Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:37 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Kutunza Mazingira kwa Kufuatilia Mwenendo wa Tembo
Marko Gideon

DAR ES SALAAM, Des 6 (IPS) - Ikiwa imeanzishwa rasmi Septemba 2005, Mbuga ya Taifa ya Saadani (SANAPA) ni ya kipekee nchini Tanzania kutokana na kuwa na mazingira tofauti na mbuga nyingine. Ni mbuga pekee yenye mazingira ya pwani, mkono wa bahari, nchi kavu na bahari. Mazingira haya yanaifanya kuwa na viumbe mbalimbali wa bahari na nchi kavu pamoja na bayoanuwai ya kipekee.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mbuga ya Saadani iliyotolewa katika warsha ya wadau wa utekelezaji wa mradi wa Pwani, mbuga hiyo ni muhimu na ina uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa watalii kama ikitunzwa vizuri kutokana na uwepo wake karibu na jiji la Dar es Salaam.

Moja ya shughuli zinazofanywa na mradi wa Pwani uliopo chini ya Ushirika wa Kusimamia Mazingira ya Pwani na Bahari (TCMP) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kwa kushirikiana na wadau wengine katika kuhifadhi na kulinda mazingira, ni pamoja na kufuatilia mwenendo wa tembo katika mbuga hiyo na eneo tengefu la Wami Mbiki. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TCMP, Jeremiah Daffa, lengo la mradi huo ulioanza kupokea ruzuku kutoka TCMP mwaka 2010 hadi Septemba 2012 ni kupunguza migongano kati ya jamii na wanyama, kuongeza utalii kwa kutambua wanyama walipo, kuanzisha maeneo ya mapitio ya wanyama kwa nia ya kuyahifadhi na kuyalinda na kuijengea Mbuga ya Saadani uwezo wa kuisimamia vizuri.

Hadi sasa tembo 17 katika mbuga hiyo na eneo tengefu la Wami Mbiki lilipo umbali wa takribani kilomita 100 upande wa maghariobi wamevikwa kola.

Mbali na mradi huo, shughuli nyingine zinazofanywa kuhifadhi mbuga hiyo ni pamoja na kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa wanajamii wanaozunguka mbuga, kusaidia miradi ya maendeleo ya jamii na kuhifadhi wanyama, mikoko na rasilimali za bahari.

Kwa kiasi kikubwa kazi hizo zinawezekana kutokana na ushirikiano uliopo kati ya sekta za umma na zile za binafsi (PPP) katika kusimamia na kuhifadhi mazingira ya SANAPA. Mbali na mradi wa Pwani, mmoja wa wadau wakuu kutoka sekta binafsi katika mpango huo ni Tent With A View Safari Lodge ambayo, miongoni mwa mambo mengine, imeanzisha kituo cha kutoa taarifa za hifadhi ya mbuga ya Saadani katika mazingira ya hoteli hiyo kinachojulikana kama ‘Saadani Wildlife Research Centre’. Kutokana na kituo hicho, wageni mbalimbali wanaotembelea SANAPA hupatiwa elimu juu ya bayoanuwai na miradi ya kuhifadhi mazingira inayoendelea katika mbuga hiyo, ikiwa ni pamoja na mradi wa kufuatilia tembo.

Hata hivyo, pamoja na mipango mizuri na jitihada za kuhifadhi na kulinda mazingira ya mbuga, Saadani inakabiliwa na changamoto kadhaa mojawapo ikiwa ni mwingiliano wa shughuli za binadamu kama vile kilimo kisichokuwa na mpangilio, kilimo cha kuhama hama na makazi ya watu kuwepo katika maeneo ambayo yangepaswa kuwa makazi na mapitio ya tembo, ukataji miti kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa na kukata mikoko katika eneo ambapo Mto Wami unaingia baharini.

Tishio jingine ni ujangili wa kasa wa kijani ambao ni moja ya wanyama waliopo katika hatari ya kutoweka duniani wanaopatikana katika eneo la mbuga hiyo, uchimbaji wa chumvi na barabara za umma na reli kukatiza katikati ya mbuga.

Akizungumzia tatizo la migongano kati ya binadamu na wanyama linalokabili mbuga ya Saadani, Mtaalam wa Hifadhi ya Tembo na Mkurugenzi wa shirika la ‘World Elephant Centre’, Dk. Alfred Kikoti alisema kwamba utafiti wa kufuatilia mwenendo wa tembo unaofanywa kwa kutumia utaaalam mkubwa wa satelaiti umegundua kuwa ng’ombe wengi wanazidi kuelekea eneo la mbuga na hivyo kutishia wanyama waiaishio katika mbuga hiyo. Hata hivyo, alisema tatizo hilo siyo la Saadani pekee, bali linazikabili mbuga nyingine nchini kama vile Selous na Katavi.

