Inter Press Service News Agency
Saturday, July 31, 2010   23:19 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   ČESKY
   DEUTSCH
   ITALIANO
   JAPANESE
   NEDERLANDS
   POLSKI
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
Mabadiliko ya Hali ya Hewa Yanashambulia Kutoka Pande Mbili
Na Marko Gideon

DAR ES SALAAM, Jan 31 (IPS) - "Mabadiliko ya hali ya hewa ni halisi na yana athari kubwa kwa binadamu," alisema Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Batilda Burian alipokuwa akizindua Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani 2009, jijini Dar es Salaam Novemba 18 mwaka jana.

Aliwaambia washiriki wakati wa uzinduzi huo "Tunakutana hapa katika wakati mgumu kwenye historia, wakati ambapo sayari yetu inazidi kuwa na joto hadi kufikia katika kiwango cha hatari kutokana na viwango vya juu vya gesi zinazochafua hewa ambazo zimesababisha kuongezeka kwa joto na mabadiliko ya hali ya hewa," alisema Dk Burian. "Mabadiliko ya hali ya hewa ni halisi. Yanaathiri kila nyanja katika jamii yetu, kuanzia kwenye afya ya uchumi wetu hadi kwenye afya yetu na watoto wetu."

"Mabadiliko ya hali ya hewa yanahusu maji katika visima vyetu na mito, yanahusu chakula na malisho ya mifugo yetu na wanyamapori na yanahusu nishati, haki za binadamu na usalama wa mwanadamu," aliongeza Waziri Burian. "Ni haki ya kibinadamu kutokana na hatari yanayosababisha katika afya ya mwanadamu kama vile kuongezeka kwa matukio ya malaria na magonjwa mengine makubwa; kuhama kwa watu kwa wingi; matatizo ya maji na usambazaji wa chakula na kupoteza maisha ya watu na vipato na utamaduni wao."

Tathmini ya haraka ya hotuba ya Dk Burian inaonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa duniani yanashambulia kutoka pande mbili nchini Tanzania.

Upande wa kwanza ni ule wa uhaba wa mvua, ambao kwa maneno ya Dk Burian, umesababisha ukame uliosababisha vifo vya ng’ombe wengi katika mkoa wa Arusha.

"Hivi karibuni sote tumeshuhudia madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu kwa mfano... ukame mkubwa mkoani Arusha na maeneo ya kati mwa nchi yetu ambapo maelfu ya mifugo imekufa na hivyo kuathiri kipato na maisha ya watu katika eneo hilo."

Uhaba wa mvua pia umekuwa moja ya sababu ya uhaba wa chakula nchini na hata kutangazwa kuathiri uchumi wa nchi.

Pamoja na kwamba Tanzania haikukumbwa na maandamano ya kupanda kwa bei za vyakula kama ilivyotokea Afrika Kusini, Nigeria, Haiti, Ivory Coast na nchi nyingine mbalimbali duniani hasa mwaka 2007 na 2008, hali ya chakula haikuwa ya kuridhisha mwaka 2008.

Kulingana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), Tanzania ilikuwa moja ya mataifa 22 duniani ambayo yalikabiliwa na kutishiwa na mgogoro wa chakula duniani.

Kupanda kwa bei za vyakula kuliripotiwa kuongeza mfumuko wa bei kukaribia dijiti mbili (asilimia 9.7) Aprili 2008.

Dk Burian alisema zaidi ya asilimia sitini ya ardhi nchini Tanzania inakabiliwa na hali ya jangwa na rasilimali maji zinazidi kupungua kutokana na ukame wa mara kwa mara ambao unaathiri kwa kiasi kikubwa vyanzo vya maji na bayoanuwai nyingine.

"Haya (mabadiliko ya hali ya hewa) yana madhara makubwa siyo tu katika maisha lakini pia katika uchumi na maendeleo ya kijamii," alisema Dk Burian.

