Makazi Duni ya Afrika Kusini Yakabiliwa na Uhaba Mkubwa wa Maji Salama ya Kunywa Na Siphosethu Stuurman
JOHANNESBURG, Juni 5 (IPS) - Maelfu ya wakazi wa Diepsloot, makazi duni kuliko yote kaskazini mwa Johannesburg, Afrika Kusini, wamepanga foleni kwa masaa kupata maji safi na salama kwa wiki nzima baada ya maji yanayosambazwa katika eneo lao kuingiliwa na mfumo wa maji taka.
Kuchafuliwa kwa maji hayo kulitokea wakati mkandarasi anayefanya kazi katika mfumo wa maji taka wa karibuni kupasua bomba la maji ambayo yanasambazwa katika eneo la Diepsloot. Pamoja na uharibifu huo kukarabatiwa, inaaminika kuwa maji taka hayo yalichafua mfumo wa maji safi. Wakazi wa hapa walitahadharishwa na mamlaka ya Maji jijini Johannesburg wasinywe maji kutoka kwenye bomba Aprili 13.
Hata hivyo, wiki moja baada ya tukio hilo, wakazi wanasema hakuna matenki ya maji ya muda mfupi ya kutosha kusambaza maji ya bomba kwa kila mtu anayeishi katika makazi hayo duni yenye zaidi ya wakazi 150,000.
"Kila linalowezekena linafanyika, tuna matenki ya akiba 65 na matenki 12 yanayohama kwa ajili ya wakazi kuyatumia kwa muda mfupi," anasema msemaji wa Mamlaka ya Maji ya Johannesburg Millicent Kabwe, akiongeza kuwa kila tenki kati ya matenki yasiyohamishika lina uwezo wa kubeba lita 5,000.
Hata hivyo, kiongozi wa kijamii Scelo Shezi anasema matenki ya muda mfupi hayana uwezo wa kubeba maji ya kutosha kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya watu katika makazi hayo.
"Tuliambiwa kuwa hakuna usafiri wa kutosha kuleta maji zaidi katika jamii …lakini kuna haja ya kuwa na matenki mengi zaidi ya maji," anasema Shezi.
Anasema wakazi wanakosa uvumilivu.
"Tuna hofu kuwa watu wanapaswa kusubiri katika foleni kwa muda mrefu mno. Ni changamoto ya kweli, na tuna matumaini kuwa litashughulikiwa hivi karibuni," anasema.
Wakati ni wilaya moja tu, kata 113, katika makazi hayo inaonekana kuanzisha mfumo wa "familia moja, ndoo moja " baada ya mapambano kuzuka kutokana na watu kutokufurahia kuhusu idadi ya ndoo ambazo watu wanabeba kuja kuchota maji, wanawake na watoto wenye ndoo nyingi mara nyingi wanaonekana wakiwa katika foleni ndefu wakisubiri zamu zao kuchota maji.
Duduzile Ngema anayeonekana kuchanganyikiwa amekuwa katika foleni kwa karibu siku nzima.
"Hatuogi, hatuoshi vyombo … tuna tatizo kubwa hapa Diepsloot. Wanasema kuwa maji yatatoka, lakini tumesubiri kwa muda mrefu. Walituambia kuwa tunaweza kufa kama tukinywa maji yaliyochafuliwa na kupatwa na magonjwa," anasema Ngema.
Anasema hali ni ya kudhalilishana, kwani wakazi wanalazimishwa kutafuta njia mbadala za kujisetiri. Ngema hakuweza kuzungumza kwa undani, lakini anasema wakazi wanatumia ndoo na wataweza tu kutupa uchafu huo kama maji ya matenki yakiwasili.
"Ni vigumu mno kwani vyoo vyetu vinahitaji maji ya kuvuta uchafu, hivyo tunashindwa kwenda vyooni, tunatumia tu ndoo," anasema Ngema mwenye hasira.
Mkazi mwingine mwenye hasira na aliyekata tamaa, Thami Dlodlo, anasema kuwa mgogoro wa maji umefanya maisha kusimama katika jamii yake.
