MAZINGIRA-UGANDA Maporomoko ya Udongo-Wataalam Waonya Bado Hali Mbaya Haijawadia Na Joshua Kyalimpa
KAMPALA, Machi 9 (IPS) - Isaac Wadyegere mwenye umri wa miaka kumi na nne kutoka kijiji cha Bundesi katika wilaya ya Bududa aliamka na mvua na baridi ya asubuhi Jumatatu na kwenda shule kama kawaida. Lakini Machi 1 haikuwa siku ya kawaida kwa mashariki mwa Uganda.
Aliposikia sauti za miamba na udongo ukipoporomoka kutoka Mlima Elgon kuelekea kuangamiza sehemu ya shule yao, Wadyegere, pamoja na wanafunzi wengine walikimbilia nyumbani.
Lakini badala ya kupata hifadhi ambayo aliitarajia, janga lilimsubiri Wadyegere.
Nyumba na familia yao iliangamizwa.
"Baba, mama, mama wa kambo, na ndugu zangu watano walifariki wote katika nyumba yetu iliyofukiwa na maporomoko ya udongo," anasema mvulana huyo.
Wadyegere ambaye sasa ni yatima anaishi katika kambi iliyoanzishwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda kwa ajili ya wahanga wa maporomoko ya udongo ambayo yalizika vijiji vingine vitatu; Nametsi, Namakansa na Kubewo katika wilaya ya Bududa.
Hadi sasa miili 92 imeshapatikana katika kifusi kazi iliyofanywa na jeshi na wafanyakazi wa uokozi na zaidi ya watu 300 bado hawajapatikana. Zaidi ya watu 300,000 watahamishwa kutokana na janga hilo baya zaidi katika kanda kulingana na Joel Aguma, kamanda wa polisi wa mashariki mwa Uganda. "Hatujajipanga kwa jambo hili na hapa tumefika, kutokana na kuwepo kwa watu wengi wa kutafuta, kiwango cha janga hili kwa kweli kinazidi uwezo wetu lakini tunajaribu kadri tunavyoweza," Aguma alisema wakati uokozi ukiendelea.
Sasa serikali imetangaza eneo la maporomoko ya Bududa kuwa makaburi ya wengi.
Waziri wa nchi anayeshughulikia kujiandaa na majanga, Musa Ecweru, anasema serikali imesitisha kutafuta miili ya waliofukiwa baada ya ugonjwa wa kuhara damu kuibuka na waokozi kuupata. "Tumegundua itachukua muda mrefu kupata miili yote na hatari inazidi kuongezeka kwa waokozi," Ecweru anasema.
Watalaam wanaonya kuwa hali mbaya bado haijatokea. Ripoti ya mwelekeo wa hali ya hewa iliyotolewa hivi karibuni na Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa na Kuishi na Mabadiliko (ICPAC) ya Mamlaka ya Maendeleo ya Serikali za Mashariki mwa Afrika (IGAD) mjini Nairobi, ilisema kuwa kanda inatarajiwa kuwa na mvua zaidi ya kawaida.
Taarifa hiyo ilitolewa wakati wa Jukwaa la Tathmini ya Hali ya Hewa la Pembe Kuu ya Afrika lililofanyika mjini Nairobi, Kenya mwezi Februari. Wanasayansi wa hali ya hewa wa kitaifa, kikanda na kimataifa walitathmini hali ya mfumo wa hali ya hewa wa kimataifa na maana yake katika mvua za msimu katika kanda nzima.
Wataalam walisema mifumo ya kikanda ambayo ni pamoja na joto la baharini katika bahari ya hindi, ambayo kwa sasa ina joto linalozidi wastani, na Bahari ya Atlantic vitakuwa ni sababu kubwa ya kunyesha mvua nchini Uganda
Profesa Laban Ogalo, mkurugenzi wa ICPAC anashauri nchi katika kanda kujipanga kadri inavyowezekana kwani mabadiliko ya mwelekeo wa mvua yanaweza kuwa baraka na laana.
"Mvua ni kitu kizuri kama kikisimamiwa vizuri. Kanda inaweza kufaidika kutokana na mvua kama inatumiwa kuongeza uzalishaji wa chakula kwa wale wanaoipata kwa wingi ili waweze kulisha wengine wanaopata mvua duni," anasema Ogalo. Alisema mvua kubwa katika kanda zinaweza kuharibu miundombinu na zinaweza kupoteza maisha.
Wataalam wa hali ya hewa wa Uganda wanaonya kuwa maporomoko ya ardhi zaidi na mafuriko katika mashariki, katikati na maeneo ya magharibi mwa nchi yanaweza kujitokeza kutokana na kuendelea kwa mvua kubwa nchini. Mto Malaba katika wilaya ya Busia mashariki mwa Uganda, karibu na wilaya ya Bududa, tayari umeshavunjika kingo zake.