Upande wa pili wa mashambulizi ya mabadiliko ya hali ya hewa ni kuongezeka kwa maji katika sayari yetu, kunakosababishwa na aidha kunyesha kwa mvua kubwa na vimbunga au kupanda kwa kina cha maji ya bahari.

Akitoa mfano wa nchini Tanzania, waziri Burian alisema madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa ni makubwa na ni ya kiwango cha juu kuwahi kutokea. Alisema haya yanaonekana katika kupanda kwa kina cha maji ya Bahari ambayo yanaathiri kilimo na kumeza visima vya maji katika maeneo ya mwambao pamoja na Zanzibar na hivyo kuongeza changamoto za kimaendeleo kwa jumuiya za mwambao wa pwani ambazo hutegemea zaidi kilimo cha kujikimu kuendesha maisha yao.

Kunyesha kwa mvua kubwa kupita kiasi pia kumeelezwa kuwa sehemu ya athari ya mabadiliko ya hali ya hewa. Majanga ya mafuriko huua watu wengi na kulingana na Dk Burian, takwimu zinaonyesha kuwa wanawake mara nyingi hufariki kwa wingi zaidi wakati wa majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa ya kuongezeka kwa maji katika sayari yetu kama vile mafuriko na vimbunga.

Akitoa mfano wa maporomoko ya udongo yaliyotokana na mvua kubwa wilayani Same, waziri Burian alisema kati ya watu 24 waliofariki dunia, 15 walikuwa wanawake, 8 wanaume na mmoja mtoto mchanga.

"Ni wakati muafaka sasa kulenga katika upande wa kibinadamu wa mabadiliko ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na usawa wa kijinsia," alisema.

Tangu katikati mwa mwezi Septemba mvua kubwa zimekuwa zikinyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi. Mvua hizi zimekwisha kusababisha mafuriko na vifo katika maeneo mbalimbali ya nchi. Mbali ya Same, mvua pia zimesabisha vifo mkoani Dodoma katika wilaya ya Kongwa na Morogoro katika wilaya ya Kilosa.

Katika baadhi ya maeneo, bado mvua hizo zinaendelea kusababisha mafuriko na kuna uwezekano pia zikawa neema katika kuongezeka kwa mavuno na hivyo kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Lakini katika baadhi ya maeneo, mvua zimesharipotiwa kuacha kunyesha na mazao kuanza kukauka hata kabla hayajafikia kipindi cha kuzaa.

Katika jiji la Dar es Salaam, wakazi wengi ambao hutegemea maji ya chini ya ardhi kwa ajili ya matumizi yao ya majumbani huhangaika usiku na mchana kutafuta maji kutokana na kukauka kwa visima kunakotokana na ukame wa muda mrefu.

Hivi ndivyo jinsi mabadiliko ya hali ya hewa yanavyoweza kushambulia sayari yetu kutoka pande mbili. (END/2010)

 

 








 Latest News from Africa
News in RSS
BURKINA FASO: Race to Achieve Goals on Sanitation
MALAWI: Innovative Campaigning by Women Candidates
SOUTHERN AFRICA: Realising Trade in Virtual Water
KENYA: Claim Disputed that Trade Measures "Aid" Counterfeiters
POLITICS-GUINEA: Women Amongst Also-Rans in Presidential Elections
ZIMBABWE: Badly Needed Work Begins on Bulawayo Water System
MADAGASCAR: Women Form Own Political Parties for Fair Representation
HEALTH: Uganda Authority Finding Less Counterfeit Drugs
TRADE-NAMIBIA: EU Backs Off on EPA
TRADE: Malawi Stands Firm on Conditions for Signing EPA
More >>
  Dernières Nouvelles
News in RSS
BURKINA FASO: Race to Achieve Goals on Sanitation
MALAWI: Innovative Campaigning by Women Candidates
SOUTHERN AFRICA: Realising Trade in Virtual Water
KENYA: Claim Disputed that Trade Measures "Aid" Counterfeiters
POLITICS-GUINEA: Women Amongst Also-Rans in Presidential Elections
A lire également>>