TANZANIA MABADILIKO YA Hali ya Hewa Yawafanya Wakulima Kucheza Kamali na Asili Na Denis Gathanju
DAR-ES-SALAAM, Machi 10 (IPS) - Mabadiiko ya mwelekeo wa hali ya hewa yamefanya kilimo kuwa kamali kwa wakulima wa Tanzania. Ukame wa muda mrefu na mafuriko yamefanya maisha ya wakulima wadogo, ambao hawana huduma za umwagiliaji, kuwa magumu zaidi.
Nchini Tanzania, ambako uchumi unategemea zaidi kilimo, wakazi wa vijijini ambao ndiyo maskini wameathirika zaidi.
Kulingana na Wizara ya Kilimo (MoA), kilimo kinachangia asilimia 60 ya Pato la Taifa (GDP). Zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wanafanya kazi katika sekta ya kilimo, ambayo inachangia asilimia 60 ya mauzo ya nje kutoka nchini humo.
Ripoti ya mwaka 2009 ya Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) inaonya kuwa Tanzania ina miongo miwili ya kukifanya kilimo kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ama sivyo itakuwa katika hatari ya kushuka kwa GDP. Kupungua kwa GDP kutakuwa asilimia moja katika miaka 20 ya mwanzo na kupungua zaidi hadi asilimia kati ya 5 na 65 katika kipindi cha miaka 75 mingine, anasema Muyeye Chambwera, ambaye ni mwandishi mwenza wa ripoti.
Wataalam wa mabadiliko ya tabia nchi wanakubaliana kuwa njia pekee ya kuzuia madhara makuwba ya uchumi ni kubadili jinsi kilimo kinavyoendeshwa.
"Njia pekee ni kuelimisha wakulima kutumia mbinu bora za kilimo, kwanai wengi bado wanatumia njia zilizopitwa na wakati, wakati wengine wanaendesha kilimo katika maeneo ambayo mvua hazitoshelezi," alisema Marc Baker, mkurugenzi mtendaji mkuu wa Carbon Tanzania, asasi isiyokuwa ya kiserikali ambayo inasaidia wakulima katika kijiji cha Arkaria, kilomita 35 magharibi mwa Arusha, kujifunza kuishi na mabadiliko ya tabia nchi.
Serikali ya Tanzania imegundua kuwa inahitaji kuchukua hatua ya haraka na ilianzisha Mpango wa Taifa wa Kutekeleza Kuishi na Mabadiliko ya Tabia Nchi (NAPA) ambao unataka kupunguza uzalishaji wa gesi chafu za viwandani na kusaidia wakulima kukubali mbinu mya za kilimo na teknolojia.
Inapanga kuelimisha wakulima juu ya njia mbadala za kilimo, kama vile kupanda mazao kwa mzunguko, kufuga mifugo ndani na kuandaa mazao ambayo yanahitaji maji machache, kama vile mtama na uwele. NAPA pia inahamasisha upandaji wa mahindi yanayostahimili ukame.
"Lengo la NAPA ni kukuza uwezo wa kuishi na mabadiliko hasa kwa jumuiya dhaifu zaidi, kutokana na kwamba uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea katika kilimo …," alithibitisha Abubakar Rajabu, katibu mkuu Ofisi ya Makumu wa Rais.
Katika nchi nzima joto lina uwezekano wa kuongezeka kati ya nyuzijoto mbili hadi nne ifikapo mwaka 2100, inatabiri MoA. Huu unaonekana kuwa muda mrefu, lakini inaonyesha kuwa mimea ya msimu kama vile mahindi na maharage, hayataweza tena kukua na inabidi nafasi yake ichukuliwe na mtama na uwele.
Uzalishaji wa mahindi, zao kuu la chakula nchini Tanzania, unatarajiwa kushuka kwa theluthi moja katika miongo michache ijayo, kwasababu zao hilo linahitaji maji mengi mno, maofisa wa MoA wanaonya. Katika maeneo ya kati ambayo ni makavu zaidi, mavuno ya mahindi yanaweza kupungua kwa asilimia 84.
Msimu wa kupanda wa mwaka jana ni mfano mzuri kuwa utabiri unatimia, pengine mapema zaidi ya inavyotarajiwa. Wakulima katika mkoa wa Iringa waliwaambia maofisa wa MoA kuwa walivuna kati ya magunia matatu hadi matano ya mahindi katika ekari moja ya ardhi mwaka 2009. Haya ni machache mno ikilinganishwa na wastani wa magunia 15 hadi 18 ya mavuno miaka michache iliyopita.
Wakulima pia wameshuhudia madhara ya mabadiliko ya mwelekeo wa mvua. "Mahindi hayafanyi tena vizuri," anasema Mama Mrema, mkulima mdogo kutoka Arusha. "Sasa nimegeukia kupanda mazao mengine kama vile mihogo na viazi vitamu, ambayo hayahitaji mvua nyingi, ili niweze kuishi."
Katika kijiji kingine cha Mwitikilwa katika mkoa wa Iringa, wanakijiji wanasema kumekuwa na mabadiliko ya kasi katika mwelekeo wa hali ya hewa wakati wa miaka thelathini iliyopita.
Dk. Emma Liwenga, mtafiti katika Taasisi ya Kutathmini Rasilimali katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ambaye alifanya utafiti kijijini humo mwaka jana, anathibitisha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamezuia wakulima wa Mwitikilwa kupanda maharage, kahawa, dengu na viazi vitamu. Utafiti wake pia ulionyesha kuongezeka kwa wadudu waharibifu kutokana na kuongezeka kwa joto.
Wakulima wamejitahidi kujiweka kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa. "Muongo uliopita umekuwa mbaya mno katika uzalishaji wa chakula, hasa katika kijiji chetu ambapo hatujatumia mbolea za kemikali kupanda mazao yetu. Tumekuwa tukirikodi mavuno machache, kwasababu ya ukame kuwa mrefu na mkali zaidi wakati mvua zikiwa haziaminiki," anasema mkulima Maimuna Hamadi.
Mvua fupi ambazo zinanyesha kati ya Aprili na Julai zimekuwa hazina uhakika, wakati joto kati ya Aprili na Agosti limeongezeka kupita kiasi, wanasema wakulima.
"Hatuna uhakika tena ni lini tunapaswa kuandaa mashamba kwa ajili ya kupanda au lini tunaanza kupanda. Ni kama kucheza kamali na asili. Hali ya hewa haitabiriki tena ikilinganishwa na baadhi ya miaka 10 au 15 iliyopita," analaumu Mwanaisha Mwampamba, mkulima mwingine kutoka Mwitikilwa.
"Mara nyingine mvua hazitoshi kwa uzalishaji wa mazao, wakati mwingine, zinakuwa nyingi kupitiliza. Zinasababisha mafuriko na kuharibu mazao," anaongeza. "Kama hali hiyo ikiongezeka, wengi wetu, ambao tuna mashamba madogo, tutatumbukia zaidi katika umaskini, kutokana na kutegemea kilimo kutunza familia zetu."
(END/2010)
|
|
|