AFRIKA KUSINI Jinsia Yapoteza Katika Mgogoro wa Elimu ya Msingi Na Ann Hellman
CAPE TOWN, Machi 11 (IPS) - Wakati tathmini ya miaka 15 ya Mkutano wa Dunia wa Beijing kuhusu Wanawake mwaka 1995 ikifanyika katika Tume ya Hali ya Wanawake mjini New York, walimu wa Afrika Kusini na wataalam wa elimu wanasema wanahofia kuwa lengo maalum la kuendeleza watoto wa kike linapotea katikati mwa kuongezeka kwa kiwango cha umaskini nchini.
Dhana yoyote kuwa mtaala unaozingatia jinsia, ambao unahakikisha usawa wa kijinsia kufundishwa inachukua nafasi ya nyuma ikilinganishwa na matatizo mengine ya kiuchumi na kijamii yanayoandama moja ya nchi zisizokuwa na usawa ulimwenguni.
Leo hii, miaka 15 baada ya kuanguka rasmi kwa serikali ya kibaguzi, serikali inakadiria inahitaji kwa uchache dola za Kimarekani bilioni 35 kujenga madarasa, kuweka huduma za maji, vyoo na umeme katika shule zote.
Hata kama kiasi hiki kimesambazwa katika kipindi cha zaidi ya miaka saba – na kuacha shule nyingi bila kuwa na huduma hizo hadi mwaka 2020 – bado serikali "haijawa na uwezo", maafisa wa serikali waliliambia bunge miezi 18 iliyopita.
Hali imezidi kuwa mbaya tangu wakati huo. Wiki sita zilizopita, afisa wa serikali anayehusika na shule za msingi na sekondari Bobby Soobrayan, aliliambia bunge la Afrika Kusini kuwa kwa sasa nchi inakabiliwa na "mgogoro katika shule za msingi".
Walimu Thandi Mapalakanye na Andre Marais wako mstari wa mbele katika mfumo wa elimu baada ya ubaguzi wa rangi.
Wakifundisha katika shule mbili kati ya maelfu ya zilizosahauliwa ambazo zilitengwa kwa ajili ya "watu weusi" na mfumo wa kibaguzi, Marais anasema, "naweza kukueleza kwa uhakika, usawa wa jinsia haufundishwi katika shule za maskini".
Marais amefundisha kwa miaka 15 sasa katika Shule ya Sekondari ya Rosendal huko Delft, jengo la zamani la Cape Town lililojengwa katika vilima vya mchanga kama kilomita 28 kutoka katikati mwa mji.
Shule ilivutia vyombo vya habari kwa sababu mbaya mwaka jana baada ya mkuu wake wa shule aliposhutumiwa na vyombo vya habari vya kigeni kutokana na kufukuza watoto wa kike wa shule mara tu walipoonekana wana mimba – na kutokana na kutokuwarushu kurejea tena mara baada ya kujifungua watoto.
"Nafundisha darasa la watoto 67. Watoto wanaketi sakafuni. Shule hii inahitaji walimu wengi mno lakini idara ya elimu inakataa kutupatia zaidi," Marais aliiambia IPS.
"Jinsia siyo suala zito kwa walimu wengi. Hakuna njia ya kushughulika na wasichana wadogo wanaopata mimba; kwa kweli hakuna uangalizi kabisa. Naweza kusema kwa usalama hali inafanana katika Delft nzima," alisema Marais.
Mapalakanye anafundisha wavulana na wasichana wenye umri wa miaka 16 hadi 18 katika shule ya sekondari ya watu weusi kihistoria karibu na Johannesburg.
Zaidi ya kilomita 1500 kutoka Delft, Mapalakanye anasema Shule ya Sekondari ya P.T. Xulu karibu na Johannesburg ina matatizo kama hayo kama ilivyokuwa kwa Shule ya Sekondari ya Rosendal.
Anaelezea kuwa katika shule yake ya wanafunzi 1200, kuna wanafunzi kati ya 90 na 110 katika kila darasa.
"Ni vigumu mno kwa wasichana lakini kutokana na matatizo mengine, hata sijaanza kufikiri masuala ya jinsia," Mapalakanye aliiambia IPS.
