MAENDELEO - CAMEROON Je Wanawake Ni Sababu ya "Kukosekana kwa Shauku la Uchaguzi"? Mohamadou Houmfa
YAOUNDE, Machi 12 (IPS) - Mtandao wa kusaidia ushiriki wa wanawake katika siasa, unakosoa kile unachokiita "kukosekana kwa shauku la uchaguzi", baada ya kubaini kuwa kuna ongezeko la watu kutokushiriki katika uchaguzi.
Shirika la kiraia la ‘More Women in Politics’ (Wanawake Zaidi katika Siasa), limetumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kushughulikia suala hilo na kujadili baadhi ya mikakati yake wakati wa mkutano mjini Yaounde, mji mkuu wa Cameroon, Machi. 8.
Uchaguzi wa wabunge na manisipaa katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati mwaka 2007 ulishuhudiwa na kiwango cha chini cha ushiriki.
Kulingana na takwimu zilizochapishwa na waziri wa utawala wa majimbo na madaraka mikoani, ni wananchi milioni tano tu wa Cameroon walijiandikisha kupiga kura mwaka 2007 nje ya jumla ya wakazi milioni 18. Na asilimia 62 ya hao, wananchi milioni tatu wa Cameroon, waliweza kupiga kura.
Kurejesha wapiga kura wa Cameroon, ambao kwa hakika wamechoshwa na michezo ya kisiasa, kwa sasa ni kilio cha vikundi vingi vya kisiasa na mashirika kadhaa ya kijamii nchini.
Mtandao wa ‘More Women in Politics’ ni sehemu ya harakati hii. Ulizinduliwa na kundi la wanawake wakiongozwa na Justine Diffo, mwanasheria anayefundisha katika Chuo Kikuu cha Yaounde II.
"Wanawake pekee ni asilimia 52 ya wakazi wote wa Cameroon, hivyo wanabeba uzito mkubwa wa wakazi ambao wanapaswa kuhamasishwa kujiandikisha kwa wingi na kushiriki zaidi katika mchakato wa uchaguzi," Diffo aliiambia IPS.
"Wanawake lazima wajiandikishe kupiga kura. Lakini kwanza wanahitaji nyaraka zao rasmi. Wakati ambapo leo hii kuna wanawake wanaokwenda kwenye biashara zao za kila siku bila ya kuwa na vitambulisho vya taifa," Catherine Abena, Waziri wa Ulinzi wa Wanawake na Familia, alisema wakati wa mkutano.
Guy Parfait Songué, mwanasayansi wa siasa na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Douala, makao makuu ya kiuchumi, alisema kuwa ushiriki mdogo wa wananchi wa Cameroon – ikiwa ni pamoja na wanawake – katika mchakato wa kisiasa una mizizi yake kutoka kwenye ghasia za mchakato wa kupinga ukoloni.
"Kuna mgogoro wa kweli wa uraia nchini Cameroon. Lazima kusahau kuwa moyo wa nchi hii ulivunjika wakati wa kabla ya uhuru na wakati wa miaka 10 iliyofuata uhuru. Wazalendo ambao walipigania uhuru wa nchi walivunjwa moyo na walowezi wa Kifaransa. Hii imedhoofisha msuguano wa kitaifa," alisema.
Kwa wasomi, ushiriki dhaifu wa kisiasa – kutoka kwa wanaume na wanawake – nchini Cameroon pia inatokana na sababu za kisaikolojia na kihistoria.
"Kuwataka watu kushiriki katika siasa ni sawa na kuwahamasisha kugombea uongozi. Lakini hatuwezi kuhamasisha moyo wa uongozi wa mtu wakati tunakataa kuthamini uwezo wao. Inaanzia na familia ambapo uongozi wa watoto (wawe wavulana na wasichana) unapingwa. Wanafunzwa kuwa na hofu na wasiwasi. Huwezi kuchochea fursa za uongozi wa mtoto baada ya kutokuwathamini katika maisha yao yote. Wazazi wanapaswa kuanza kwa kubadili mahusiano na watoto," Songué alielezea.
Waziri wa ulinzi wa wanawake na familia anakubali kuwa kuna tatizo halisi. "Wanawake wana utamaduni duni. Na nyaraka ambazo zinaweka usawa wa jiinsi, kama vile katiba, hazijulikani vizuri sana," alisema Jean-Pierre Makanga, naibu mkurugenzi wa utetezi wa haki za familia katika wizara hiyo.
Hii imejitokeza pamoja na ukweli kuwa vyama vya siasa vinatetea usawa zaidi wa kijinsia. Moja ya vyama hivi ni Rassemblement démocratique du peuple camerounais (Chama cha Kongamano la Demokrasia Cameroon), ambacho ni chama kilichopo madarakani kwa sasa.
"Ni mara chache mno chama kinafuata sheria zilizowekwa na viongozi wake juu ya kuingiza wanawake na vijana katika orodha yake ya wagombea wakati wa uchaguzi wa ubunge na manisipaa," Makanga alibainisha, akielezea mtizamo ambao unaathiri ushiriki wa wanawake katika siasa.
Hata hivyo, uwakilishi wa wanawake katika maisha ya kisiasa nchini Cameroon umeboreshwa kidogo kidogo kutokana na utetezi wa jinsia na jitihada za serikali.
Akinukuu wizara ya utawala wa majimbo na madaraka mikoani, Makanga alibainisha kuwa mwaka 1982 kulikuwa na wanawake 336 katika halmashauri za manisipaa ikilinganishwa na leo hii ambao ni 1,651. Mafanikio pia yalirikodiwa katika bunge ambapo wanawake walichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1957. Bunge sasa lina wanawake wabunge 10 kati ya 180.
Lakini mafanikio bado hayatoshi, kwani kulingana na Makanga, tangu kuundwa kwake wanawake waliwakilisha asilimia 8.41 ya wale waliokuwa bungeni, ikilinganishwa na asilimia 11.16 ya viongozi wa kuchaguliwa katika halmashauri za manisipaa.
"Wanawake wanapaswa kushirikishwa katika vyama na makundi, na siyo tu kulipa ada zao, kula, kunywa na kusaidiana na wengine wakati wa matatizo," alisema Songué.
"Nitatumia kila mkutano kusambaza ujumbe: kura ya mwanamke ni suala la msingi katika kuchagua wawakilishi na hasa kuchagua wanawake wengine," Ngala Esther Ntale aliapa. Ntale ni mbunge na mwanachama wa chama cha Social Democratic Front, chama kikuu cha upinzani.
Uchagzui wa seneti umepangwa kufanyika mwaka huu nchini Cameroon tangu Rais Paul Biya alipotangaza kuundwa kwa useneti, wakati uchaguzi wa rais unaofuata unatarajiwa kufanyika mwaka 2011.
Kwa kutambua kuwa "uchaguzi unafanikiwa tu kama tunaweza kuhamasisha wadau wakuu asilimia 60 ya wapiga kura," mtandao wa "More Women in Politics" unapanga kuchukua hatua ya kuhamasisha asilimia 52 ya wanawake wa Cameroon ili sauti za wanawake zisikike zaidi, Diffo alisisitiza.
(END/2010)
|
|
|