Inter Press Service News Agency
Sunday, September 22, 2019   19:38 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Sanaa Iletayo Uzima
Marko Gideon

PANGANI, TANGA, Julai 15, 2011 (IPS) - Pangani siyo wilaya mpya nchini Tanzania. Wengi wanatambua wilaya ya Pangani kuwa moja ya wilaya zilizoanzishwa miaka mingi na moja ya vitovu vya ukoloni na biashara nchini Tanzania. Mji wa Pangani uliopo katika eneo Mto Pangani unapomwaga maji yake katika Bahari ya Hindi, upo umbali wa takribani Kilomita 42 kutoka Tanga mjini.

Unapoingia katika mji wa Pangani unapokelewa na vitu vingi ambavyo kama ni mgeni lazima utashangaa. Miongoni mwa vitu hivyo ni majengo ya zamani ambayo yana historia ya ukoloni. Moja ya majengo hayo ni lile linalotumika kama ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Zipporah Pangani. Umbali wa takribani mita mia mbili kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika mji huu mdogo unaokadiriwa kuwa na wakazi elfu hamsini, unakutana na mandhari nzuri ya Mto Pangani unavyomwaga maji yake katika Bahari ya Hindi. Kandokando mwa mto huo mkubwa kuna barabara ambayo imepangiliwa vizuri pamoja na kwamba imejaa mashimo ambayo yanaashiria lami iliyotengenezwa wakati wa zama za mkoloni. Pia kuna majengo na bustani ambapo vyote hivyo vimepangiliwa vizuri na kuleta mandhari ya kupendeza ya mji huo mkongwe nchini.

Mbali na Mto Pangani na kuona majengo ya zamani, mgeni pia ataona mabango yamebandikwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo yakiwa na nembo ya UZIKWASA. Neno hili linasimama badala ya shirika lisilokuwa la kiserikali katika wilaya hiyo lijulikanalo kama Uzima kwa Sanaa.

"Uliposikia neno uzima kwa sanaa ulihisi nini?" Hassan Bumbuli, mmoja wa maofisa wa shirika hilo alimuuliza kwa utani mwandishi wa makala hii alipotembelea ofisi zao Juni 6 na 7 mwaka huu, akiwa ameambatana na ujumbe wa maofisa wengine kutoka Ushirika wa Kusimamia Mazingira na Rasilimali za Pwani na Bahari (TCMP) ambalo linafadhili baadhi ya miradi ya UZIKWASA. "Ulihisi ungekuta watu wakicheza ngoma ndani ya majengo yetu?" aliongea kwa utani Bw Bumbuli na mwandishi kumjibu kwa utani pia "Ndiyo, nilidhani ningekuta kazi nzito ya kucheza ngoma humu ndani".

TCMP ni shirika linalofanya kazi kwa kushirikiana na Kituo cha Rasilimali za Pwani na Bahari (Coastal Resource Centre) chini ya Chuo Kikuu cha Rhode Island nchini Marekani, serikali ya Tanzania chini ya Shirika la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) na kufadhiliwa kwa kiasi kikubwa na Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

Pengine siyo jambo la kushangaza kuona kuwa wengi nchini Tanzania wanahusisha suala zima la sanaa na uchezaji ngoma na pengine michezo ya kuigiza au uchoraji. Lakini UZIKWASA inatafsiri tofauti ya dhana hiyo ya sanaa.

Ndani ya moja ya ofisi zake tatu zilizopo kandokando mwa Mto Pangani, shirika hilo limetandaza machapisho mbalimbali kuhusu VVU na UKIMWI, elimu ya uzazi na kujamiiana kwa vijana, matumizi ya kondomu, elimu ya malaria kwa watoto na wajawazito, magonjwa ya ngono na ushauri nasaha na kupima VVU – yote haya yakifanya kazi ya kuonyesha jinsi gani sanaa inaweza kuleta uzima.

Kwa mfano, unaweza kushuhudia machapisho yenye vichwa vya habari kama vile "Maswali waliyouliza vijana kuhusu UKIMWI na kizazi kipya", "Maswali waliyouliza vijana kuhusu mimba", Mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke", "Maswali waliyouliza vijana kuhusu mahusiano ya kimwili", Maswali waliyouliza vijana kuhusu matumizi ya kondomu", Walinde watoto na wajawazito dhidi ya malaria", "Yafahamu magonjwa ya ngono na athari zake", "Mbinu maalum za kumpa kijana kupambana na maisha", "Kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto", "Fahamu ushauri nasaha na kuchunguzwa maambukizo ya VVU na chapisho juu ya elimu ya "Kuingia utu uzima".

Haya yote yanatoa picha kuwa UZIKWASA siyo shirika la kufundisha uchezaji wa ngoma, bali linatumia aina zote za sanaa ili kulinda maisha ya mwanadamu hasa vijana wa kike na wa kiume.