Mtafiti mwandamizi wa Kituo cha Haki ya Elimu na Mabadiliko cha Johannesburg, Salim Vally, anakadiria kuwa unyanyasaji wa kijinsia mashuleni umezidi tangu mwaka 2002 wakati utafiti wa karibuni ulionyesha kuwa asilimia 33 ya waathirika wa ubakaji Waafrika Kusini walikuwa wasichana ambao walibakwa na watu wa jumuiya za shule, wanafunzi wenzao au wafanyakazi wa shule.
Vally aliiambia IPS kuwa lengo la serikali la Maendeleo ya Milenia kuhusu jinsia halisaidii.
Malengo ya pili na tatu yanataka usawa wa jinsia katika shule za msingi na sekondari ifikapo mwaka 2015.
"Tuna usawa wa jinsia mashuleni; hakika kuna wasichana wengi zaidi katika shule za sekondari kuliko wavulana. Lakini takwimu za usawa wa jinsia zinafunika masuala mengine, kama vile jinsi tunavyohakikisha usawa wa usalama kwa elimu ya wasichana. Inachukua zaidi uwiano wa usawa kati ya wanaume na wasichana kutafutia ufumbuzi hali za ubaguzi wa kijinsia na unyanyasaji," alisema.
Kiasi kikubwa cha unyanyasaji dhidi ya wasichana kina uwezekano wa kuathiri usawa katika elimu yao.
"Mtaala rasmi unakamilika na maneno ya kupinga ngono. Ikilinganishwa na mtaala wakati wa ubaguzi wa rangi ni maendeleo makubwa," Vally anasema.
Lakini anaonya kuwa hata kama sera za "mtaala unaozingatia jinsia" za Afrika Kusini zinatekelezwa bado kuna wasiwasi zaidi na upinzani.
Anaongeza kuwa wasichana katika vitongoji vya maskini Afrika Kusini, au makazi duni, hawalingani na wenzao katika maeneo ya mijini. Kulingana na ripoti ya karibuni ya Utafiti wa Kaya, asilimia 16 ya watoto wa Afrika Kusini hawana mzazi mmoja au wote wawili. Wasichana kutoka makazi yasiyokuwa rasmi au maeneo ya vijijini, pale ambapo kiwango cha uhaba wa ajira ni cha juu hadi asilimia 60, wana uwezekano wa kuishia kutunza dada na kaka zao wenye umri mdogo.
"Kuna shinikizo kubwa kwa wasichana wanaokwenda shule kwasababu wanaonekana kama watoa huduma majumbani," Vally anaongeza.
Mgawanyiko wa kitabaka unaonyesha katika mahojiano na wanafunzi machotara ambao wanahudhuria shule zenye vifaa zaidi ambazo chini ya ubaguzi wa rangi, zilihifadhiwa kwa ajili ya wazungu tu.
Salmah Peters (17) yupo mwaka wake wa mwisho katika Shule ya Sekondari ya Hottenhots Holland huko Somerset West, kitongoji kilichopo umbali unaopata kilomita 40 kutoka Cape Town.
Anaonekana kutokuvutiwa na masuala ya jinsia kwa ujumla na anazungumzia uzoefu katika shule yake kuwa wasichana wanahamasishwa na walimu kujifunza masomo ambayo hapo awali yalikuwa yakichukuliwa na wanaume tu kama vile uhandisi.
"Katika miaka miwili ya awali ya sekondari wanatenganisha wasichana na wavulana katika madarasa tofauti kwasababu wanasema sisi wasichana tutafanya vizuri kuliko kama wavulana wangekuwepo kutubughudhi. Lakini katika miaka mitatu ya mwisho tunakuwa katika madarasa ya pamoja" Peters anasema.
"Hakuna unyanyasaji dhidi ya wasichana hapa, pamoja na kwamba mara nyingine tunapigana kwa ajili ya wavulana na mambo mengine madogo madogo," anaongeza.
"Maisha kwa tabaka la watoto wa kike kutoka watu weusi wanaofanya kazi nchini Afrika Kusini ni magumu zaidi. Inabidi mara kwa mara kukumbusha watu kuwa, zama baada ya ubaguzi wa rangi, wakati wa ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kijinsia na mgawanyo wa matabaka bado zipo katika jamii na katika mfumo wa elimu," Vally anahitimisha.
(END/2010)
|
|
|