HAKI Habari ya Mafanikio ya Afrika Katika Uwezeshwaji wa Kijinsia Na Thalif Deen*
UMOJA WA MATAIFA, Machi 10 (IPS) - Kila wakati suala la uwezeshwaji wa kijinsia linapochukua nafasi ya juu katika mjadala wa kimataifa, baadhi ya nchi za Ulaya, Asia na Amerika Kusini zinatoa sifa kubwa kutokana na mafanikio katika siasa, elimu, huduma za afya au uhuru wa mashirika ya kiraia hata kama Afrika imeachwa nyuma zaidi katika rikodi za kisiasa.
Rwanda imeongoza kimataifa katika suala la kuwa na wanawake wengi zaidi katika nafasi za kuchaguliwa, huku zaidi ya nusu ya wabunge wakiwa wanawake, anasema Litha Musyimi-Ogana, mkurugenzi wa kurugenzi ya wanawake, jinsia na maendeleo katika Umoja wa Afrika (AU) wenye wanachama 53, umoja mkubwa zaidi wa mataifa ya Afrika.
Cape Verde, taifa jingine la Afrika lina mafanikio makubwa, lina "kiasi kikubwa zaidi cha mawaziri wanawake duniani:" wakati wa hesabu ya mwisho, wanafikia 12 kati ya 17.
Lakini bado, Musyimi-Ogana anasema, AU inatambua kuwa pamoja na asilimia 70 ya nchi wanachama wake kuwa na sera za jinsia, kuna "changamoto nyingi za utetekelezaji".
Sababu ni kwa nini sera hizi hazitekelezwi ni kutokana na kukosekana kwa rasilimali fedha.
Matokeo yake, AU imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika kukabiliana na "vikwazo katika rasilimali".
Wakati huo huo, imeshaanzisha itifaki – waraka wa 'Haki za Wanawake' ulioridhiwa na nchi 27 – katika Mkataba wa Haki za Binadamu Afrika.
Lalla Ben Barka, naibu katibu mtendaji mkuu wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa Afrika (ECA), anadai kuwa Afrika imepata "mafanikio ya kujivunia" katika kuziba pengo la jinsia katika elimu ya msingi, hasa kutokana na "kuwa na elimu ya bure, na ya lazima" – katika bara zima.
Aliiambia Tume ya Hali ya Wanawake (CSW), ambayo inamaliza vikao vyake viwili Ijumaa, kuwa asilimia 65 ya nchi katika kanda zilikuwa zikifanya utafiti kuhusu hali ya wasichana, na baadhi ya nchi zimerekebisha mtaala wa shule kuonyesha sura nzuri ya wanawake.
Hata hivyo, bado kuna mapengo katika maeneo kadhaa: haki ya urithi kwa wanawake, elimu ya juu na kutokomeza tamaduni mbaya na zenye vikwazo katika maendeleo ya wanawake.
Alisema Liberia ilipata mafanikio makubwa kwa kuchagua rais wa kwanza mwanamke katika bara la Afrika, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye aliingia madarakani Januari 2006.
Ben Barka pia alisema kuwa asilimia 47 ya nchi zina sheria za kutokomeza tohara kwa wanawake (FGM), na nyingi zimetoa huduma kubwa kwa waathirika.
Kulingana na Tsegga Gaim Misgun wa Umoja wa Kitaifa wa Wanawake wa Eritrea, jitihada za kutokomeza FGM zilianza nyuma mwishoni mwa miaka ya 1970 – hata kabla ya uhuru rasmi wa Eritrea mwaka 1993 – na serikali ya waasi wa Eritrean People's Liberation Front.
Kutokana na jitihada hizi, watu wa Eritrea walikuwa wameanzisha sheria za jumuiya kupiga marufuku FGM. Katika mipango hii, serikali ya Eritrea ilipiga marufuku tohara Machi 2007.
"Sheria zilifanya tohara kwa wanawake kuwa kosa la jinai," Misgun alisema.
Noluthando Mayende-Sibiya, waziri wa wanawake, watoto na watu wenye ulemavu wa Afrika Kusini, aliwaambia wajumbe kuwa pamoja na kwamba unyanyasaji dhidi ya wanawake unabakia kuwa "wasiwasi mkubwa wa serikali", nchi yake iko katika hatua ya juu ya kuandaa mpango makini wa kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia.
Mipango hii ni pamoja na sheria katika makosa ya kujamiiana; usafirishaji wa binadamu; unyanyasaji majumbani; na sheria ya watoto.
Kituo cha kutunza watoto cha "Thuthuzela Care Centre", kilielezewa kama kituo kinachofanya kazi kubwa kwa waathirika wa unyanyasaji wa majumbani, na kupongezwa kama mfano "bora" katika ripoti ya mwaka 2007 ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuhusu unyanyasaji wa watoto.
"Kazi hizi zinaigwa na nchi nyingine katika ngazi ya kimataifa," alisema.
Mayende-Sibiya pia alisema kuwa Afrika Kusini inajivunia kwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaopelekwa katika kulinda amani, ambao ni sawa na wastani wa asilimia 40 ya walinzi wa amani kutoka nchini humo.
Alphonsine Mbie N'na, waziri wa afya na masuala ya jamii wa Gabon, alisema nchi yake imeunda mkakati wa kupunguza umaskini ikiwa ni pamoja na mtihani wa kutangaza shughuli za kijamii na kiuchumi miongoni mwa wanawake, huku washindi wakipata dola 40,000 na safari za nje.
Katika nyanja ya ajira, Gabon haina ubaguzi wa kuajiri wala mshahara. Shule na vitabu ni bure.
Nchini Ethiopia, waziri wa masuala ya wanawake ni sehemu ya nguzo ya utendaji ya serikali.
Na ili kukuza usawa wa kijinsia katika kilimo – sekta kuu ya kiuchumi nchini humo - Ethiopia inasajili majina ya wanandoa kwa ajili ya kupata vyeti vya ardhi ili kuhakikisha kuwa wanawake wanaweza kumiliki njia za kiuchumi.
(END/2010)
|
|
|