Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:37 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Wanajamii Wachangia Katika Kuhifadhi na Kuongezeka Kwa Idadi ya Kasa
Na Marko Gideon*

Dar Es Salaam, Oct 10 (IPS) - Uhifadhi wa viumbe hai wa bahari walio katika hatari ya kutoweka iliyojikita katika jamii umefanikiwa kuongeza idadi ya kasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi nchini Tanzania tangu mwaka 2009.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Mradi wa Kuhifadhi Kasa wa kijiji cha Ushongo wilayani Pangani, Kikundi cha Marafiki wa Maziwe na shirika la hifadhi za viumbe wa bahari la SeaSense zinaonyesha kuongezeka kwa idadi ya kasa walioanguliwa na viota tangu mwaka 2009.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kijiji cha Ushongo ambaye pia ni mmoja wa viongozi katika mradi wa kasa, Mungia Mgaza, kutokana na kazi ya hifadhi, viota vya kasa viomeongezeka kutoka 19 mwaka 2009 hadi 81 mwaka 2010. Kasa walioanguliwa wameongezeka pia kutoka 440 mwaka 2009 hadi 5,839 mwaka 2010.

Takwimu za shirika la SeaSense zinaonyesha pia kuonegzeka kwa kasa walioanguliwa katika nusu ya mwaka 2011. Kwa mujibu wa SeaSense, vifaranga 3,221 wa kasa walianguliwa kwa mafanikio katika kipindi cha Januari hadi Juni 2011.

Katika ripoti yake iliyowasilishwa katika mkutano wa nusu mwaka wa wadau wa Mradi wa Pwani unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na kutekelezwa na Ushirika wa Kusimamia Mazingira ya Pwani na Bahari (TCMP) jijini Dar Es Salaam Agosti 24 na 25, 2011, SeaSense ilisema viota 53 vya kasa wa kijani vilipatikana na kuhifadhiwa na viota vingine 13 vilihamishwa kutoka kisiwa kilichozama baharini cha Maziwe.

Katika jitihada za kuhamasisha ushiriki wa wanajamii katika kuhifadhi kasa, shirika hilo limeanzisha mtandao wa maofisa wa hifadhi katika vijiji sita wilayani Pangani: Choba, Ushongo, Kikokwe, Sange, Mkwaja na Madete.

Shughuli nyingine za hifadhi ni pamoja na mafunzo kwa maofisa wa uhifadhi wa kijiji cha Sange, mafunzo kwa wafanyakazi wa hoteli ya Saadani Safari Lodge juu ya jinsi ya kuwahifadhi na kuwatunza kasa, warsha za elimu ya mazingira kwa walimu 32 wa shule za msingi na wavuvi katika kijiji cha Sange ambao walipatiwa mafunzo ya jinsi ya kutoa kasa walionaswa katika nyavu za uvuvi.

Mgaza anakubali kuwa hifadhi imevutia utalii wa wageni wa ndani na nje ya nchi ambao huja kushuhudia jinsi kasa wanavyoanguliwa. Mapato yanayotokana na utalii wa kasa yameweza kuboresha vipato na maisha ya wanakijiji, ambao wengi wao sasa wanasaidia katika kazi ya uhifadhi. Kwa mujibu wa SeaSense, utalii wa kasa umejitokeza kutokana na fursa za kuangalia kuanguliwa kwa vifaranga. "Sehemu ya mapato ya utalii inagawiwa kwa kijiji kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii, " ilisema SeaSense katika ripoti yake kwenye mkutano wa wadau wa mradi wa TCMP Pwani.

"Sitaki kusema wanakijiji wanaingiza fedha nyingi, lakini wanaingiza kipato kutokana na kazi ya uhifadhi, kuwatunza kasa. Wanasafiri katika maeneo mbalimbali ya fukwe kutafuta viota na mayai, kama wakiyapata wanayaleta katika eneo la kuangulia," alisema mwanachama wa Kikundi cha Rafiki wa Maziwe, Kesrtin Erler wakati wa ziara ya kikazi ya maofisa wa TCMP Pwani katika kijiji cha Ushongo hivi karibuni.

Mbali ya kukusanya mayai ya kasa kutoka pande mbalimbali za fukwe na Kisiwa cha Maziwe, pia wanafuatilia kuanguliwa kwa kasa. "Kwetu sisi jambo muhimu katika mradi huu nikufanya kazi pamoja," aliongeza.

"Ni mradi usiokuwa na ukomo, ikiwa tutaendelea kuwa na fedha za kuendesha mradi, tutaendelea nao, miaka mitano, miaka kumi na hata miaka arobaini."

