Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:56 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Wadau wa Mazingira Bagamoyo Wataka Mikoko Itunzwe
Na Marko Gideon

DAR ES SALAAM, Mar 1 (IPS) - Wadau wa mazingira wilayani Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani wameishauri serikali na wadau wengine kuongeza jitihada za kutunza mikoko katika mwambao wa Bahari ya Hindi ikiwa ni pamoja na katika maeneo ambayo mito inaingia baharini.

Waliyasema hayo mjini Bagamoyo Februari 7, 2012 wakati wa mkutano wa Kamati ya Mjumuisho wa Sekta Mbalimbali katika Kusimamia Mazingira ya Pwani (ICM) katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Mkutano huo ulilenga kujadili mpango kazi wa Mradi wa Pwani wa mwaka 2012 unaolenga Kusimamia Mazingira na Rasilimali za Pwani na Bahari (TCMP Pwani Project) unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID).

Wakitoa maoni yao kwenye mkutano huo, wadau wa mazingira walisema pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali, hali ya sasa ya misitu ya mikoko katika mwambao wa pwani hairidhishi. Ukataji wa mikoko umeshaacha baadhi ya maeneo yakiwa hayana rasilimali hiyo kabisa.

Baadhi ya maeneo yanayolalamikiwa na wadau ni kijiji cha Mlingotini pamoja na maeneo mengine wilayani Bagamoyo. Walisema tatizo la ukataji mikoko kwa kiasi kikubwa linatokana na wawekezaji, ambao wanapopatiwa ardhi kwa ajili ya kilimo huomba kibali cha kukata miti hiyo adimu duniani kwa ujanja katika vijiji husika, jambo ambalo halikubaliki kisheria.

Mikoko ni miongoni mwa miti adimu ambayo inahifadhiwa na serikali kisheria kutokana na umuhimu wake kwa bayoanuwai katika ukanda wa pwani. Umuhimu wake ni pamoja na kuwa mazalia mazuri ya samaki, kuzuia chembe chembe za michanga zifike baharini na kuyafunika matumbawe na pia katika kuhifadhi mazingira ya pwani kwani huzuia mmomonyoko wa ukingo wa bahari na maingilio ya mito unaotokana na mawimbi makubwa ya bahari.

"Mikoko hutumika kama makazi, chakula na mazalia ya samaki wakubwa, kamba wadogo na chaza," inasema ripoti ya Usimamiaji Shirikishi wa Mikoko nchini Tanzania, iliyoandikwa na Martin E Adams.

Mikoko pia inawindwa kwa udi na uvumba na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kutokana na faida yake kubwa wanayoipata kwa kuuza miti hiyo. Mbali na matumizi mengine, miti ya mikoko hutumika kwa kutengenezea mashua. Pia hutumika kwa mkaa, ujenzi wa nyumba, dawa za miti shamba, uzalishaji wa asali na chakula cha mifugo kwa jamii mbalimbali za pwani na Zanzibar. Ni kutokana na faida hiyo, mikoko inazidi kukatwa hata kama ni kinyume cha sheria kukata miti hiyo.

Serikali inatambua umuhimu wa mikoko na mustakabali unaotishia kutoweka kwa rasilimali hiyo. "Mwaka 1987, marufuku ya uvunaji wa mikoko nchini kote ilitangazwa na Mkurugenzi wa Misitu," inasema ripoti hiyo ya Usimamiaji Shirikishi wa Mikoko. Na mwaka 1991, Mpango wa Taifa wa Kusimamia Mikoko ulianzishwa ambapo rasilimali hiyo iliwekwa chini ya udhibiti wa Mkurugenzi wa Misitu ambaye ndiye pekee mwenye mamlaka ya kutoa kibali kwa mtu yoyote kukata mikoko.

Lakini hali ya mambo katika ngazi ya jamii ni tofauti kabisa, kwa mujibu wa wadau hao wa mazingira. "Kuna mgongano mkubwa wa mamlaka ya kiutawala," walisema, na kuongeza kuwa wakati sekta ya misitu imepewa mamlaka ya kusimamia mikokoko, kwa mfano, sekta ya ardhi inapopima ardhi kwa ajili ya kugawa viwanja au kwa ajili ya wawekezaji haizingatii mamlaka waliyopewa sekta ya misitu – eneo linalopimwa na kupewa mwekezaji linakatwa mikoko yote.

"Kama wajumbe wa ICM tunapaswa kupunguza migongano ya kisekta," waliazimia wadau hao. "Haiwezekani mtu wa ardhi akapima bila kuzingatia mipaka.

Walisema kuwa hali ilivyo sasa inaonyesha wawekezaji wengi wanapopewa eneo la fukwe wanadhani wanamiliki eneo lote la bahari. Walisema hali hiyo imesababisha mikoko kukatwa katika ufukwe mkubwa wa Bagamoyo katika maeneo kama vile Nunge na Mlingotini.

