Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:37 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Waghana Wajifunza Kuhifadhi Mazingira ya Pwani Kutoka Tanzania
Na Marko Gideon

DAR ES SALAAM, MACHI 30 (IPS) - Ujumbe wa watu kumi kutoka nchini Ghana ulihitimisha ziara ya siku 10 nchini Tanzania kwa kuelezea hadithi kadhaa za mafanikio na mifano inayofaa kuigwa na nchi yao katika kuhifadhi mazingira na rasilimali zinazopatikana katika ukanda wa pwani na bahari.

Ujumbe huo katika ziara iliyoandaliwa na Mradi wa Pwani wa Mpango wa Kusimamia Mazingira ya Ukanda wa Pwani (TCM-Pwani) ambao unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) na kupata msaada wa kiufundi kutoka Kituo cha Rasilimali za Bahari cha Chuo Kikuu cha Rhode Island nchini Marekani ulitumia siku kumi kutembelea baadhi ya miradi ya hifadhi ya mazingira na rasilimali za pwani na bahari inayoendeshwa na TCMP-Pwani na washirika wake katika vijiji vya Mlingotini wilayani Bagamoyo, wilayani Pangani mkoani Tanga, Zanzibar na Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (Marine Parks and Reserves Unit).

Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Afisa Wanyamapori kutoka Mkoa wa Magharibi mwa Ghana, Felix Nani alisema wamevutiwa mno na jinsi Tanzania inavyohifadhi mazingira na rasilimali za pwani na bahari kupitia Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu.

"Tumekuja kujifunza jinsi gani maeneo tengefu baharini yanahifadhiwa hapa kwani nchini Ghana hatuna mpango wowote wa kuyahifadhi maeneo hayo pamoja na kuwa na sheria," alisema Nani, akiongeza kuwa ziara hiyo imehusisha wadau muhimu katika eneo la kusimamia mazingira na rasilimali za pwani kutoka nchini mwao. Wadau hao ni pamoja na watendaji waandamizi serikalini, wavuvi, wachuuzi wa samaki, wasimamiaji wa wanyama pori na viongozi wa jamii zinazopatikana katika mwambao wa pwani.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Dk. Adilian Chande, kitengo chake kilichopo chini ya Idara ya Maendeleo ya Uvuvi kilianzishwa baada ya serikali kuona kuwa kulikuwa na uharibifu mkubwa katika maeneo ya bahari yenye wingi wa bayoanuwai. Hivyo ikaonekana kuna haja ya kuhifadhi maeneo hayo.

Kikiwa kimeanzishwa chini ya Sheria ya Maeneo Tengefu ya Bahari Namba 29 ya mwaka 1994, Kitengo hicho kinaendeshwa na Bodi ya Wadhamini ambayo lengo lake kuu ni kusimamia menejimenti na utawala wa maeneo tengefu ya bahari na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali katika maeneo hayo.

Kitengo kinatambua maeneo makuu matatu ya hifadhi. Maeneo ambayo matumizi ya rasilimali ikiwa ni pamoja na uvuvi hauruhusiwi kabisa ambayo kwa lugha ya Kiingereza yanajulikana kama ‘no take area’.

Maeneo ya matumizi ya jumla (general user zone), ambayo matumizi ya rasilimali hata kwa watu wanaotoka nje ya hifadhi yanaruhusiwa kwa utaratibu wa kupewa vibali maalum. Na maeneo mengine ni yale ya matumizi maalum (specified user zone) ambayo watu kutoka nje ya hifadhi hawaruhusiwi kutumia rasilimali wala kufanya uvuvi. Hata hivyo, watu wanaoishi ndani ya hifadhi wanaruhusiwa kuendesha uvuvi ila kwa kufuata utaratibu uliowekwa ikiwa ni pamoja na kutokutumia nyavu zinazokwenda chini sana hadi kuyafikia matumbawe.

"Maeneo yote hayo yanabainishwa na wadau ikiwa ni pamoja na wanajamii wenyewe wanaoishi kuzunguka hifadhi," alisema Dk. Chande.

Matamshi yake yalirejewa na Nani ambaye alisema moja ya masomo muhimu ambayo wamejifunza na wangerejea nayo nyumbani ni jinsi Tanzania inavyoweza kushawishi jamii kuwa wadau muhimu katika hifadhi ya mazingira na rasilimali za pwani. "Nimevutiwa mno na muundo uliopo kuanzia serikali kuu hadi serikali ya kijiji. Muundo huu umehamasisha jamii kushiriki na kuwa wamiliki wa miradi," alisema.

"Tumekuja kujifunza kutokana na mambo yenu mazuri, kiwango cha ushirikishwaji wa jamii, sera mlizonazo, njia zinazotumiwa na wavuvi kama ni endelevu – tumeshuhudia mengi na tumejifunza mengi."

