoja zinaweza kuzalishwa katika nchi mbalimbali duniani. Hii ni fursa kubwa kwa Afrika kubobea katika kazi moja moja na kujiweka katika mzunguko wa biashara wa kimataifa," aliiambia IPS.
"Baadhi ya nchi tayari zimeshafanya hivyo, lakini bado ni moja moja tu. Mauritius, kwa mfano, inazalisha bidhaa kwa ajili ya H&M, (duka kubwa la nguo duniani). Kutokana na kuwa na vifaa na sekta nzuri ya huduma, kampuni hiyo ya kimataifa inatambua kuwa itapata bidhaa zake kwa wakati unaotakiwa na hii imechangiwa na mazingira ya kisheria tulivu na yanayotabirika, kwani hakuna sheria ambazo zinatarajiwa kutungwa hivi karibuni," alisema.
Kwa anabainisha kuwa picha haifahamiki sana katika baadhi ya maeneo ya Afrika, kwani biashara ndani ya bara ni kubwa kuliko maeneo mengine. Jumla ya bidhaa zinazosafirishwa nje katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenda Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara tayari inazidi jumla ya bidhaa zinazosafirishwa nje kwenda EU mwaka 2000. Mataifa mengine kama vile Zambia na Senegal pia yanasafirisha bidhaa zaidi kwenda barani Afrika kuliko kwenda Ulaya.
Hata hivyo, bado kuna baadhi ya kanda zinaonyesha picha inayokatisha tamaa.
Rugwabiza ana imani kuwa Afrika, kutokana na utegemezi wake mkubwa wa biashara na dunia ya nje, inaathirika zaidi na mitikisiko ya nje. Hii inajitokeza hasa katika sekta ya kilimo, kama ambavyo mgogoro wa chakula umeonyesha.
"Mwaka 2008, Afrika iliagiza nafaka za jumla ya dola bilioni 15, huku asilimia tano tu ya nafaka zikiwa zimeuzwa nje kutoka Afrika. Ruzuku za kilimo katika nchi zenye maendeleo makubwa, uwekezaji usiotosheleza na uzalishaji duni wa kilimo na vikwazo visivyokuwa vya biashara (kati ya mataifa ya Afrika) bado ni kikwazo kikubwa," aliongeza.
Shoprite (Pty) Ltd, kwa mfano, kampuni ya kimataifa yenye makao yake nchini Afrika Kusini, inatumia nyaraka 20,000 kwa wiki kupata ruhusa ya kusambaza nyama na bidhaa za mimea katika maduka nchini Zambia pekee. Katika nchi zote ambako inafanya kazi, vibali vipatavyo 100 vinahitajika kwa kuingia mara moja kila wiki, lakini hivi vinaweza kuongezeka hadi 300 kwa wiki wakati wa msimu wa shughuli nyingi.
Kutokana na ukiritimba huu wa kisheria, kunaweza kuwepo kwa nyaraka hadi 1,600 zinazokwenda sanjari na kila lori la Shoprite lenye bidhaa linalovuka mpaka katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Lakini mambo yanaweza kubadilika. Kwa mfano, EAC imeweza kupunguza idadi ya vituo vya ukaguzi, wakati Uganda na Rwanda wameanzisha kituo kimoja cha mpaka baina yao ambacho kinafunguliwa kwa masaa 24 kwa siku.
Kwa anasema kuwa mataifa ya Afrika yanategemea kwa kiasi kikubwa kuagiza bidhaa kutoka nje kutoka soko la dunia, hususan chakula, na hiyo inatokana zaidi na kukosa uwezo wa kuzalisha.
Ana imani kuna haja ya kuwa na baadhi ya mizania kati ya malengo ya muda mfupi na muda mrefu. Wakati katika malengo ya muda mfupi nchi zinapaswa kuwa na uwezo wa kuagiza chakula haraka na kwa urahisi kadri inavyowezekana kufikia mahitaji ya lazima, katika mikakati ya muda mrefu ni lazima kuzalisha chakula chao wenyewe bila ya kutegemea kuagiza bidhaa kutoka nchi zenye maendeleo makubwa ambazo zina ushindani usiokuwa wa usawa kutokana na kupatiwa ruzuku kubwa kutoka serikalini.
Kutegemea katika uagizaji bidhaa nje kunadhoofisha wazalishaji wa ndani na uwezo wao wa baadaye. Kwa hali hii, nchi zinahitaji kutumia ushuru na sera nyingine za biashara kama hizo kupunguza baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hata kutoka kwa majirani zao, angalau kwa muda fulani.
"Kwanza nchi zinatakiwa kuongeza uwezo wao wa kuzalisha halafu biashara itafuata. Mara zote WTO inafikiri juu ya kuongeza biashara, lakini suala kubwa kwa Afrika ni jinsi gani ya kuongeza uwezo wake wa kuzalisha. Halafu biashara itafuata yenyewe," Kwa aliiambia IPS.
(END/2012)
|
|
|