SIASA-NIGERIA Katika Kivuli cha Wanaume: Wanawake Wanabaguliwa Katika Siasa Mustapha Muhammad
KANO, Machi 12 (IPS) - Miaka kumi baada ya Nigeria kurejea katika utawala wa kiraia bado wanawake wanapewa nafasi ya pili katika siasa zilizojaa wanaume katika taifa lenye wakazi wengi zaidi Afrika, wanasema wanaharakati na wanasiasa wanawake.
Tangu taifa hilo la Afrika Magharibi lenye wakazi milioni 140 kujinasua kutoka kwenye utawala wa kijeshi na kurejea katika utawala wa demokrasia ya vyama vingi bila kurejea nyuma mwaka 1999, wanaume wamekuwa vibosile wakati wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya wapiga kura (asilimia 54), wanashikilia nafasi chache tu ndogo ndogo za kuchaguliwa.
"Pamoja na kwamba ni muongo sasa tangu nchi irejee kwenye utawala wa kiraia bila kurejeshwa nyuma, wanawake wa Nigeria bado wanapigania suala la kubaguliwa kisiasa ambapo hawapewi nafasi ya kushika vyeo vya kuchaguliwa kisiasa," Rabi Musa, mwanaharakati wa haki za wanawake aliiambia IPS.
"Pamoja na kuboreka kwa kiasi kwa ushiriki wa wanawake na uwakilishi katika siasa kati ya mwaka 2003 na 2007, uboreshaji huo hauonyeshi nguvu ya wanawake kitakwimu," alisema Musa, mratibu wa shirika la Women’s Right Advancement and Protection Alternative (WRAPA).
Kati ya mwaka 1999 na 2003 jumla ya wabunge wanawake 15, walichaguliwa. Takwimu hizi ziliboreka kidogo kutoka mwaka 2003 hadi 2007 na kwa sasa kuna wanawake 26 katika bunge.
Nigeria imetia saini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake lakini wanawake nchini wanaendelea kutoa sauti yao dhidi ya siasa kuendelea kuwa chini ya wanaume.
"Sisi wanawake ni wapiga kura wengi lakini wakati wa uchaguzi ni vigumu kupewa fursa sawa kufikia ndoto zetu za kushiriki kikamilifu katika siasa za nchi yetu kupitia ofisi za kuchaguliwa," mwanasiasa mwanamke Maryam Jari aliiambia IPS katika mkutano wa kisiasa.
"Mkutano wa Beijing unahitaji kila nchi ambayo ilishiriki katika mkutano kutenga asilimia 30 ya nafasi na ofisi za umma kwa ajili ya wanawake lakini nchini Nigeria bado hatujafikia asilimia hata 10," Jari alisema.
Kwa nini kubaguliwa?
Sababu za kijamii, kitamaduni na kidini zinachangia zaidi ubaguzi wa wanawake katika siasa za Nigeria, hasa katika sehemu ya nchi yenye Waislam wengi ambapo siasa zinaonekana kama jambo la wanaume tu.
Siasa za Nigeria zinatumia gharama kubwa kwani zinahitajika kutumia fedha nyingi kupanga na kuhamasisha kuungwa mkono kushinda uchaguzi. Nchini Nigeria, wagombea wanawake wanapata ufadhili kutoka kwa wafadhili.
Wanawake nchini Nigeria hawajawezeshwa kiuchumi kama ilivyo kwa wanaume. Katika jumuiya nyingi wanawake ni tegemezi kiuchumi kwa waume zao ambao hudhibiti kipato cha familia. Hata wakati wanawake wanaruhusiwa kujihusisha katika shughuli za kuwaingizia fedha, waume zao wanadhibiti fedha hizo. Mairo Usman, mwanasiasa katika jiji la Kano kaskazini mwa Nigeria, alisema nguvu duni za kiuchumi kwa wanawake zinachangia wanaume kudhibiti siasa.
"Wanawake nchini Nigeria wana fedha chache kwa mbali kuliko wanaume na hata katika siasa kuna pengo kubwa la kiuchumi kati ya wanaume na wanawake, jambo linalowafanya wanaume kuwa na ushindani mkubwa dhidi ya wanawake kwasababu ni wao wenye fedha za kutupa na kushinda kura," Usman alisema.
"Wale miongoni mwetu ambao tunataka kuingia ofisi za kisiasa tunahitaji msaada wa kifedha kutoka kwa wanaume ambao mara nyingi wanapendelea kusaidia wanaume wenzao kutokana na mfumo dume ambao unatembea kwenye mishipa ya damu ya wanaume wetu," alisema.
