DR-KONGO EU Tatakiwa Kupiga Marufuku 'Madini kutoka Kwenye Vita' Ida Karlsson
STOCKHOLM, Machi 4 (IPS) - Baada ya hatua ya seneti ya Marekani kutaka kuzuiliwa kwa fedha za madini zinachochochea vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), shirika la kutetea haki za binadamu la Global Witness (GW) linaitaka Ulaya kufuata nyayo.
"Tunautaka Umoja wa Ulaya (EU) kuanzisha sheria ya kuzuia madini kutoka maeneo ya vita mashariki mwa DRC kuingia katika soko la Ulaya," Lizzie Parsons kutoka GW, shirika la kimataifa linalochunguza uhusiano kati ya uchimbaji wa maliasili na ukiukwaji wa haki za binadamu, aliiambia IPS.
Kulingana na GW, vikundi vyenye silaha vinadhibiti biashara ya madini mashariki mwa DRC. Vikundi hivi vyenye silaha vinapata faida kutokana na biashara ya mamilioni ya dola kutokana na madini na kudhibiti migodi kwa nguvu na kuomba hongo au kodi. Wale wanaonunua "madini kutoka maeneo ya vita" ni pamoja na makampuni yaliyopo katika nchi wanachama wa EU.
Mchango wa biashara ya madini umetambulika kuwa moja ya sababu zinazochochea vita na kuchangia ukiukwaji wa haki za binadamu mashariki mwa DRC tangu kuanza kwa vita.
Wanaharakati wa haki za binadamu kwa muda mrefu wametoa wito wa jinsi gani "madini kutoka maeneo yenye vita" yanauzwa kununulia silaha kwa ajili ya vikundi vya waasi ambavyo mara kwa mara vinafanya mauaji mabaya dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji ya watu wengi, ubakaji, utesaji na ajira za kulazimishwa.
Katika kipindi cha miezi michache iliyopoita, GW ilikusanya taarifa katika kanda na kutembelea migodi ambayo iko chini ya udhibiti wa vikundi vya waasi.
Parsons anasema vikundi vya waasi wenye silaha vingekuwa maskini na visingekuwa na silaha nzito kama visingefanya biashara. "Tunajua kuwa biashara ya madini ni sehemu kubwa ya kipato chao."
GW itatoa wito kwa wauzaji ambao wanapata madini kutoka DRC kubainisha madini hayo yanakotoka. Pia wanapendekeza kuwepo kwa uchunguzi wa mipakani na ukaguzi kwenda sambamba na maazimio haya. Kulingana na shirika hilo la kutetea haki za binadamu ni makampuni machache tu yamefanya baadhi ya jitihada, lakini hayo hayatoshi.
"Sera za makampuni zimekuwa katika karatasi tu. Na idadi kubwa ya makampuni, ikiwa ni pamoja na Apple, hayajakubaliana na tatizo hilo kabisa," Parsons anasema.
"Madini ya maeneo ya vita" – aina ya bati, tantalum na tungsten – baada ya kuchimbwa, yanasafirishwa kutoka DRC kwenda Asia Mashariki ambako yanasindikwa na kuwa vito vya thamani kwa ajili ya bidhaa za elektroni. Vito hivyo vinatumika katika kutengeneza vifaa vya i-pods, kamera za digitoo, simu za mkononi na kompyuta ndogo duniani kote.
Global Witness inasema kuwa, hadi sasa, serikali zimefanya kazi ndogo mno kukabiliana na na biashara ya madini katika maeneo ya vita. Lakini mwaka uliopita Marekani iliendesha hoja. Mei 2009, rasimu ya sheria inayotaka makampuni ya Marekani kuonyesha asili ya madini yake ulipelekwa kwa seneti.
Kulingana na Mwakilishi Maalum wa EU katika Maziwa Makuu ya Afrika, Roeland van de Geer, EU imethibitisha kujitolea kwake na kuchukua hatua za kisheria za kushirikiana katika kupambana na uchimbaji haramu wa madini katika maeneo yenye vita.
Lakini hadi sasa EU haijawa na sheria yoyote ile inayotaka kuzuiwa kwa madini kutoka maeneo yenye vita mashariki mwa DRC kuingia Ulaya.
"Baadhi ya wataalam wanataka kutumiwa kwa ‘mpango wa Kimberly’, ambao unazuia almasi, wakati wengine wanadhani kuwa hakuna uwezekano kuwa hatua za kisheria za kimataifa zitachangia katika kupambana na uchimbaji haramau wa madini," Van de Geer aliiambia IPS.
Kwa sasa ofisi yake inafanya kazi kama sekretariati ya uchimbaji haramu wa maliasili mashariki mwa DRC.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linaloandaa njia ya kuanzisha kuzuiwa kwa mali na vikwazo vya kusafiri kwa makampuni ambayo yanaunga mkono vikundi vyenye silaha mashariki mwa DRC kupitia biashara haramu ya madini.
Uchimbaji haramu wa maliasili siyo jambo jipya mashariki mwa DRC. Imekuwa sehemu ya mgogoro tangu ulipoanza kwa mara ya kwanza mwaka 1996 na umewekwa katika kumbukumbu za mashirika yasiyo ya kiserikali na Jopo la Wataalam wa Umoja wa Mataifa.
(END/2010)
|
|
|