Kasa ni miongoni mwa viumbe wa bahari waliopo katika hatari ya kutoweka, kwani tafiti duniani kote zinaonyesha kuwa miaka hamsini iliyopita kulikuwa na kasa wengi baharini kuliko ilivyo sasa, alisema Erler, akiongeza kuwa kuna sababu nyingi ni kwa nini idadi ya kasa inazidi kupungua siku hadi siku.

"Tunakula kasa, tunakula mayai, tunajenga hoteli katika fukwe zinazotumiwa na kasa kwa ajili ya kutaga na kuangulia vifaranga," alibainisha.

Kuna ongezeko la shughuli za binadamu katika pwani ya wilaya ya Pangani. Kwa mfano, kuna hoteli za kitalii zipatazo 5 katika ufukwe wa kijiji cha Ushongo, kulingana na Mgaza. Hoteli hizi ni pamoja na Emayani Beach, Driftars, Tulia, Mkombozi na Beach Crab. Akiandika kwa ajili ya tovuti ya Geographic News, Fredrica Lindsay anasema kwa kuanguliwa kwa kasa, mwanga ni muuaji mkuu. Mwanga unawafukuza kutoka kwenye viota vyao katika fukwe kuelekea kwenye eneo lenye mwanga mkali zaidi ambalo mara nyingi ni eneo la maji linalogawa pwani na bahari ambalo halijaendelezwa.

"Lakini maendeleo ya mwambao wa pwani — taa zenye mwanga mkali, taa kali za maeneo ya kuegesha magari na kwenye majengo zinaweza kuwachanganya na kuvuruga mwenendo wao wa kutaga. Kasa jike mwenye mayai mengi na vifaranga wanaweza kudanyanyika na kukimbilia kwenye taa za kutengenezwa na mwanadamu," anasema Lindsay. "Wakati vifaranga wanapokimbilia mitaani na kwenye maegesho ya magari, wanakufa kwa wingi katika mazingira hayo."

Kulingana na shirika la Turtle Foundation, "kasa wamekuwa wakiishi katika sayari dunia zaidi ya miaka milioni 150 iliyopita na inadhaniwa kuwa itakuwa vigumu kuwepo kwa kasa katika bahari na sayari hii katika siku za usoni, kama hatua kubwa za kuwatunza hazitachukuliwa."

Shirika hilo linasema katika tovuti yake kuwa ni kasa 1 hadi 2 tu kati ya 1,000 ambao wanaanguliwa wanakua na mara wanapofikia umri mkubwa wanakabiliwa na maadui wakuu wawili: papa na adui mkubwa zaidi ni mwanadamu.

Lakini wakati maendeleo katika fukwe za Tanzania ni ya msingi, "ni muhimu kuhifadhi kasa kuwarejesha kwenye Bahari kwasababu wana mchango mkubwa katika Bahari, hasa kasa wanaofugwa hapa (Pwani ya Pangani)," alisema Erler. "Hawa ni wasafishaji wa matumbawe, wanakula uchafu unaozunguka matumbawe, na kama hakuna viumbe wanaokula uchafu huo matumbawe yanaweza kufa. Hii ni njia mojawapo ya kuleta usawa wa mfumo wa bayoanuwai".

Alisema watu katika kijiji walikuwa wanakula kasa siku zilizopita, lakini sasa wanasema hawali tena kasa na wanashiriki katika uhifadhi. "Ikilinganishwa na miradi mingine, huu ni mradi mdogo sana, lakini unafanya kazi," aliongeza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TCMP, Jeremiah Daffa, Mradi wa TCMP unatoa ruzuku kwa shirika la SeaSense ambalo linasaidia juhudi za wanajamii katika baadhi ya vijiji vya Pangani kuhifadhi kasa.

Hata hivyo, pamoja na juhudi za wanajamii ambazo zimeongeza idadi ya kasa, changamoto zinaendelea kuwepo. Mgaza alisema baadhi ya wavuvi haramu katika vijiji vya jirani wanaendelea kuvua kasa hata kama ni kinyume na sheria za kitaifa na kimataifa.

Kulingana na SeaSense, uuaji wa kasa na matumizi ya nyavu haramu kwa ajili ya kuvulia ni moja ya changamoto kubwa zinazokabili uhifadhi wa viumbe hao wa bahari wanaoelekea kutoweka. Shirika hilo lilirikodi kuuawa kwa kasa 23 kati ya Januari na Juni 2011.

Kulingana na mkurugenzi wa TCMP, watu wanakula kasa kutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni imani kuwa nyama ya kasa inaongeza umri wa kuishi na mayai yanaongeza nguvu za kiume kwa wanaume wasiokuwa na nguvu au wenye nguvu ndogo.

*Mwandishi anapatikana katika barua pepe gidey2000@yahoo.com. Makala za IPS zinaweza kuchapishwa bure katika chombo chochote cha habari. Chombo kikihitaji picha zinapatikana kwa kutuma maombi kwenye anuani hapo juu (END/2011)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>