Vyoo Vingi, Maisha Bora Nchini Zimbabwe Busani Bafana
BULAWAYO, Zimbabwe, Juni 5 (IPS) - Serikali na wataalam wa usafi wa mazingira wanasema Zimbabwe inahitaji kuongeza jitihada za kukuza usafi na kuwekeza katika vyoo na utoaji wa maji salama, wakati nchi ikikabiliwa na ugonjwa wa homa ya matumbo.
Taifa hilo limeripoti kuwa zaidi ya watu 3,000 wamekabiliwa na gonjwa la homa ya matumbo tangu Machi. Homa ya matumbo inaambukizwa kwa kula chakula au kunywa maji yenye kinyesi cha binadamu aliyeambukizwa ugonjwa. Wagonjwa wengi wanatoka mji mkuu wa nchi hiyo wa Harare, na kwa uchache kumeripotiwa vifo vya watu wawili.
Hata hivyo, matumizi ya "vyoo vya kichakani" au kujisaidia katika maeneo ya wazi ni kitendo kinachotumika kwa kiasi kikubwa, ambapo serikali ya Zimbabwe ina mashaka juu ya gonjwa hilo. Waziri wa Rasilimali Maji wa Zimbabwe Samuel Sipepa Nkomo alisema inaonyesha mtizamo uliojengeka kwa kiasi kikubwa juu ya suala zima la usafi wa mazingira na usafi wa mwili miongoni mwa watu katika taifa hili la kusini mwa Afrika.
"Tuna tatizo kubwa la kujisaidia katika maeneo ya wazi na inabidi kufanya kazi kwa pamoja kushughulikia tatizo hilo," Nkomo aliiambia IPS.
Zimbabwe ilipata hasara kubwa katika kuwekeza kwenye programu ya usafi wa mazingira kati ya mwaka 2008 na 2009. Zaidi ya watu 4,000 walifariki kutokana na kipindupindu na zaidi ya watu 100,000 waliambukizwa kutokana na kutokuzingatia tabia za usafi na kukosekana kwa vyoo. Kipindupindu pia kinaambukizwa kwa kula chakula au maji yenye kinyesi cha mtu aliyeambukizwa.
"Kuenea kwa kipindupindu kunasemekana kusababishwa na usafi duni wa mwili na kutokunawa mikono yetu mara kwa mara. Mbali ya hilo, homa ya matumbo ni ugonjwa unaotokana na usafi duni wa mwili," alisema Noma Neseni, mkurugenzi wa Tasisi ya Maji na Maendeleo ya Usafi wa Mazingira, shirika lisilo la kiserikali ambalo ni kituo cha kikanda cha kujenga uwezo wa maendeleo ya maji na sekta ya usafi wa mazingira.
Neseni alisema changamoto kubwa ya Zimbabwe ilikuwa ni kubadili mitizamo ya watu kuhusu usafi wa mazingira na usafi wa mwili. "Hatulengi katika kukuza masuala ya usafi wa mwili, lakini katika miundombinu, jambo ambalo halipaswi kuwa hivyo."
Takwimu zilizotolewa na Mpango wa Ufuatiliaji wa Pamoja wa Shirika la Afya Ulimwenguni na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) zinaonyesha kuwa shabaha za taifa nchini Zimbabwe ni kufikia asilimia 80 ya usafi wa mazingira katika eneo la vijijini, asilimia 100 kwa maeneo ya mjini, na asilimia 100 katika kusambaza maji vijijini na mijini.
Kwa kuangalia makadirio ya karibuni zaidi ya utoaji wa huduma za usafi wa mazingira mwaka 2010, Zimbabwe inahitaji kuongeza kiasi hicho kutoka asilimia 52 hadi asilimia 77 katika maeneo ya mijini na kutoka asilimai 32 hadi asilimia 68 katika maeneo ya vijijini ili kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia, malengo nane kuhusu kupambana na umaskini na kuleta maendeleo ambayo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walikubaliana kuyafikia ifikapo mwaka 2015.