Mjumbe mwingine, Emilia Abaka-Edu, ambaye ni mchuuzi wa samaki, pia alikiri kujifunza mengi jinsi jamii inavyoshiriki katika shughuli za hifadhi. "Nimevutiwa mno na ushiriki wa wanakijiji – kuona wanakijiji wanazingatia sheria," alibainisha.

Ushiriki wa wanawake pia ulipongezwa. Kwa mujibu wa John Eshun, ambaye ni mvuvi, ameshuhudia mazingira mapya kabisa kuona wanawake katika ukanda wa pwani wanaendesha shughuli za kuboresha vipato vyao badala ya kutegemea uvuvi pekee. "Tumeona wanawake wilayani Bagamoyo, Tanga na Zanzibar ambao wanajishughulisha na kilimo cha mwani. Wanawake hawa ni wajasiriamali wa ukweli kwani wanazalisha bidhaa mbalimbali kama vile sabuni kutokana na mwani. Wanafanya jamii za pwani kuwa na uwezo wa kuendesha maisha yao hata baada ya akiba ya samaki iliyopo baharini kupungua kwa kiasi kikubwa," alisema.

"Nimevutiwa kuona muundo uliojengeka vema, mfumo wa usimamiaji uliojengeka vizuri katika idara ya uvuvi katika kila kijiji hasa ushirikishwaji wa wanawake. Nchini Ghana, wanawake hawajashirikishwa kikamilifu katika shughuli za uvuvi, kwa kiasi kikubwa uvuvi ni kazi ya wanaume."

Lakini kuna baadhi ya mambo yanayofanana kati ya Ghana na Tanzania katika suala zima la ushiriki wa wanawake. "Kama ilivyo nchini Tanzania, nchini Ghana wanaume wengi hawauzi samaki, wanaouza ni wanawake," alisema Eshun.

Kwa upande wake, Nani alisema Ghana ina sheria mpya ya mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine, inataka kuhifadhi mazingira na rasilimali za pwani na bahari na moja ya sababu kuu za ziara yao ni kuona jinsi gani Ghana inaweza kutekeleza sheria hiyo mpya.

"Tulikuwa bado wadogo, nyie mlikuwa ni watu wazima. Mnatambua jinsi gani Mwalimu (Julius Kambarage Nyerere) na (Kwame) Nkrumah walivyoishi pamoja. Tumejifunza mambo mengi mno kutoka kwenu," aliwaambia washiriki wa mkutano wa kuwapokea wageni hao ulioandaliwa na Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu baada ya kuhimitimishwa kwa ziara hiyo iliyofanyika kati ya Mei 27 na Juni 4 mwaka jana.

Hifadhi ya mazingira ya pwani na bahari na rasilimali zake inatambuliwa na mikataba mbalimbali ya kimataifa. Kwa mujibu wa Tamko la Jeddah la Kukuza Utekelezaji wa Mipango ya Kikanda ya Kuhifadhi Bahari kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu wa mwaka 2007, rasilimali za bahari na pwani ni chanzo kikuu na akiba kubwa ya chakula, huchangia kuimarisha uchumi na afya ya watu wengi duniani.

Tamko hilo linasema mazingira na rasilimali za pwani na bahari yanakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na madhara ya kuendelea kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira ya bahari na pwani.

Tamko la Cape Town la Mpango wa Afrika wa Kukuza na Kulinda Mazingira ya Pwani na Bahari, hasa katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara la mwaka 1998 linatambua "umuhimu wa mazingira ya pwani na bahari kama chanzo kikuu cha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi, na chanzo cha ustawi wa watu wake".

Kwa upande wake, Tamko la Jeddah linatoa wito wa kukuza na kuongezeka kwa ushiriki wa mamlaka za kitaifa na kikanda, wanajamii na wadau wengine katika kusimamia na kuhifadhi mazingira na rasilimali za pwani na bahari.

Hata hivyo, utekelezaji wa Ghana wa yale waliyojifunza kutoka nchini Tanzania juu ya hifadhi ya mazingira na rasilimali za pwani kwa kushirikisha wanajamii hautakuwa rahisi sana. Kwa mujibu wa Dk. Chande, hatua za awali za kuanzisha hifadhi za bahari siyo rahisi sana kwani kuna wakati inabidi matumizi ya nguvu yatumike ili kuhakikisha sheria zinazingatiwa, "kwani siyo rahisi kwa wanajamii wote kukubaliana na mambo mazuri, ni lazima wengine watapinga".

"Katika miaka mitano ya awali nina uhakika kuwa mtakabiliwa na baadhi ya upinzani, lakini baada ya hapo wanajamii watawaelewa na kuwa wadau kamili", alisema Dk. Chande. (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>