Siasa zinatumia muda mwingi huku wanasiasa wakitembea mbali na mara nyingi wakitumia usiku hotelini mbali na nyumbani wakati wa mikutano ya siasa. Mikutano hiyo ya kisiasa mara nyingi ina fujo na wakati mwingine ghasia zinaibuka wakati majambazi wa kisiasa wanapochukua nafasi ya kati, wakitoa matusi na kupiga silaha zilizotengenezwa kienyeji. Kutokana na mazingira hayo, wanasiasa wanawake kwa ujumla wanaonekana wenye wapenzi wengi wa kufanya nao ngono katika jamii ambayo ina imani kuwa jukumu la mwanamke linapaswa kusimamia nyumba.
"Mara nyingi tunaonekana kama wanawake rahisi kuchukuliwa na wanaume kwasababu ni wanasiasa ambao, kwa asili ya siasa, wanakaa nje usiku wa manane wakihudhuria mikutano ya kisiasa na mara nyingine wanalala hotelini mbali na nyumbani," Jari aliiambia IPS.
"Siasa zinahusisha kuingiliana na wanaume na wanawake na utamaduni wetu na dini kwa kiasi kikubwa unazuia kuchangamana kati ya wanawake na wanaume ambako kunaonekana kama kutokuwa na heshima," aliongeza.
Aisha Suleiman, mkazi wa Kano, awali alisita kujiunga na siasa za kibaguzi kutokana na unyanyapaa unaotokana na kujiunga huko. Alisema mtizamo mbaya wa baadhi ya mashabiki wa siasa wanawake, ambao wanaonyesha wanasiasa wanawake kama "wasiofunzwa tamaduni" na "wakatili" ilimkatisha tamaa kujiingiza katika siasa.
"Jinsi mashabiki wa siasa wanawake wanavyorusha lugha za matusi, kutumia madawa na vilevi vingine katika mikutano ya siasa kunawafanya wasiwe wanaowajibika," Suleiman alisema.
Haja ya kuleta tofauti na mabadiliko ya mtizamo wa umma dhidi ya wanasiasa wanawake hatimaye ulibadili mawazo ya Suleiman na alijiingiza kwenye siasa.
"Kama sote tunabaki nje na kuruhusu wanawake hawa wasiojengeka kitamaduni kuendelea kuonyesha mitizamo yao mibaya katika siasa, hatutaweza kuchukuliwa kwa uzito," Suleiman mwenye umri wa miaka 25-alisema.
Mohammed Ali Mashi, mkuu wa shirika la haki za binadamu la General Improvement of Persons Initiatives (GIOPIN), alisema mila na imani za kidini zinazopotoshwa zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kubaguliwa kwa wanawake kisiasa.
Viongozi wa dini ya Kiislam wenye msimamo mkali wanafanya kampeni na katika redio kulaani ushiriki wa wanawake katika siasa kuwa ni kwenda kinyume na imani za Kiislam. Mashi alipinga viongozi hao wenye msimamo mkali, akisema kuwa mawazo yao hayakilishi msimamo halisi wa Uislam.
Mashi ana imani wanawake polepole wanaachana na mawazo ya aina hiyo na kujiingiza katika siasa na kugombea ofisi za kuchaguliwa kutokana na kampeni za kuhamasisha umma. Hata hivyo, alisema kampeni zaidi zinapaswa kuimarishwa kupunguza pengo kubwa la kisiasa kati ya wanaume na wanawake.
"Kutokana na kwamba Uislam unahamasisha wanawake kusaka elimu, sioni sababu ni kwa nini jamii kunyima wanawake usawa wa kisiasa na wanaume kwasababu pia wana haki ya kuchangia katika kujenga taifa kama ilivyo kwa wanaume," Mashi alisema.
Hatua za kubadili hali
NGOs za jinsia kama vile WRAPA zimeanzisha kampeni ya uhamasishaji kuondoa unyanyapaa wa kuwa na wapenzi wengi wa kufanya nao ngono kwa wanasiasa wanawake. "Sote tuko nje kuondokana na mawazo ya umma ya imani kuwa wanasiasa wanawake wana wapenzi wengi na hulala hotelini wakati wa mikutano na kufanya mapenzi wanapohitaji," alisema Musa.
"Tunashangaa ni kwa nini jamii haioni wanasiasa wanaume ambao hulala hotelini kwa ajili ya mikutano (ya kisiasa) kwamba ni wazinzi. Ni kwa nini wanawake? Inavunja moyo sana," alilaumu.
(END/2010)
|
|
|