Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   20:13 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Kuhamasisha Kilimo cha Embe Kupunguza Madhara ya Mabadiliko ya Tabia Nchi
Marko Gideon

DAR ES SALAAM, Feb 6, 2012 (IPS) - Mabadiliko ya tabia nchi yapo kila mahali, ni dhahiri na madhara yake yanajidhihirisha kwa uwazi zaidi kuliko siku za nyuma. Yanaathiri watu kutoka kila sekta na nyanja zote za maisha. Watu wanaoathirika zaidi ni wale wanaoishi katika nchi zinazoendelea hususan katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wake wanategemea kilimo cha mvua.

Wataalam wanabashiri kuwa kilimo katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kitaathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi. Hadi ifikapo mwaka 2050, mabadiliko katika mwenendo wa hali ya hewa utasababisha kupungua kwa wastani wa mavuno ya mpunga, ngano na mahindi kwa asilimia 14, 22 na asilimia tano kwa mpangilio huo hapo juu, hii ni kwa mujibu wa shirika lenye makao yake mjini Washington DC lijulikanalo kama Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Sera za Chakula (International Food Policy Research Institute).

"Kila mtu anatambua mabadiliko katika mwenendo wa mvua, ambayo yamekuwa na madhara makubwa kwa mamilioni ya watu ambao wanategemea kilimo cha mvua, hususan barani Afrika," alisema Dk. Tomaz Salomão, katibu mkuu wa Jumiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika alipokuwa akitoa maoni yake juu ya msimamo wa Afrika katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa 17 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi Ulimwenguni (COP 17), uliofanyika mjini Durban, Afrika Kusini, kuanzia Novemba 28 hadi Desemba 9 2011.

Tanzania na hasa jamii za pwani, ni miongoni mwa waathirika wakuu wa mabadiliko haya.

"Mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri … kuongezeka kwa maji ya bahari kunaathiri ardhi ya kilimo na kumeza baadhi ya visima vya maji baridi katika mwambao wa Tanzania bara pamoja na Zanzibar, na hivyo kuongeza changamoto za kimaendeleo kwa jamii za pwani ambazo kwa kiasi kikubwa hutegemea kilimo cha kujikimu kuendesha maisha yao," alisema Waziri wa Nchi wa Zamani katika Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira - Dk Batilda Burian, alipokuwa akizindua Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani jijini Dar es Salaam mwaka 2009.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mradi wa Pwani wa Ushirika wa Kusimamia Rasilimali na Mazingira ya Pwani (TCMP Pwani) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani USAID), "madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yanaonekana wazi katika maeneo mengi ya pwani nchini Tanzania. Madhara yanatarajiwa kuongezeka zaidi katika siku zijazo na kuharibu kabisa bayoanuwai tete katika maeneo hayo, kuathiri vibaya wakazi wa pwani, watumiaji wa rasilimali za pwani, maeneo ya burudani, miundombinu, uvuvi na utalii kama hakutachukuliwa hatua za haraka na madhubuti.

Jumuiya maskini za pwani mara nyingi ndizo zinazoathirika zaidi na zenye uwezo mdogo wa kujikwamua na madhara hayo.

Ili kusaidia jamii za pwani kuendesha maisha katika mazingira ya mabadiliko ya tabia nchi, mradi wa TCMP Pwani uliendesha tathmini ya kujua madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi na mipango ya kuendesha maisha katika hali hiyo ya mabadiliko katika vijiji vya Mlingotini na Kitonga wilayani Bagamoyo.

Ripoti ya tathmini iligundua kuwa vijiji hivyo viwili vinakabiliwa na tishio la kuongezeka kwa maji ya bahari, maji ya chumvi kuvamia vyanzo vya maji baridi, uharibifu wa miundombinu katika mwambao wa pwani, kupungua kwa uzalishaji wa zao la biashara la mwani, kupungua kwa samaki wanaovuliwa, kuongezeka kwa mafuriko, ukame na mvua zisizokuwa za kuaminika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali ya mabadiliko ya tabia nchi inahitaji hatua madhubuti kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa jamii za pwani katika vijiji hivyo zinaendesha maisha yao hata baada ya kujitokeza mabadiliko makubwa zaidi ya hayo. Moja ya ufumbuzi ni kuwa na mipango ya shughuli mbadala kama vile upandaji wa mazao ambayo hayawezi kuathirika kiurahisi na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kilimo cha embe katika kijiji cha Kitonga katika eneo la Ruvu kwenye njia kuu ya magari yaendayo mkoani wilayani Bagamoyo, mradi wa majaribo ulioanzishwa na wanakijiji wa Kitonga na kupatiwa msaada na TCMP Pwani, unatarajiwa kuwa habari njema ya mafanikio ya baadaye ya jinsi wanajamii katika maeneo ya pwani wanavyoweza kuendesha maisha yao katika hali ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kijiji cha Kitonga na mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Tabia Nchi ya Kijiji, Hamis Njagila, mradi ulianza Septemba 2010 kwa kuchagua wajumbe 12 – 6 wanaume na sita wanawake katika Mkutano Mkuu wa Kijiji ili kuunda Kamati ya Mabadiliko ya Tabia Nchi ya Kijiji kuanza utekelezaji wa mradi wa majaribio wa kilimo cha embe. Kamati ilichagua kilimo cha embe baada ya ushauriano na Kamati ya Mazingira ya Pwani ya Wilaya ya Bagamoyo na wataalam wa mabadiliko ya tabia nchi wa mradi wa TCMP Pwani, baada ya kufanya ziara ya kubadilishana uzoefu katika kijiji cha Mlingotini na baada ya kuhudhuria warsha ya kuongeza ufahamu wa mabadiliko ya tabia nchi.