Bildard Baguma, naibu katibu mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda, anasema kuna uwezekano mkubwa wa mafuriko kutoka mto huo kama mvua zitaendelea. Baguma anasema watu katika maeneo yaliyoathirika watahamishwa kutoka katika vijiji vyao na kupelekwa maeneo ya juu ambako kambi za muda zitawekwa.
Serikali ya Uganda imewataka wakazi katika maeneo ya mabondeni na yenye mafuriko kuhama kabla ya janga kutokea. Wizira ya kujiandaa na majanga tayari imeshaandikisha watu waliopo katika maeneo hatari kwa ajili ya kuhama. Zaidi ya watu 300,000 walioathirika katika ukanda wa Mlima Elgon na maeneo ya mabondeni ya jirani ya Butaleja, Budaka na Tororo wanatarajiwa kuhamishwa.
Deus Bamanya, mtaalam wa hali ya hewa mwandamizi katika idara ya hali ya hewa, anaelezea kuwa hali hiyo mbaya ya hewa kusini mwa Ulaya ilidhoofisha mfumo wa mgandamizo mkubwa kaskazini mwa Afrika, ambao uliweza kusukuma ukanda wa mvua kwenda Uganda. Mvua kubwa ambazo zingeweza kusababisha mafuriko zinatarajiwa kuendelea hadi Juni.
Waziri Mkuu Apollo Nsibambi ameliambia bunge serikali inaomba wafadhili kutoa fedha kusaidia katika zoezi la uhamishaji kabla mvua zaidi hazijaja na kufanya uharibifu.
Kutokana na nchi kuwa katika maombolezo ya vifo vya wale waliofariki katika wilaya ya Bududa, maporomoko ya udongo yamewafanya mamia magharibi mwa Uganda kuhamishwa. Mvua kubwa zilisababisha maporomoko ya udongo Machi 4. Maafisa kutoka wizara ya maandalizi ya majanga wamekimbilia Kabale, ambayo inapakana na Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kutathmini kiwango cha uharibifu.
Mamlaka ya wilaya yanasema maporomoko ya udongo yalikumba kata ndogo za Rubaya na Butanda na kuharibu nyumba na kufunga barabara pekee inayoingia maeneo hayo. Wafanyakazi wa uokozi walitumia siku nzima kusafisha barabara kabla hawajafika katika eneo hilo.
Watu watatu wamethibitishwa kufa baada ya kubebwa na maji yaliyokuwa yakisafiri kwa kasi katika daraja la Kigarama katika wilaya ya Kabale. Askari wameungana na mamlaka ya wilaya ya Kabale katika kupata usahihi wa taarifa kuwa watu bado wamefunikwa udongo na matope katika nyumba zao.
Mark Choono, mratibu wa dharula wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa nchini Uganda, anaonya kuwa kufumuka kwa magonjwa pia kuna uwezekano mkubwa kujitokeza.
"Tunajikita zaidi katika kusamba maji salama ya kunywa, ambalo ni tatizo kubwa zaidi katika maeneo yaliyoathirika na maporomoko ya udongo na mafuriko. Tumeshaanza kusambaza dawa za kusafisha maji kwa watu walioathirika," anasema Choono.
Tayari katika Bududa watu 60 wamekumbwa na kipindupindu.
Lakini wakati uharibifu unaendelea baadhi ya wataalam wanasema kuwa uharibifu wa uoto wa asili katika milima unaofanywa na walowezi, ambao wamesafisha maeneo kwa ajili ya kulima mazao, yamefanya ardhi kukosa nguvu, na hivyo kusababisha maporomoko ya udongo.
Dk. Festus Bagoora, mtaalam wa hali ya hewa na ardhi katika Idara ya Jiografia ya Chuo Kikuu cha Makerere, anasema shughuli za binadamu za zamani zimechangia janga hilo.
"Sababu mbalimbali zinasababisha hili, miamba inadhoofishwa kutokana na hali ya hewa lakini watu wameharibu uoto wote wa asili milimani kwa ajili ya kilimo na kutokana na mvua kubwa maporomoko yana uwezekano mkubwa kutokea," anasema Bagoora.
Aliiambia IPS kuwa yeye na wataalam wengine waliwasilisha utafiti wa mazingira kwa Mamlaka ya Usimamiaji wa Mazingira ya Taifa wakionya maeneo ambayo maporomoko ya udongo yanaweza kujitokeza lakini hakuna hatua imechukuliwa.
Anasema walipendekeza kuhamishwa kwa watu katika maeneo waliyohisi kuwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na mafuriko na maporomoko ya udongo.
(END/2010)
|
|
|