ELIMU-TANZANIA Kulazimishwa Kuacha Shule Watoto Wenye Mimba Na Arnaud Bébien
DAR-ES-SALAAM, Machi 10 (IPS) - Mimba ni sababu kuu ya watoto wa kike kuacha shule nchini Tanzania. Na sheria inayozuia wazazi watoto kurejea tena shule baada ya kujifungua haijawarahisishia kuendelea na elimu yao.
Lakini pongezi kwa shinikizo la Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), serikali ya Tanzania sasa imepitisha sheria mpya kuruhusu wazazi watoto kuendelea na elimu yao.
Kabla ya kurekebishwa kwa sheria, baadhi ya watoto wa kike walijiunga na vyuo vya ufundi stadi ambavyo viliwawezesha kurejea tena shule.
Vituo hivyo vinapatikana katika nchi nzima na vinategemea wizara ya elimu. Mafunzo yanafadhiliwa kwa msaada wa familia: watoto wa kike wanajifunza ufundi kama vile ususi na ushonaji) au wanachukua mafunzo ya shule ya jioni.
Bethsheba, 18, anasoma katika Kituo cha Temeke, lakini anaishi na shangazi yake. Mama wa mtoto mdogo Thabit, alipata mimba na mtoto wa rafiki yake na jirani mwaka 2006.
"Aliniambia ananipenda. Kutokana na kwamba nilikuwa nikisubiri matokeo ya mtihani wa mwaka wa mwisho nilidhani ni wakati mzuri kuwa na mahusiano," aliiambia IPS. Kwa sasa, Bethsheba anasoma masomo ya kujifua katika kituo hicho, na anatarajia kuweza kurejea sekondari hivi karibuni.
Hata hivyo, pamoja na nia njema, kurejea shule ni kugumu, hasa bila ya kupata msaada wa familia.
Catherine, 16, alipata mimba akiwa katika madarasa ya juu. "Nilikuwa katika mwaka wangu wa 3 nilipolazimishwa kuacha shule kutokana na kuwa na mimba," anakumbuka. "Nataka kwenda shule ya ufundi, lakini ni vigumu kwasababu sina mtu wa kumwangalia mtoto wangu wa kike nyumbani."
Mimba za utotoni siyo tatizo jipya nchini Tanzania na limesababisha mjadala wa kitaifa.
Katika kikao cha Bunge la Feb. 10, mbunge kutoka chama cha upinzani cha 'Civic United Front', alimkosoa naibu waziri wa elimu, Mwantumu Mahiza, kutaka aelezee hatua zilizochukuiwa na serikali kupunguza idadi ya wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni.
Mahiza alisema kuwa wizara yake inaandaa sheria na sera mpya kushughulikia suala hilo, akiongeza kuwa asilimia sita ya wasichana wanaacha shule kila mwaka kutokana na mimba. Asilimia ishirini na tano ya wanawake nchini Tanzania chini ya miaka 18 tayari wana watoto.
Kulingana na takwimu za wizara ya elimu, watoto wa kike 28,600 waliacha shule kati ya mwaka 2004 na 2008 kutokana na kupata mimba. Katika ngazi ya shule ya sekondari takwimu zinashangaza: mwaka 2007 mtoto wa kike mmoja katika kila watano alipata mimba na hakumaliza shule.
Moja ya sababu kubwa za idadi kubwa ya wasichana kupata mimba ni kwamba wengi wanafanya ngono isiyokuwa salama na hawapati huduma za njia za uzazi wa mpango. Vile vile, kuna suala la kijamii. Kwa mfano, katika mkoa wa Shinyanga (magharibi mwa Tanzania), wazazi huwatishia kuwafukuza mabinti zao nyumbani kama wanaingia sekondari.
Wengi wanawaomba mabinti zao kutofaulu masomo yao ili waweze kuolewa mapema iwezekanavyo. Katika baadhi ya maeneo ya vijijini nchini, watoto wa hadi umri wa miaka 11 wanapata mimba. Wengine wanalaumu Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, ambayo imeweka umri wa kuolewa kwa msichana kuwa miaka 14. Kwa baadhi ya wazazi mahari wanazopokea wanapoolewa watoto wao wa kike inakua chanzo cha kipato.
Vile vile, kati ya wakazi hawa ambao asilimia 80 wanaishi vijijini, wazazi wenye kipato cha chini mara nyingi hawana kipato cha kuwapeleka watoto wao shule za sekondari. Wanapomaliza shule ya msingi wakiwa na umri wa miaka 13 au 14, wasichana wanabaki nyumbani katika kijiji chao na kupata mimba.
"Idadi kubwa ya wazazi hachukulii kwa uzito mkubwa suala la kuwapeleka watoto wao shule," inasema wizara ya elimu.
Hata hivyo, suala hilo linachukuliwa kwa uzito mkubwa na watendaji wa serikali kwani wengi wa watoto hawa wanakabiliwa na changamoto ambazo hawajajiandaa kukabiliana nazo. Mwimbaji wa Benin ambaye ni balozi wa UNICEF, Angélique Kidjo, alizuru Tanzania mwezi Januari kuhamasisha juu ya suala hilo.
"Inanikasirisha kuona watoto wa kike hawa kwasababu kuwa mama na umri wa miaka 16 siyo jambo rahisi," alisema mjini Dar es Salaam alipokutana na wazazi watoto.
Kutokana na shinikizo la UNICEF serikali ya Tanzania ilipitisha sheria mpya Januari 2010 ambayo inaruhusu wazazi wenye umri mdogo kurejea tena shule. Hii ilikuwa haiwezekani kabisa kabla ya hapo. Lakini sasa UNICEF inatambua kuwa siyo kila kitu kimewezekana, baadhi ya shule bado haziwezi kupokea wasichana wanaorejea shule baada ya kujifungua kwani hazijui sheria hiyo mpya.
Mbali ya hatari ya kuambukiza VVU wakati wa kufanya ngono, wasichana hawa wenye umri mdogo pia wanakabiliwa na matatizo wakati wa kujifungua. Nchini Tanzania, robo tatu ya wazazi hujifungulia nyumbani ambako hakuna huduma za kutosha na tiba.
Angelina, 16, alikuwa na mimba wakati alipoacha shule akiwa shule ya sekondari mjini Dar es Salaam. Mtoto wake alizaliwa akiwa hajatimiza siku na kuwa na tatizo la moyo. Alikaa miezi minne hospitalini, lakini sasa anasoma katika chuo cha ufundi stadi kinachofanana na cha Temeke. Hadithi yake mara chache ina matokeo chanya katika nchi ambayo wazazi watoto kama ilivyo yeye hawana bahati.
Kwa baba mtoto, ambaye ni dereva wa basi, aliweza kukimbia bila kutafutwa. Kutelekeza watoto ni tabia inayojitokeza mara nyingi kwa wasichana hawa wenye watoto na umri mdogo. Wengine ni wadogo mno kuwa wazazi na wanatelekezwa na baba watoto wao huku wakiwa hawana njia ya kuwasaidia.
Mara nyingine wazazi wanasaidia mabinti wanapoweza, lakini baadhi hawasiti kuwafukuza nyumbani. Matokeo yake: wasichana wengi wa umri mdogo wenye watoto wadogo wanauza matunda na mbogamboga kandokando mwa barabara, kwa ajili ya kujisaidia wenyewe.
(END/2010)
|
|
|