"Kama kunakuwepo na kunawa mikono kwa mara kwa mara, kusingekuwepo na mtu yoyote ambaye angeandamwa na magonjwa hayo," alisema Neseni. "Tuna maendeleo makubwa ya miundombinu, lakini miundombinu bila kubadili mtizamo hautatufikisha popote. Tunahitaji watu kuwa na ufahamu juu ya masuala ya usafi wa mwili. Sehemu ya tatizo ni kuwa tunachukulia suala la usafi wa mazingira na maji kama la serikali; tunahitaji sekta binafsi kufanya kazi kwa kushirikiana na kila mtu."
Neseni alitoa wito wa kuwepo kwa uratibu wa sekta binafsi na za umma katika kukabiliana na changamoto zinazokabili usafi wa mazingira, usafi wa mwili na ugavi wa maji nchini Zimbabwe.
Masuala haya muhimu yatakuwa masuala ya msingi katika Mkutano wa Pili wa Viongozi wa Juu kuhusu Usafi wa Mazingira na Maji kwa Wote (SWA) ushirikiano unaoendeshwa na UNICEF mjini Washington D.C. Ijumaa Aprili 20.
Mkutano huo umeleta pamoja zaidi ya mawaziri 60 wanaohusika na masuala ya maji na usafi wa mazingira na fedha kutoka mataifa zaidi ya 30 yaliyoendelea. Pia waliokuwepo walikuwa mashirika ya wahisani na mashirika ya kiraia ambayo yanafanya kazi ya kukuza upatikanaji wa maji salama, usafi wa mazingira na usafi wa mwili kwa wote (WASH) kupitia kuongezeka kwa vitega uchumi.
Kwa mujibu wa taarifa fupi ya SWA, mawaziri hao wanatarajiwa kuja na ufumbuzi wa jinsi gani ya kushughulikia mgogoro wa WASH.
Nkomo anaunga mkono kuwa hali hiyo inatokana na Zimbabwe kuwa na utendaji mbovu katika eneo hilo.
"Sisi tupo nyuma mno katika usafi wa mazingira, pamoja na kuwa ni wazuri kidogo katika ugavi wa maji," Nkomo aliiambia IPS kutoka mjini Washington D.C. "Kuzuka kwa kipindupindu mwaka 2008 na homa ya matumbo mwaka huu ni tahadhari kuhusu madhara ya kutokutumia fedha zaidi katika usafi wa mazingira na miundombinu ya maji. Lakini tunafanya jitihada kuboresha hali."
Nkomo, ambaye anaongozana na Waziri wa Fedha wa Zimbabwe Tendai Biti katika mkutano huo, alisema nchi hiyo ilikuwa inaandaa rasimu ya mkakati wa kitaifa wa usafi wa mazingira na maji kwa ajili ya kuwasilishwa kwa wadau mwishoni mwa Aprili.
"Huu utakuwa ni mfumo wa sekta nyingi za kuhamasisha watu juu ya hatari ya kujisaidia katika maeneo ya wazi, na pia kuimarisha miundombinu bora."
Mkakati utaongoza uwekezaji na kukuza usafi wa mazingira, na upatikanaji wa maji safi katika maeneo ya mjini na mijini. Wiki hii, Waziri wa Afya na Masuala ya Watoto alitoa tahadhari kuwa magonjwa yanayosababishwa na maji kama vile kipindupindu yanaondelea kuzidi kuwa tishio.
Takwimu zilizotolewa wiki hii na Kitengo cha Udhibiti wa Magonjwa ya Milipuko na Idadi ya Watu katika Wizara ya Afya na Mambo ya Watoto zinaonyesha kuwa wagonjwa wa kipindupindu waliongezeka mara mbili katika robo ya kwanza ya mwaka 2012 hadi kufikia 8,154 kutoka wagonjwa 4,000 walioripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana. Nusu ya wagonjwa hawa walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano. Wizara ilisema inajipanga kuanzisha chanjo kuzuia idadi ya watoto wanaopatwa na ugonjwa wa kipindupindu kwa watoto.
(END/2012)
|
|
|