RUSHWA-SIERRA LEONE: Wimbo Wachochea Mjadala wa Utawala Mohamed Fofanah
FREETOWN, Nov 18 (IPS) - Hakuna kitu ambacho kimewahi kuchochea mjadala wa utawala bora nchini kama ilivyo kwa wimbo uliotolewa na mmoja wa wanasanaa maarufu nchini Sierra Leone, Emerson Bockarie.
Wimbo, "Yesterday Betteh Pass Tiday", uliorikodiwa kwa lugha ya Krio, una maana ya "jana ni bora kuliko leo". Umepeleka mawimbi ya na kuanzisha mjadala nchini kote, siyo kutokana na mashairi yake au midundo yake, au mtindo aina ya zouk ambao unapendwa zaidi nchini Sierra Leone, lakini kutokana na maudhui yake ya kutoa maoni kuhusu jamii.
Wimbo huo unalinganisha serikali iliyopita ya Chama cha Sierra Leone People (SLPP) na ile ya chama tawala cha All Peoples’ Congress (APC). Bockarie anasema kuwa serikali ya Sierra Leone ilikuwa mbaya chini SLPP, lakini sasa ni mbaya zaidi.
Wimbo huo unaonyesha rushwa, gharama kubwa za maisha, undugu, ukabila, usambazaji duni wa huduma, mishahara duni ya serikali na takwimu za kiuchumi, unahitimisha kuwa mambo hayajabadilika kuwa mazuri chini ya serikali mpya.
"Tunapenda wimbo huu kwasababu Emerson amesema kila kitu, hakuna kinachoonekana kusonga mbele," alisema Sahid Sesay mwalimu wa shule ya msingi mjini Freetown. Alisema serikali iliongeza mshahara kwa asilimia 20, lakini haujawa na faida "kwasababu bei zote na kila kitu katika soko zimepanda".
Serikali ya APC iliingia madarakani kwa jukwaa la mabadiliko, na katika hotuba yake ya uzinduzi Rais Ernest Bai Koroma alitangaza yeye na timu yake wameonyesha "kuwa hawavumilii kabisa rushwa".
Mohamed Turay, mtafiti msaidizi katika Chuo cha Fourah Bay mjini Freetown, alisema: "Nadhani bado serikali ina mikakati ya kupambana na rushwa tu kwa ajili ya kuridhisha matakwa ya wafadhili, bila kuitekeleza kikamilifu. Tume hiyo bado inaathirika na kukosekana kwa dhamira ya kisiasa."
Turay alitoa mfano wa Afsatu Kabba, waziri wa zamani wa nishati, ambaye alikiuka waziwazi sheria za manunuzi kwa kutoa zabuni kwa Income Electrix, kampuni binafsi ya kusambaza umeme, kuzalisha megawati 25 za umeme wakati kulikuwa na makampuni mengine ambayo yangeweza kuifanya serikali kutumia gharama ya chini na kwamba hata zabuni hiyo ilipotolewa ni 10MW tu zilizalishwa.
"Lakini hakuna kilichotokea katika hali kama hiyo. Sasa amehamishiwa kuongoza wizara ya uvuvi na rasilimali za majini. Tunawezaje kusema serikali ina nia ya kupambana na rushwa?" aliuliza Turay.
Pia alisema Sheria ya Tume ya Kupamba na Rushwa (ACC) ilielekeza kuwa viongozi waandamizi serikalini, ikiwa ni pamoja na wanandoa wenzao na watoto, walipaswa kutangaza mali zao. Wakati rais alipotangaza mali zake, mawaziri wengi na viongozi wa umma hawakutangaza mali zao, pamoja na kuwepo kwa tume hiyo.
Valnora Edwin, mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Sierra Leone linalojulikana kama Campaign for Good Governance, alisema kumekuwa na maboresho kidogo katika ngazi za serikali.
Edwin alibainisha kuwa Sheria Mpya ya ACC mwaka 2008 imeimarishwa, na tume sasa ina uhuru halisi. "Lakini nadhani tunapaswa kuona hakuna ng’ombe wa kafara," aliongeza kwa ukali. "Pia unaona kuwa serikali imekuwa ikijaribu kuleta umeme katika jiji, lakini bado haijaanza kufanya kazi kikamilifu, na isiwe tu katika mji mkuu lakini pia nchi nzima."
Edwin aliongeza kuwa mitandao ya usafiri na barabara ni duni, na gharama za mawasiliano ziko juu mno. "Mawasiliano ya simu nchini hayafanyi kazi, na makampuni ya simu ya binafsi yanatoza fedha nyingi. Yote haya yanachangia mazingira mabaya ya uwekezaji."