"Watu walipanda mikoko, wawekezaji wakaikata," alisema mmoja wa wadau hao, akiongeza kuwa hiyo kwa kiasi kikubwa inatokana na maamuzi yasiyozingatia maamuzi wala matumizi ya sekta nyingine.

Aliwataka wajumbe wa ICM kukaa chini na kujua jinsi ya kutoa maamuzi ya kisekta. "Unapaswa kujua sekta yangu inahitaji nini, sekta ya mwenzangu inahitaji nini, na wala siyo katika uholela huu ambao unahatarisha uendelevu wa rasilimali zetu," alishauri.

Wakati wadau wakilalamika juu ya kuendelea kwa ukataji na uvunaji mikoko katika mwambao wa pwani ya Bagamyo, sheria ya ardhi inajulikana kuwa wazi juu ya matumizi mbalimbali ya ardhi. Inatambua maeneo ya hifadhi, ardhi ya hifadhi, ardhi ya kijiji na ardhi ya kawaida, walisema wanakamati hao. "Huwezi kupima ardhi katika eneo linalotambulika kuwa ni la hifadhi. Hii inaweza kufanyika tu kwa kubadili matumizi ya ardhi hiyo, na mamlaka ya kutoa uamuzi kama huo yapo chini ya Rais peke yake," alifafanua mjumbe mmoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TCMP Bwana Jeremiah Daffa, alisema elimu ya ufahamu wa mazingira inahitajika kuzidi kutolewa kwa watu mbalimbali. "Tuzidi kutoa elimu kwa watu mbalimbali. Watu wanapaswa kuzidi kupata elimu ya uhifadhu na utunzaji wa mazingira, lakini kama wataachwa hali itazidi kuwa mbaya," alitahadharisha.

Wakati mkurugenzi wa TCMP akitoa tahadhari ya hali kuja kuzidi kuwa mbaya, wadau wa mazingira walisema tayari hali imeshakuwa mbaya kwani taarifa zinaonyesha kuwa kuna ukataji mkubwa wa mikoko katika mto Ruvu kiasi cha kufanya maji ya chumvi kutoka baharini kukaribia mtambo wa maji wa Ruvu.

"Sasa maji ya bahari yanapanda hadi maeneo ya daraja la barabara ya kuelekea Msata. Kuna wakati yalikaribia Mitambo ya Kusukuma Maji ya Ruvu. Hali ikiachwa iendelee kuna wakati maji yanayosukumwa kwenda Dar es salaam yatakuwa ya chumvi," alidai mmoja wa wajumbe hao.

Wajumbe wa ICM walitoa wito kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanajamii wa pwani na mashirika mbalimbali kushiriki katika kuhakikisha uendelevu wa miti hiyo. TCMP Pwani kwa kupata msaada wa kiufundi kutoka Kituo cha Rasilimali za Bahari cha Chuo Kikuu cha Rhode Island, ni moja ya mashirika yanayohamasisha kwa vitendo upandaji na uhifadhi wa mikoko.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Mradi huo, Baraka Kalangahe, moja ya shughuli zinazofanywa na mradi wake wa miaka minne tangu mwanzoni mwa mwaka 2010 ni kuhifadhi misitu ya mikoko.

Alisema kutokana na jamii za pwani kuishi katika mazingira ambayo yana rasilimali ambazo zisipotumika kwa uendelevu zitaisha, mradi wake, pamoja na mambo mengine, unapambana kuhakikisha kuwa misitu kama ile ya mikoko haitoweki. "Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa udhalimu unaofanywa na binadamu haumalizi rasilimali hizi," aliwaambia wajumbe wakati wa mkutano wa ICM. "Kwa kufanya hivyo tunalinda rasilimali, wanyama na viumbe hai waliopo katika misitu hiyo," aliongeza.

Kuna njia nyingi ambazo mradi unazitumia kuhakikisha mikoko haimaliziki. Moja ya njia hizo ni kusaidia mamlaka za vijiji na wilaya kutunga sheria ndogo ndogo za kuhifadhi misitu ya mikoko.

Mfano mzuri wa sheria ndogo ndogo ni ile ya kijiji cha Kiharaka ambayo, pamoja na mambo mengine, inataka kuwezesha na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika kutunza, kutumia na kuhifadhi maliasili zilizopo katika kijiji cha Kiharaka.

Madhumuni mengine ni kusaidia utunzaji wa ikolojia katika misitu ya mikoko na bahari katika kijiji na kuchukuliwa kwa hatua za kisheria katika kusimamia maliasili zilizopo ikiwa ni pamoja na uwezo wa kutoa adhabu kwa wale wanaokiuka taratibu za usimamiaji shirikishi wa mipango ya maliasili za kijiji. (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>