MALAWI Mfumo Dume katika Urithi Unazuia Wanawake Kumiliki Ardhi Na Claire Ngozo
LILONGWE, Machi 9 (IPS) - Mercy Gondwe, 51, kutoka Rumphi kaskazini mwa Malawi, alikuwa katika ndoa kwa miaka 34. Wakati mume wake alipofariki mwaka 2008, alifikiri angerithi ardhi ambayo walikuwa wakilima pamoja tangu walipooana. Lakini haikuwa hivyo.
Shemeji wa Gondwe alichukua umiliki wa ardhi siku ya mazishi, kwasababu mila inataka mwanaume pekee kuwa na haki ya kumiliki ardhi. Gondwe na watoto wake sita, wenye umri kati ya miaka nane na 20, hawana cha kuchagua lakini kuishi na shemeji. Masharti ya mahari ambayo mume wa Gondwe ametoa alipooa yanasema kuwa mwanamke na watoto wake ni mali ya mume na famili yake.
"Watoto wangu na mimi bado tunaendelea kupanda mazao katika ardhi, ikiwa ni pamoja na tumbaku, lakini shemeji ananipangia cha kufanya na mazao yangu," Gondwe anasema.
Tumbaku ni zao kuu la kibiashara la Malawi. Kulingana na Gondwe, yeye na mume wake wamekuwa wakulima tumbaku tangu walipooana. Kwa miaka, mapato ya tumbaku yalisaidia kujenga nyumba ya tofali za kuchoma iliyoezekwa kwa bati, walifuga ng’ombe 22 na kuwafanya watoto wao wote kubakia shuleni.
Mwanamke anasema familia yake ilikuwa ikionekana yenye uwezo, ikilinganishwa na asilimia 65.7 ya wakazi wengine wa Malawi wapatao milioni 13.1 ambao, kulingana na serikali ya nchi hiyo, wanaishi chini ya mstari wa umaskini chini ya dola moja kwa siku.
"Lakini sasa mali zetu zote zipo chini ya familia ya mume wangu. Sina hisa yoyote kabisa. Shemeji yangu hupeleka tumbaku sokoni, na hunipatia kiasi kidogo tu cha fedha anaporejea," Gondwe aliiambia IPS.
Wanawake wanaoishi katika jumuiya za mfumo dume kaskazini mwa nchi wanaweza tu kumiliki ardhi ya kimila kupitia waume zao na shemeji zao, anathibitisha Maggie Kathewera-Banda, mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Women’s Legal Resources Centre (WOLREC).
"Kunyimwa kwa umiliki wa ardhi, mila kaskazini mwa Malawi zinanyima nafasi yao halisi ya maendeleo ya nchi," alielezea.
Kathewera-Banda anabainisha kuwa ardhi ni chanzo kikuu cha kipato cha kuendeshea maisha na usalama wa chakula nchini, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo umiliki wa kimila na jumuiya unatumika.
Wanawake ni zaidi ya nusu ya wakazi wote nchini Malawi, na asilimia 85 ya wao wanategemea kilimo cha kujikimu. Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kilimo ni mchangiaji mkuu wa uchumi wa Malawi – kinachangia asilimia 38 ya Pato la Ndani la Taifa (GDP) na asilimia 80 ya mapato yanayotokana na kuuza bidhaa nje. Sekta hiyo pia inatoa ajira kwa asilimia 85 ya wakazi.
Hata hivyo, karibu asilimia 75 ya ardhi nchini Malawi ni ya kimila, kulingana na Ripoti ya Takwimu ya Taifa mwaka 2004, ambayo kwa kiasi kikubwa inawaweka wanawake katika nafasi isiyokuwa na faida katika umiliki.
Wizara ya Ardhi nchini humo katika ripoti yake ya mwaka 2009 imesema kuwa sera mpya ya Ardhi ya Taifa nchini Malawi inaonyesha nia ya serikali kushughulikia suala hilo, kwasababu ina vikwazo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Malawi. Sera ilipitishwa na baraza la mawaziri na bunge mwaka 2002 na Tume ya Sheria Maalum ilianzishwa mwaka 2003 kupitia sheria zote zinazohusiana na ardhi. Sheria ya Marekebisho ya Ardhi sasa inabidi kupitishwa bungeni.
Sera ina lengo la kusahihisha na kuimarisha haki za ardhi za kijadi, miongoni mwa mambo mengine, na ina nia ya kuwezesha haki ya ardhi kwa Wamalawi wengi wanaoishi katika ardhi ambayo hapo awali ilikuwa inamilikiwa kimila. Itaruhusu ardhi yote ya kimila kusajiliwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria ili isitumike vibaya.
Katika sera ya ardhi, wamiliki wote wa ardhi ya kimila, ikiwa ni pamoja na familia, watahamasishwa kusajili ardhi zao kama mashamba binafsi ya kijadi na kuwa na haki ya kumiliki ardhi. Sera inasema kuwa italinda faida za umiliki wa ardhi ya kimila, lakini pia kuhakikisha usalama wa kumiliki.
"Inatarajiwa kuwa, kupitia sera ya ardhi, wanawake katika jumuiya za mfumo dume watawezeshwa na watasajiliwa kumiliki ardhi kwa jina la familia. Familia inapaswa kuwa ndogo, ambayo ni mume, mke na watoto wao," alielezea Kathewera-Banda.
Anasema hii itahakikisha wanawake wanamiliki ardhi pamoja na sheria za kimila na za nchi, ambazo kwa kiasi kikubwa zinabagua na kuzuia haki ya wanawake kuwa na ardhi. Sehemu ya 20 na 24 ya katiba ya Malawi inawapatia wanawake haki ya kumiliki ardhi na haki ya kutokubaguliwa kwa misingi ya jinsia au kuolewa au kutokuolewa, ikiwa ni pamoja na haki ya kuwa na kuendelea kuwa na ardhi binafsi au kwa kushirikiana na wengine, bila kujali ameolewa au hajaolewa, Kathewera-Banda alielezea zaidi.
Wanozga Nyasulu, 43, kutoka Mzimba kaskazini mwa Malawi yupo katika hali kama ya Gondwe – lakini mume wa Nyasulu bado yupo hai. "Anatoa uamuzi wa kipekee juu ya ardhi. Kutokana na mila zinavyotaka, natarajiwa kusaidia kulima tu ardhi," alilalamika.
Nyasulu anasema mume wake anatoa maamuzi ni lini waanze kufanyia kazi shamba, ni zao gani la kupanda, ni nini cha kula na nini cha kuuza: "Ni mila, na hakuna anayeweza kupinga. Unaweza kuonekana mjinga kama ukiipinga."
Aliieleza IPS kuwa anasubiri kwa hamu kuanza kufanya kazi kwa sera ya ardhi, wakati mfumo dume katika urithi wa ardhi utakapokoma.
(END/2010)
|
|
|