SIASA Suala la "Wewe Kwanza"Katika Kuzuia Umilikaji wa Silaha za Nyuklia Uchambuzi na Haider Rizvi
UMOJA WA MATAIFA, Feb 3 (IPS) - Ni utata unaoendelea juu ya mpango wa nyuklia wa Iran unaosaidia kuendeleza ajenda ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia umilikaji wa silaha za nyuklia? Kwa idadi kadhaa ya wanadiplomasia na wataalam ambao walishiriki katika mijadala ya zamani ya umoja wa Mataifa kuhusu kuenea kwa silaha za nyuklia, jibu ni ndiyo – pamoja na kwamba siyo muhimu kwa sababu zilizotarajiwa.
"Iran inapinga undumilakuwili," David Kreiger, rais wa shirika la Nuclear Age Peace Foundation (NAPF), lenye makao yake nchini Marekani aliiambia IPS. "Unawezaje kuwa na msimamo mmoja unaopinga mpango wa Iran wa kurutubisha madini ya uranium na msimamo mwingine ambao uko kimya kabisa kuhusu silaha za nyuklia za Israel?"
Israel inaaminika kuwa na zaidi ya mabomu 300 ya nyuklia, pamoja na kwamba silaha zao zinabakia kuwa siri kubwa.
Utawala wa Barack Obama nchini Marekani kwa sasa upo katika jitihada za kimataifa za kushughulikia suala la Iran la kurutubisha madini ya uranium, lakini unaendelea kubakia kimya juu ya kutoa wito wa kuifanya Mashariki ya Kati isiwe ukanda wenye nyuklia, Kreiger alibainisha.
Ana imani suala hili halitakuja kutatuliwa kama mataifa yenye nyuklia, hasa yale yanayotoka uzingo wa Magharibi, yanabakia yasiyokuwa na dhamira ya kuachana na silaha zao za nyuklia.
Uongozi wa Iran umerejea tena na tena kukanusha kuwa ina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia, na kudai kuwa inaendeleza mpango wa amani wa kuzalisha nishati za nyuklia na ni haki yao ya msingi na kwamba kwa kufanya hivyo haikiuki Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT).
NPT imepitishwa na mataifa yote ambayo yanashikilia uanachama wa Umoja wa Mataifa, isipokuwa India, Pakistan, Israel na Korea Kaskazini. Mkataba wa mwaka 1968 unaruhusu watiaji saini wake kuzalisha na kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani, na kutaka mataifa yenye silaha za nyuklia kuchukua hatua ya kuondokana na silaha zao hizo.
Kwa upande wake, kwa nguvu zake zote Iran imepingana na mataifa ya Magharibi kutokana na shutuma zao kuwa inajaribu kutumia mpango wake wa nyuklia kwa malengo ya kijeshi, na kudai kuwa Marekani na mataifa mengine yenye nyuklia wanapaswa kuchukua hatua kuachana na silaha zao za nyuklia, kama wanavyotakiwa kufanya hivyo na NPT.
Katika Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa – ambayo imepewa kazi ya kujadili suala la kuzuia kuenea kwa nyuklia – idadi kubwa ya wajumbe wameuliza maswali juu ya kukosekana kwa dhamira kwa upande wa mataifa makubwa kusonga mbele na mipango ya kukomesha silaha za nyuklia.
"Hatukubaliani na sababu zozote zile za kutengeneza au kumiliki kwa wakati wote silaha za nyuklia," alisema Luiz Filipe de Macedo Soares, mwenyekiti wa New Agenda Coalition (NAC) kutoka Brazil, katika Mkutano wa Baraza Kuu mapema mwezi huu.
Ikiwa imeanzishwa mwaka 1998, NAC inahusisha nchi kadhaa ambazo zimeachana na mipango yao ya nyuklia ili kuzingatia NPT, nchi hizo ni Misri, Ireland, Mexico, New Zealand, Sweden, Afrika Kusini na Brazil.
"Kuachana na silaha za nyuklia na kuzuia kueneza silaha hizo ni mambo ambayo yanahusiana na inayofaa kushinikizwa kwa pamoja," alisema Soares. "Kwa hiyo mipango yote hiyo inahitaji mafanikio ya kuendelea na yasiyorejea nyuma."
Kwa NAC, ni dhahiri kuwa uhakika pekee dhidi ya kuzuia kuenea na matumizi ya silaha za nyuklia ni kutokomeza kabisa na kuhakikisha zimetokomezwa kabisa silaha zote.
"Kutokana na kwamba idadi ya mataifa kadhaa yanaona kumiliki silaha za nyuklia ni muhimu kwa usalama wao, inawezekana kukawepo na nchi nyingine ambazo zitataka kuwa na silaha hizo, na hatari itaendelea kuwepo ya kwamba zinaweza kuangukia katika mikono ya watu wasiokuwa watawala," Soares alisema.
NAC haikubaliani na "sababu yoyote ya kutaka kuwa na silaha hizo au kuendelea kumiliki milele silaha za nyuklia kutoka kwa nchi yoyote ile ", alisema Soares, ambaye ana imani kuwa kuwa na silaha za nyuklia "hakuwezi kuchangia katika amani na usalama wa kimataifa".
Umoja wa Mataifa unakaribia kufanya mkutano mkubwa katika majira ya kiangazi yajayo kutathmini NPT. Katika taarifa ya karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema anataka mataifa yenye silaha za nyuklia kuchukua hatua madhubuti kuachana na silaha hizo.
Ban ametaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 15 kuitisha mkutano wa kilele juu ya kuachana na silaha za nyuklia, na ametoa wito kwa nchi zisizokuwa wanachama wa NPT kuondosha uwezo wao wa silaha hizo. "Kuondokana na silaha ni lazima kuimarishe usalama," alisema hivi karibuni.
(END/2010)
|
|
|