HAKI-MALAWI Nchi Siyo Salama kwa Mashoga Na Claire Ngozo
LILONGWE, Machi 13 (IPS) - Kwa kasi kubwa Malawi inazidi kukosa usalama kwa mashoga kwani polisi wa nchi hiyo hivi karibuni walianzisha kampeni ya kuwinda na kukamata watu maarufu wanaotuhumiwa kwa ushoga.
Polisi wanadai wanapeleleza masuala yanayohusiana na ‘tabia za ushoga’ kwani ushoga ni kinyume cha sheria nchini Malawi.
Uwindaji huo unafuatia sherehe ya uchumba ya wanaume wawili, Tiwonge Chimbalanga na Steven Monjeza, ambayo ilifanyika katika mji maarufu kibiashara nchini humo, Blantyre, katika Siku ya Sikuu ya Pili ya Krismasi (mwaka 2009). Wapenzi hao walikamatwa siku mbili baada ya kufunga ndoa na tangu wakati huo wamekuwa kizuizini wakati wakisubiri kusikilizwa kwa kesi yao.
"Tulizindua upelelezi kwasababu tuna taarifa kuwa kuna watu maarufu nyuma ya Tiwonge Chimbalanga na Steven Monjeza," alisema Dave Chingwalu, msemaji wa polisi wa kanda ya kusini mwa Malawi.
Watu maarufu katika jamii ni pamoja na wabunge, viongozi wa dini na wasomi ambao wanatuhumiwa katika upepelezi huo, kulingana na Chingwalu. Polisi haijatoa majina ya watu ambao wanalengwa katika upepelezi huo.
Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika katika miezi ya hivi karibuni imekuwa na ubaguzi zaidi. Feb. 9, Davis Mpanda, 29, alihukumiwa miaka 10 jela baada ya kukutwa na hatia ya kufanya mapenzi kinyume na maumbile. Vifungu vya 153 na 156 vya Kanuni za Makosa ya Jinai vinalifanya kosa la ushoga kuwa la jinai na mtu yoyote atakayekutwa na kosa chini ya vifungu hivi anaweza kufungwa jela miaka isiyopungua mitano na isiyozidi 14.
Hakimu Diana Mangwana wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lunzu Kusini, mjini Blantyre alimkuta na hatia Mpanda pamoja na mshikaji wake, kijana mwenye umri wa miaka 15. (Umri wa kuolewa nchini Malawi ni miaka 15.) Kijana huyo alimwambia hakimu kuwa alikubali kufanya ngono na Mpanda mara tano.
Mahakama ilimwachia kijana huyo wa kiume huru, akisema adhabu yake ingekuwa "maumivu ya kisaikolojia ambayo ataishi nayo katika maisha yake yote".
"Makosa haya yanakiuka maadili ya Malawi. Mhalifu ni mdhalilishaji kwasababu alichokifanya kwa kijana wa umri mdogo ni sawa na rushwa ya ngono. Alimtumia kijana huyo kutimiza haja zake za kimwili zisizokuwa za kawaida," Mangwana alisema wakati akitoa hukumu mahakamani.
Mtu mwingine ambaye aliangukia katika msimamo wa kukabiliana na mashoga nchni Malawi ni Peter Sawali, 21. Feb. 8, alikutwa na hatia na kuhukumiwa kufanya kazi za jumuiya kwa wiki mbili na mahakama ya hakimu wa Blantyre kutokana na kubeba bango lililokuwa linatetea haki za mashoga kandokando ya barabara kuu katika mji huo wa kibiashara, Barabara ya Masauko Chipembere.
"Sawali alikutwa na hatia kufanya tendo ambalo lina uwezekano wa kuvuruga amani," alisema Beatrice Mwachande, msemaji wa polisi mjini Blantyre.
Tony Chirwa mwenye umri wa miaka sitini alikamatwa Feb. 19 baada ya kushukiwa kumlawiti mwanaume mwenye umri wa miaka 23. Chirwa yupo kizuizini mwa polisi.
Kiongozi wa juu wa serikali pia alishazungumzia kukerwa na tabia za ushoga. Waziri wa Jinsia, Watoto na Maendeleo ya Jamii Patricia Kaliati, Jan. 19 hakukubaliana na uamuzi wa mahakama nchini Malawi kumwachia mwanamke msagaji katika wilaya maarufu kwa kilimo cha chai ya Mulanje.