"Hii inafanya kuwepo kwa shinikizo kubwa kutokana na shughuli za binadamu – tuna shinikizo la ng’ombe, ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa, wawekezaji wakubwa wanaochukua maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya kuyaendeleza bila kutumia mfumo wowote wa upangaji wa ardhi," alisema wakati wa mkutano wa mpango kazi wa mradi wa Pwani mapema mwezi Novemba 2011.

Alisema Saadani ni mbuga ndogo mno kuweza kukabiliana na shinikizo la binadamu na mifugo na wakati huo huo kuongezeka kwa idadi ya wanyama. "Tunapaswa kukabiliana na shinikizo la kibinadamu na mwenendo wa mifugo kwa kuwa na mpango wa kupanga matumizi ya ardhi," alipendekeza. "Kama hatutachukua hatua sasa, Saadani itakuja kupungua hadi kufikia hatua ya kupoteza hadhi yake ya kuitwa Mbuga ya Taifa".

Wadau wa hifadhi ya mbuga hiyo kama vile World Elephant Centre wanasisitiza ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili SANAPA na mbuga nyingine nchini Tanzania.

"Tunadhani hatua za haraka za dharula zinahitajika kama tunataka kuzuia kuanguka kwa sekta nzima ya wanyamapori nchini Tanzania na hadhi yake kama kivutio kikubwa cha watalii," linasema shirika la World Elephant Centre katika tovuti yake. "Ushiriki wa wadau wote umethibitisha bila mashaka kwamba … inawezekana kukabiliana na hali ambayo … tayari imeshaanza kuelekea kuwa janga. Hali iliyopo inahitaji ushiriki wa sekta za umma na binafsi kwa kutumia hatua za dharula za muda mfupi na mikakati ya muda mrefu itakayotekelezwa na mamlaka za hifadhi za taifa … kwa kushirikiana kikamilifu na wanajamii wanaozunguka maeneo ya hifadhi".

Ili kusimamia vema mazingira ya SANAPA na viumbe hai waishio humo pamoja na rasilimali zake, kuna haja ya kuunganisha mipango mbalimbali ya usimamiaji, kuchukuliwa kwa hatua na kutunga sera kwa kuzingatia mtizamo mpana wa kimazingira, kisiasa, kijiografia, kiuchumi na kiutamaduni, alisema Halima Kiwango wa SANAPA wakati wa warsha ya wadau wa mradi wa Pwani Agosti 24 na 25 2011 jijini Dar es salaam.

Wadau katika mkutano huo waliitaka World Elephant Centre kufanya uchambuzi wa takwimu ambazo tayari zimeshapatikana kupitia njia ya satelaiti ili kutumika katika kushawishi watunga sera katika ngazi ya kitaifa.

Pamoja na changamoto zinazoikabili SANAPA, mkurugenzi wa TCMP ana matumaini na jitihada zinazoendelea kuhifadhi mbuga hiyo. Ana imani kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali tayari umeshaleta matunda katika kuhifadhi mbuga hiyo. "Haya ni mafanikio makubwa kwani wadau mbalimbali wanahamasika kufanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa mazingira ya Saadani na rasilimali zake yanahifadhiwa na kulindwa," anasema Daffa. "Jitihada za kuhifadhi mbuga zimesababisha binadamu katika jamii zinazozunguka mbuga kuishi kwa amani pamoja na wanyama bila kubughudhiana."

Maneno yake yanafanana na yale ya mtendaji katika ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Constantine Shayo ambaye aliwaambia wanakijiji wa Saadani mwaka huu kuwa yeye binafsi alishangazwa na jinsi binadamu wanavyoweza kuishi pamoja na wanyama katika mbuga hiyo.

"Nimesikia kuwa simba wa hapa hawashambulii binadamu kwasababu mmekuwa marafiki wakubwa wa mazingira kiasi kwamba wanyama wana chakula kingi cha kutosha na hivyo hawana muda wa kuwabughudhi," Dk Shayo aliwaambia wanakijiji waliohudhuria mkutano wa ujumbe anaouongoza kama mwenyekiti wake wa Timu ya Kusimamia Miradi Inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) katika Shule ya Msingi Saadani. (END/2011)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>