Jitihada za jamii zimewezesha kusafishwa kwa ekari 24 za ardhi, inayomilikiwa na kamati hiyo chini ya utaratibu wa umiliki wa ardhi wa kijiji. Mradi una lengo la kupanda miche ya miembe ipatayo 1250 chini ya usimamizi wa karibu wa watalaam wa mabadiliko ya tabia nchi wa TCMP Pwani na maofisa ugani wa wilaya ya Bagamoyo.

Upandaji wa miembe ulichaguliwa na kamati ili kuongeza faida kwa jamii na mazingira. Miembe inaweza kuzalisha matunda kwa ajili ya chakula, kipato kutokana na kuuza matunda hayo pamoja na mbao na asali pale inapotumika kwa ufugaji wa nyuki. Miembe pia inatoa kivuli, inazuia mmomonyoko wa udongo na inaweza kupunguza ongezeko la joto duniani kutokana na uwezo wake wa kunyonya hewa ukaa. Pia inaweza kusaidia wanajamii kufaidika na kipato kutokana na mpango wa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu za viwandani kutokana na uangamizaji wa misitu (REDD).

"Tuliamua kuhamasisha wanajamii kupanda miti ya miembe kutokana na faida nyingi zinazotokana na miti hiyo kwa ajili ya maisha yao na mazingira," anasema Jairos Mahenge, mkuu wa timu ya wataalam wa mabadiliko ya tabia nchi katika TCMP Pwani.

Hata hivyo, mipango ya kuwezesha jamii kuendesha maisha wakati wa mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo ya pwani haiwezi kutekelezwa bila ya kuwepo kwa changamoto. "Utekelezaji wa mipango ya kuwezesha jamii kuendesha maisha katika mabadiliko ya tabia nchi kunaleta changamoto mpya na hata uwezekano wa kusababisha migogoro. Wataalam wa masuala ya pwani wanahitaji kufahamu hali hii na kuishughulikia mapema," kinasema Kijitabu cha Mwongozo kwa Wana Mipango ya Maendeleo Kuwezesha Jamii Kuendesha Maisha katika Mabadiliko ya Tabia Nchi Kwenye Maeneo ya Pwani.

Moja ya changamoto kubwa ni mabadiliko ya hali ya hewa yanayojitokeza kila mara ambayo yanaweza kuathiri mipango ya kuwawezesha wananchi kuendesha maisha yao katika mabadiliko.

Kwa upande wa TCMP Pwani, zoezi la upandaji miche ya miembe ilibidi kufanyika katika majira ya ukame kwa kutumia umwagiliaji. Kamati ya mabadiliko ya tabia nchi katika kijiji cha Kitonga ilipendekeza maji ya kumwagilia shamba hilo katika eneo hilo lenye uhaba mkubwa wa maji yatokane na chanzo kilichopo umbali wa kilomita nne kutoka shambani. Wanakamati wanatumia madumu ya ujazo wa lita 20 ili kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa.

Mpango wa kupanda miche hiyo ya miembe wakati wa ukame ulitokana na dhana kuwa "mabadiliko ya tabia nchi hayana majira, tunaweza kukaa kwa miaka mitatu bila mvua, je katika hali kama hiyo ya mabadiliko makubwa ya hali ya hewa tunafanyaje?" anauliza Mahenge. "Kuna jibu moja tu, kukabiliana na hali kadri inavyowezekana".

Mahenge anasema hii ni sababu kuu ni kwa nini mradi huo wa majaribio ulianza kutekelezwa wakati wa ukame. Anasema madhara ya mabadiliko ya tabia nchi katika ngazi ya jamii yanahitaji hatua za kukabiliana nayo ambazo hazitegemei moja kwa moja mvua.

"Siyo jambo rahisi kufanya kwani suala lenyewe lina mambo mengi yanayohusiana. Linagusa, miongoni mwa mambo mengine, maeneo muhimu mno ambayo ni msingi wa maisha ya watu. Mambo hayo ni pamoja na kilimo na usalama wa chakula, masuala ya afya na ajira," alisema Dk. Salomão.

"Tunachotakiwa kukubaliana nacho ni kwamba watu wanatakiwa kuja pamoja kuokoa ubinadamu, dunia yetu na kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinakuwa na maisha bora," aliongeza.

Wanajamii katika kijiji cha Kitonga wameshasikia wito huu. Mradi huo wa majaribio una lengo la kuhamasisha wengine katika kijiji na mazingira yanayozunguka kijiji kujifunza njia za kuendesha maisha katika mabadiliko ya tabia nchi. Taarifa zinaelezea kuwa tayari mradi umeshaanza kuvutia wanakijiji wengine ambao wanataka kuanzisha kilimo chao cha embe cha jumuiya. Lakini, matokeo kamili bado hayajapatikana.

"Habari ya mafanikio inatarajiwa kusikika baada ya miaka 3 wakati wanafamilia wetu watakapoanza kufaidi matunda kwa ajili ya chakula na kuboresha maisha yao kutokana na vipato vinavyotokana na kuuza matunda hayo", alisema Njagila. (END/2012)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>