HAKI-UGANDA Wageni Katika Nchi Yao Evelyn Matsamura Kiapi
KAMPALA, Jan 29 (IPS) - Kila wakati wa jioni kabla ya jua kuzama, Pepe Julian Onziema hufunga milango katika vyumba vyake kwenye jengo la kupanga ambavyo hutumia pamoja na mpenzi wake katika kitongoji cha Ntinda mjini Kampala, kutokana na kukosa uhakika kama ataiona siku inayofuata. Onziema ni shoga na anaishi kwa hofu ya maisha yake kwasababu ya kampeni ya kitaifa inayowaona mashoga kuwa wahalifu nchini Uganda
Mwanaharakati maarufu huyo ni mratibu wa kitaifa wa Sexual Minorities Uganda, mtandao wa mashirika ya kutetea mashoga (LGBT).
Wakati gazeti nchini humo la Red Pepper lilipochapisha orodha ya watuhumiwa wa LGBT, jina lake lilikuwa limo – na kufuatia kuchapishwa kwa habari hizo, baadhi ya mashoga walifukuzwa na wenye nyumba wao, wakati wengine nyumba zao zilichomwa moto. Kama ilivyo kwa LGBTs wengine nchini Uganda, Onziema amekamatwa, kutemewa mate, kushambuliwa, kutukanwa na hata kupigwa mawe na majirani. Hawezi tena kutumia usafiri wa umma au kukaa kwa furaha katika mgahawa kwa hofu ya kutambuliwa na kutupwa nje.
Wakati kosa la kuchukiwa likifanywa dhidi yake, hawezi kuripoti kwa polisi, kwasababu kufanya mapenzi kati ya watu wenye jinsia moja nchini Uganda ni kinyume na sheria.
"Ni ulimwengu wa kijinga tunaoishi kama mashoga. Tunateseka kweli," Onziema anasema.
Muswada
Katika miezi ya karibuni kampeni iliyoongozwa na wabunge na viongozi wa kidini imeongeza ubaguzi.
Ngono kati ya watu wa jinsia moja ni kosa linalostahili adhabu ya kifungo cha maisha katika vifungu vya Kanuni ya Adhabu na Katiba ya mwaka 1995.
Lakini Aprili 2009, waziri wa maadili na uadilifu, Nsaba Buturo, alitangaza sheria za sasa hazitoshelezi kupambana na ushoga, ambao aliuelezea kama 'kukosa maadili na suala lisilokuwa la Kiafrika'.
Kwa sasa Uganda iko katika mchakato wa kupitisha Muswada wa Kupambana na Ushoga (2009) ambao ni kosa la jinai kuwa shoga. Vifungu vyenye utata katika rasimu ya muswada ni pamoja na hukumu ya kifo katika fasili mpya ya kosa la jinai la "ushoga wa kukithiri" – ambapo inahusu shoga mwenye VVU anapofanya ngono na mtu ambaye aidha ana umri wa chini ya miaka 18 au mlemavu. Hukumu hiyo ya kifo pia ipo katika kukamatwa mara nyingi kwa mtu akifanya ngono na mwenzake wa jinsia moja.
Muswada pia unatishia kutaka wazazi, wenye nyumba za kupanga na wafanyakazi wa afya kutoa taarifa za LGBT ama sivyo watafunguliwa mashitaka.
"Wale ambao wamesoma kisawa sawa muswada huo watatambua kuwa unamwathiri karibu kila mtu. Ni Muswada ambao umma haujahamasishwa juu yake na sisi kama mashoga pia hatujapewa fursa ya kuhamasisha umma juu yake," alisema Onziema.
Upinzani
Kusimamia haki zao za binadamu – iwe haki za afya, kujieleza, au kuishi – ni hatari kwa jumuiya ya mashoga nchini Uganda.
Juni 2008 katika mkutano wa kimataifa kuhusu UKIMWI/VVU mjini Kampala, Onziema alikuwa miongoni mwa LGBT na wanaharakati wa VVU/UKIMWI waliotoa misimamo ya upinzani ya amani iliyotolewa na mkurugenzi mkuu wa Tume ya UKIMWI Uganda, Dk Kihumuro Apuuli, kuwa hakuna fedha zitaelekezwa katika programu za VVU zinazolenga wanaume ambao hufanya mapenzi na wanaume wenzao.
"Mashoga ni miongoni mwa watu wanaochochea zaidi kuenea kwa VVU nchini Uganda, lakini kutokana na rasilimali chache, hatuwezi kuelekeza programu zetu sasa," aliripotiwa akisema.
