Tanzania Muswada wa Fedha za Uchaguzi Utawawezesha Wanawake Na Marko Gideon
DAR ES SALAAM, FEB 28 (IPS) - Hivi karibuni, suala la Muswada wa Kudhibiti Fedha za Uchaguzi lilichukua vichwa vya habari magazeti, redio na televisheni nchini.
Akizungumzia Muswada huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, alisema "Sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi iliyopitishwa na Bunge katika kikao kilichopita ni jambo la kihistoria na ni hatua ya kimapinduzi".
Alisema sheria hiyo ina nia ya kuzuia nchi kufika pabaya. "Inatuweka mahali pazuri pa kuanza mapambano na watu wanaotaka kupata uongozi kwa nguvu ya pesa. Pia inasaidia kuwabana watu wanaogeuza haki yao ya kupiga kura kuwa ni mradi au bidhaa ya kunufaika nayo kipesa kwa kuiuza," alisema rais Kikwete wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa viongozi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), jijini Mwanza Februari 25, 2010.
"Sasa ole wao wahongaji, ole wao wahongwaji na ole wao wanaoomba kuhongwa," alionya rais.
Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi wa Mwaka 2009 (The Election Expenses Bill, 2009), ulipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao chake cha 18 kilichomalizika Feberuari 12, 2010. Kwa kiasi kikubwa hatua hii inaonekana kuwa dhamira ya dhati ya serikali ya kupambana na rushwa nchini.
Kulingana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, tathmini iliyofanywa mwaka 2009 na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Kupambana na Rushwa (United Nations Convention Against Corruption 2003 – UNCAC) kwa kushirikiana na Serikali za Uingereza na Uholanzi kuhusiana na mapambano dhidi ya rushwa nchini imeonesha kwamba Tanzania ni nchi inayopambana na rushwa kwa dhati.
"Aidha, Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika ambayo imekamilisha mchakato wa tathmini hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Kupambana na Rushwa," alisema Waziri Mkuu Pinda katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge la 18 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Februari 12, 2010.
Hata hivyo, alisema rushwa bado imeendelea kujikita katika nyanja za utoaji huduma kwa jamii, na utoaji kandarasi.
"Aidha, rushwa ipo katika chaguzi hasa za ndani ya vyama vya siasa, Taasisi na Asasi ambazo uongozi unapatikana kwa njia za uchaguzi, hususan Uchaguzi Mkuu. Mara zote rushwa inalenga zaidi katika mapato ya kifedha na rushwa ya zawadi," alisema.
Pamoja na kuwa na msimamo tofauti, kambi ya upinzani Bungeni, iliunga mkono Muswada huo.
Akitoa mchango wa kambi ya upinzani Bungeni, mbunge wa viti maalum kutoka chama cha CHADEMA, Halima Mdee alisema kambi yake inatambua umuhimu wa uwepo wa sheria hiyo yenye lengo la kudhibiti matumizi ya fedha wakati wa kampeni, lakini upinzani ndiyo umekuwa mwaathirika mkuu wa fedha chafu na safi wakati wa uchaguzi na kubainisha kuwa ni wao kwa miaka mingi wamekuwa wakidai uwepo wa sheria hiyo.
Mbali ya kambi ya upinzani kukiri kuathirika na nguvu ya fedha wakati wa uchaguzi, kundi ambalo halijasikika sana, lakini linaathirika moja kwa moja na fedha hizo ni wanawake.
Pamoja na kampeni kubwa kuhamasisha kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika nafasi za ubunge katika nchi mbalimbali duniani, bado idadi ya wanawake inabakia kuwa ya chini ikilinganishwa na wenzao wanaume.
Kulingana na takwimu za karibuni za Muungano wa Mabunge Duniani, (IPU), idadi ya wabunge wanawake duniani ni asilimia 18.3 tu mwaka 2008.
Tanzania imepiga hatua, pamoja na kwamba bado haijafikia shabaha ya usawa wa kijinsia katika ngazi ya utoaji wa maamuzi ya 50:50 kama inavyotakiwa na Umoja wa Afrika.
Kulingana na makala ya shirika la habari la IPS, ya Julai 2009, Tanzania ina asilimia 30.4 ya wabunge wanawake. Lakini ili kufikia shabaha ya 50:50 ifikapo mwaka 2015, kuna haja ya kuwepo kwa mabadiliko ya kisheria, kitamaduni na kimtizamo juu ya kuwapa wanawake uongozi katika nchi ambayo bado ina mfumo dume.
Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi wa Mwaka 2009 ni hatua chanya katika kuleta usawa wa kijinsia. Hii ni kutokana na wanawake wengi hasa wanaogombea katika majimbo kushindwa kupambana na wanaume ambao baadhi hupata uongozi kwa nguvu ya pesa.
(END/2010)
|
|
|