"Hatuwezi kupika, hatuwezi kuoga, na hatuwezi kufanya kitu chochote. Hakuna maisha bila maji, tunahitaji maji, maji safi," anasema Dlodlo.
Anasema wakazi wanalazimika kununua maji, lakini wengi wao hawana ajira na hawawezi kumudu kununua maji. Diepsloot ni makazi yasiyopangwa ambayo yana nyumba za tofali za kuchoma zilizojengwa na serikali, na kuwa na maji ya bomba na umeme, na kuna vibanda duni vya mabati na mbao ambavyo havina maji ya bomba.
Familia katika nyumba za serikali zina mita za maji na zinalipia bei ya punguzo. Hata hivyo, wakazi maskini zaidi hawawezi kumudu kulipia maji, na wanatumia mabomba ya jumuiya ambayo yanatoa maji bure katika kitongoji hicho.
"Sasa tunanunua maji, kutoka kwa watu wa mikokoteni kwa bei ya dola 1.25 kwa ndooo. Tunanunua ili watoto wetu waweze kwenda shule, na kwa ajili ya kunywa. Lakini hatufanyi kazi … hatuna fedha za kutosha kununua maji. Ni vigumu mno kwetu kwasababu hata hatuna maji ya kunywea dawa," anasema Dlodlo.
Katika baadhi ya maeneo katika kitongoji hicho maji salama yamerejeshwa, lakini Mamlaka yaMaji Johannesburg yanasema haiwezekani katika wakati huu kusema ni lini maji yatarejea kwa wakazi wote wa Diepsloot.
Mamlaka ya Maji ya Johannesburg yamekosolewa na chama cha upinzani cha Afrika Kusini cha Democratic Alliance, kutokana na kuchelewa kurejesha maji katika eneo la Diepsloot.
Hata hivyo, Profesa Akpofure Taigbenu kutoka Idara ya Uhandisi wa Maji katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand anasema inachukua siku chache tu kurejesha maji safi na salama, baada ya kuchafuliwa.
"Inachukua siku kadhaa kurejesha mfumo katika hali ya kawaida, lakini siku sita kwa maoni yangu ni nyingi. Suala muhimu ni kuwa na mtandao mzuri wa matenki ya maji; inatakiwa kuwa na umbali mdogo wa kutembea kutoka makazi ya mtu hadi kwenye matenki ya maji. Kama umbali ni mrefu, unawachosha wakazi," anasema Taigbenu.
Mamlaka ya Maji ya Johannesburg yanasema kuwa kurejesha maji safi na salama ni mchakato mrefu.
"Ugumu wa kutatua hali hii na ukubwa wa mtandao, mchakato wa kuondoa maji taka katika mfumo wa maji safi, na michakato ya kiuhandisi na kisayansi ina maana kuwa inachukua muda mrefu kidogo," anasema Kabwe. "Hatua zilizochukuliwa ambazo zinatokana na michakato hii zimeonyesha maboresho makubwa katika suala la ubora, lakini haziendani na viwango vya kitaifa bado."
Kabwe pia amehusisha matatizo ya maji ya jiji hilo na kuchakaa kwa miundombinu.
"Miundombinu ya zamani inahitaji kubadilishwa. Mamlaka ya Maji ya Johannesburg ina programu ya kuboresha miundombinu ambapo tunaboresha mifumo ya maji safi na maji taka katika jiji zima. Hii siyo changamoto ambaypo tunaweza kuikabili mara moja, lakini Mamlaka ya Maji ya Johannesburg inasonga mbele katika kushughulikia matatizo ya miundombinu," anasema msemaji huyo mwanamke.
Wakati huohuo, Waziri wa Masuala ya Maji Edna Molewa anasema Afrika Kusini inahitaji kuwekeza dola bilioni 71 katika miundombinu ya maji, huduma na mahitaji ya menejimenti katika muongo ujao. Hata hivyo Hazina ya taifa ina bajeti ya asilimia 44 tu ya kiwango kinachohitajika kuboresha huduma za maji nchini Afrika Kusini.
(END/2012)
|
|
|
| |
|
|