Wakati wanaume ambao wanafanya mapenzi na wanaume wenzao huonekana kama watu waliopo katika hatari kubwa ya kuambukizwa na kuambukiza VVU, hakuna programu za kuwaingiza katika mkakati wa kitaifa wa kupambana na VVU/UKIMWI.
"Nilifanya kazi kama mshauri rika wa VVU kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo kwasababu nilikuwa nasaidia wapinzani wanaofanya mapenzi ya jinsia moja," Onziema anasema.
LGBTs wengi wanaogopa kwenda kupima VVU au hata kutoa ushauri nasaha kutokana na unyanyapaa wa aina mbili wa kuwa wachache wenye kupendelea aina hiyo ya mapenzi na kuwa na VVU.
"Tulikuwa na watu ambao wanajua hali zao na wengine ambao walikwenda kupatiwa Ushauri Nasaha na Kupima (VCT) chini ya kivuli kwamba wanakwenda moja kwa moja. Tunahitaji mifumo na sera ambapo mashoga wanaweza kuelezea waziwazi hadithi zao ili madaktari waweze kusimamia tiba zao vema," Onziema alisema.
Kufuatia kukamatwa kwake katika maandamano, polisi ilimlazimisha kwenda kufanyiwa vipimo vya mwili "kujua" jinsia yake.
"Walikuwa wakibishana kijinga juu ya jinsia yangu. Maafisa wawili wa kike waliingia kwenye chumba changu, wakati wa tatu, mwanaume, alisisima katika dirisha. Walinitaka kuvua nguo. Kutokana na kusita, polisi mmoja mwanamke aliamua kunivua chupi kwa nguvu na kushika sehemu zangu..."
Shinikizo la wafadhili
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa akikosoa ushoga kwa muda mrefu, na aliunga mkono kwa nguvu muswada mpya. Hata hivyo, katika mkutano wa hivi karibuni na wanachama wenzake wa chama tawala cha National Resistance Movement katika Ikulu Jan. 13, Museveni alisema asingeunga mkono Muswada ambao unahusisha hukumu ya kifo.
"Hili ni suala la sera za kigeni na inabidi kujadili katika hali ambayo haitaathiri kanuni zetu, lakini pia kuzingatia maslahi yetu ya nje," Museveni aliwaambia wanachama, akiwataka 'kwenda polepole' juu ya Muswada. Hakufafanua zaidi.
Mashirika ya haki za binadamu yametoa wito kwa mataifa ya Magharibi kutokutoa misaada kwa Uganda kama Muswada huo wa kikandamizaji ungepitishwa: nusu ya bajeti ya taifa inategemea misaada ya kimataifa.
Wachambuzi wanapendekeza kuwa rais wa Uganda anapigia magoti shinikizo la kimataifa baada ya kubaini kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown, Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hilary Clinton wote wametoa wito kwa rais kufikiria upya kwa Muswada huo.
Mapema mwaka huu, Mbunge wa Chama cha Labour nchini Uingereza Harry Cohen alifikisha hoja bungeni akitaka serikali ya Uingereza kuidai Uganda iondoe adhabu za jinai katika ushoga. Serikali ya Marekani pia imetishia kuiondoa Uganda katika mpango wa African Growth and Opportunities Act (AGOA) kama Muswada huo ungepitishwa. AGOA ni mpango wa kiuchumi ambao unatoa upendeleo wa kutokutozwa ushuru kwa bidhaa zinazotoka nchi za Kiafrika.
Hata hivyo, Sempa, ambaye anadai ushoga umetoka nje, anasema Uganda haipaswi kuogopa shinikizo la wafadhili.
"Lazima tuwe na nguvu. Nchi yoyote ile (kama Uganda) kuingiza ushoga katika sera zake za nje ni kosa kubwa. Na kama uuzaji wetu wa pamba kwenda Marekani una maana kuwa tunapata ushoga kwa kubadilishana, hiyo ni biashara ambayo hatuwezi kufanya."
Spika wa bunge la Uganda, Edward Ssekandi, alisema mjadala wa Muswada huo utaendelea pamoja na Rais kutoa wito wa 'kwenda polepole’.
"Siku inapoisha, Naomba," Onziema anasema. "Naomba kwamba hakuna shoga yoyote ameingia kwenye matatizo siku hiyo. Hata sipati usingizi wa kutosha. Huwezi kuzima simu yako kwasababu mtu anaweza kuhitaji msaada. Unaweza kuokoa maisha."
(END/2010)
|
|
|