Moja ya shughuli za UZIKWASA ni kukabiliana na maambukizo ya VVU/UKIMWI katika vijiji vya wilaya ya Pangani. Kazi hii hufanywa kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi wa vijiji chini ya Kamati za UKIMWI za Vijiji (Village Multi-sectoral AIDS Committees-VMAC). Na moja ya shughuli za shirika hapa ni kutoa elimu ya jinsi ya kukabiliana na VVU/UKIMWI na pia kusambaza kondomu kwa walengwa ambao miongoni mwao ni pamoja na kundi la wavuvi ambalo linaonekana kuwa katika hatari ya kuambukizwa VVU/UKIMWI kutokana na asili ya kazi zao.

"Kazi zao zinawafanya kuwa mbali na nyumbani kwa muda mrefu ambapo huishi kwenye makambi. Wavuvi wa kiume na kike wanapokuwa makambini wanaweza kuanzisha tabia hatarishi," anasema Ofisa Mradi wa UZIKWASA, Novatus Urassa. "Tabia hatarishi pia zinaweza kujitokeza wakati wavuvi wa kiume wanapokutana na wanawake na mabinti wanaokwenda kununua samaki kwa ajili ya uchuuzi."

Alisema mwaka huu mradi huo unaopokea ufadhili kutoka Mradi wa Pwani (Pwani Project) wa TCMP ulifikia vijiji 6 na wavuvi 200. Mwaka ujao unatarajia kufikia vijiji vyote 33 katika wilaya ya Pangani.

Mwandishi wa makala hii alipotaka kujua ni sababu zipi zilisababisha UZIKWASA kutekeleza mradi wa kusambaza kondomu, Urassa alisema ilitokana na mapungufu kadhaa ya matumizi ya kondomu wilayani humo. Haya ni pamoja na kuwepo kwa vituo vichache vilivyouza bidhaa hiyo, kuwepo kwa wauzaji wachache na hivyo kusabisha upatikanaji kuwa mgumu. Iligundulika kuwa tatizo la usambazaji na matumizi duni ya kondomu lilitokana kwa kiasi kikubwa na imani za kidini na kitamaduni juu ya matumizi ya kondomu. Viongozi wa dini walihubiria waumini wao kuwa kondomu ni dhambi.

Utafiti wa kubainisha maeneo yanayosambaza kondomu ulioendeshwa na UZIKWASA uliweza kujua nani wanauza kondomu, idadi ya kondomu zinazouzwa kwa siku, kwa nini wengine hawauzi kondomu na kama wanapenda kuuza siku zijazo.

UZIKWASA imepata mafanikio katika eneo hili. Kulingana na maofisa wake viongozi wa kidini wanaonekana kukubali kuwa VVU/UKIMWI haina dini. Hii imewafanya wasiendelee kuhubiri tena dhidi ya kondomu wala kutetea matumizi yake.

"Wameendelea kuhubiri maadili mema kama njia nyingine ya kujikinga na VVU/UKIMWI bila kugusia masuala ya matumizi ya kondomu," anasema Urassa. Pia usiri uliogubika suala zima la kuongelea kondomu mbele ya umma umeanza kuondoka. Kwa kiasi sasa watu wanaweza kusimama mbele ya umati na kuendelea kuchangia katika mjadala unaohusu matumizi ya kondomu.

Sanaa inayoleta uhai haishii kwenye kupambana na magonjwa pekee, lakini pia kwenye kusaidia shughuli za kuongeza kipato ili wananchi waweze kuendesha maisha yao bila shida. Hapa unakutana na mradi wa Vikundi vya Kuweka na Kukopa (SACCOs). Kwa sasa UZIKWASA inalenga katika kuhakikisha kuwa makundi yenye matatizo zaidi katika jamii kama vile walemavu, yatima, wajane na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI yanajengewa uwezo wa kuanzisha SACCOs zao au kujiunga na SACCOs zilizopo.

UZIKWASA ina redio yake ya jamii ambayo bado haijaanza rasmi kurusha vipindi. ikiwa bado kwenye majaribio haijaruhusiwa bado na Tume ya Mawasiliano nchini kurusha vipindi rasmi isipokuwa muziki. Lakini itakapoanza kurusha vipindi rasmi, redio hiyo ya jamii inatarajiwa kuwa mhimili mkubwa wa kueneza kwa wananchi kazi zinazofanywa na TCMP na UZIKWASA. Vipindi ambavyo vinaandaliwa kwa kushirikiana na wananchi sasa ni pamoja na kampeni na elimu ya mazingira, afya, VVU/UKIMWI, ujasiriamali na uzazi salama. Kwa hiyo, redio ya jamii Pangani ni chombo kingine kitakachosaidia kuleta uzima kwa njia ya sanaa wilayani humo.

"Hongereni kwa kazi nzuri mnayoifanya katika wilaya yangu. Ni kazi ambayo unaweza kuipima na tunaiona" alisema Mheshimiwa Zipporah Pangani, Mkuu wa Wilaya ya Pangani alipokuwa akizungumza ofisini kwake na ujumbe wa TCMP Juni 6, 2011. (END/2011)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The download of the specified resource has failed.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>