Nellie Somanje wa Mulanje, ambako Kaliati ni mbunge wake, alikutwa hana hatia na mahakama baada ya kutuhumiwa "kufanya mapenzi na wasichana wawili" wenye umri wa miaka 15 na 18, ambaye alimwajiri.
Hakimu wa Daraja la Pili wa Mulanje, Lameck Mkwapatira, alisema katika hukumu yake kuwa alimwachia Somanje kutokana na kukosa ushahidi dhidi yake na kwamba wasichana hao walimweleza kuwa walikubali kuwa na mahusiano ya kimapenzi naye.
Hata hivyo, Kaliati anamshutumu hakimu kutokana na kuhamasisha ushoga na "kuweka mfano mbaya" nchini. Waziri aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa alimfukuza Somanje kutoka eneo hilo na tangu wakati huo ameshamrejesha katika "wilaya anakotokea ", ya Mangochi, katika mwambao wa Ziwa Nyasa.
Mashirika ya haki za binadamu yana wasiwasi kuhusu kulengwa kwa mashoga. Uwindaji wa mashoga utasababisha "kundi hili tete" kujificha, kulingana na Gift Trapense, mkurugenzi wa haki za binadamu katika Kituo cha Maendeleo ya Watu.
Trapense aliiambia IPS kuwa maambukizi ya VVU miongoni mwa wanaume wanapofanya mapenzi na wanaume wenzao yako "juu mno" katika asilimia 21.4. Kiwango cha maambukizi nchini ni asilimia 12. "Tayari ni suala zito linalotia wasiwasi kuwa wako katika tishio kubwa la VVU. Uwindaji wa polisi ni ukiukwaji wa jumla wa haki za binadamu kwani wananyima mashoga haki ya kuishi kwa uhuru," alisema Trapense. "Watakwenda mbali mno kuwinda mashoga."
Vile vile, nchi inasubiri hatma ya wapenzi ambao ni watu maarufu, Monjeza na Chimbalanga. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Blantyre Nyakwawa Usiwa Usiwa ameweka Machi 22 kuwa siku ya kutoa hukumu yake juu ya kesi hiyo. Kesi hiyo imevuta hisia za watu wengi ndani ya Malawi na kimataifa.
Shirika la Human Rights Watch, Amnesty International na wabunge wa bunge la Uingereza wamelaani jinsi mashoga wanavyotendewa nchini Malawi. Baada ya kukamatwa kwake, wapenzi hao wamechunguzwa akili na kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.
Serikali ya Norway, moja ya wafadhili wakuu wa Malawi, ilionya serikali ya Malawi kuheshimu haki za mashoga ama sivyo inajiweka katika hatari ya kuvuruga rikodi yake ya haki za binadamu.
"Tunatambua kuwa Malawi imepata mafanikio makubwa katika haki za binadamu lakini kuna wasiwasi maalum juu ya kuendelea kubaguliwa kwa jumuiya ya mashoga," Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Erik Solheim aliuambia mkutano wa wanahabari. Solheim yupo katika ziara fupi nchini Malawi.
"Kimataifa, suala la ushoga halihusiani tu na haki za binadamu lakini pia kulinda makundi ya wachache kama ilivyo kwa mashoga. Serikali haipaswi kukiuka haki za msingi za mtu mmoja mmoja," alisema Solheim.
Jitihada za wanandoa mashoga nchini humo za kupinga hukumu hiyo mahakamani zimegonga mwamba. Wanasheria wanaowawakilisha Chimbalanga na Monjeza wameitaka mahakama ya katiba kuchukua msimamo wa suala hilo. Walitoa hoja kuwa Kanuni za Kuendesha Makosa ya Jinai zilizotumiwa kukamata wanandoa hao zinapingana na haki za mtu binafsi, utu, imani, dhamira na uhuru wa kujieleza.
Lakini mwanasheria mkuu nchini, Lovemore Munlo, alitupilia mbali ombi hilo kwa misingi ya kiufundi katika sheria. Munlo alisema katika uamuzi wake kuwa ombi la wanasheria wa wanandoa hao lilikosa usahihi juu ya hukumu ambayo mahakama ya katiba ilitarajia kuiidhinisha.
(END/2010)
|
|
|