Alisema: "Hakuna mtu atakayekuja kuwekeza nchini, na wachache ambao wanakuja wanahamisha gharama kubwa za uendeshaji kwa walaji, hivyo gharama ya kuishi inakuwa juu mno.
"Nadhnai bado hatujapata watu wanaofaa kusukuma nchi mbele, hivyo ni hali kama hiyo kama ilivyokuwa kwa serikali ya zamani ambayo ilikuwa na matatizo ya muundo mbaya wa serikali kiutawala, kuzuia rushwa na kukuza uchumi. "Sekta ya afya ni mbaya zaidi, kwani imekuwa na uhaba wa wafanyakazi. Madaktari bado ni wachache. Hakuna manesi wenye ujuzi maalum, hakuna utafiti, na madawa hayatoshi na ni ya gharama kubwa. Tunaliona hili katika kiwango cha juu cha vifo vya watoto wachanga na uzazi," Edwin alisema.
Bado kuna matatizo katika usambazaji wa maji ya bomba katika mji mkuu, Freetown, acha katika wilaya. Mapungufu haya yanafuatia Ripoti ya Hali ya Haki za Binadamu 2008 iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu Sierra Leone (HRCSL).
Pamoja na kukubali kuwa kumekuwa na mafanikio mazuri ya serikali katika kutokudhibiti vyombo vya habari, na katika kufanyia mageuzi mahakama ili kuweza kuongoza vizuri masuala ya wilaya, ripoti ilisema kuwa ukandamizaji wa vyombo vya habari, mazingira mabaya ya magereza, vikosi vya polisi wanaokula rushwa, ulinzi duni wa haki za wanawake (ikiwa ni pamoja na kushughulikia kwa ufanisi na kwa mafanikio kwa unyanyasaji wa wanawake) bado kunaendelea.
Ripoti pia ilisema kuwa Sierra Leone ilikabiliwa na changamoto nyingi katika kutekeleza haki za binadamu (hasa kiuchumi na kijamii). HRCSL ilipendekeza kuwa serikali "zinatakiwa kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa huduma za afya za kutosha, ikiwa ni pamoja na madawa, magari ya kubebea wagonjwa, madaktari na wafanyakazi wengine wa afya katika hospitali na vituo vya afya nchini kote".
Afisa uhusiano wa wizara ya afya, Abasss Kamara, anakubali kuwa Sierra Leone ina kiwango cha juu kabisa cha vifo vya watoto wachanga duniani, lakini anadai serikali inachukua hatua kubwa kutoa huduma katika sekta ya afya, na kupunguza kwa kasi kubwa vifo hivyo.
"Tumeandaa Mpango Mkakati wa Afya wa Taifa kwa miaka mitano kushughulikia afya ya uzazi na watoto wachaga. Tumeshatoa mpango wa utekeleaji wa miezi mitatu kulenga vituo vya afya na hospitali katika wilaya tano na mji mkuu, ambao utaboreshwa katika mafunzo na vifaa vya kukabiliana na afya ya uzazi," Kamara alisema.
Alibainisha: "Tayari tumeshazindua mradi wa tiba kwa kutumia simu, na madaktari wa Sierra Leone wataweza kupata ushauri kutoka kwa wataalam duniani kote – hasa nchini India – kuwezesha upasuaji. Mradi huu utapunguza uhaba wa nguvu kazi na wataalam katika sekta ya utabibu."
Waziri wa habari, Ibrahim Ben Kargbo, aliiambia IPS kuwa serikai imeahidi kutekeleza ahadi zake zote nchini Sierra Leone.
Kargbo alisema kuwa sera zao zimetafsiriwa katika hali ya kuweza kutekelezeka. "Mtu anaweza kuona kuwa nchi iliboresha nafasi yake kwa kupanda kwa nafasi nane hadi 148 (kutoka 156 mwaka 2009) katika ripoti ya mwaka ya Mazingira ya Kufanya Biashara, ambayo ilihususisha nchi 183. "Hii ina maana kuwa tunajenga mazingira bora ya biashara, ajira na kumiminika kwa fedha."
Ripoti ya Mazingira ya Kufanya Biashara ilitolewa na Benki ya Dunia kufanya utafiti wa sheria zinazoathiri moja kwa moja biashara, na haipimi mazingira ya jumla kama vile ukaribu wa taifa na masoko makubwa, ubora wa miundombinu, mfumuko wa bei au uhalifu.
Kargbo aliendelea "Kwa ujumla Sierra Leone iliibuka mbele ya jirani wake Liberia (149), Ivory Coast (168) na Guinea (173) katika Mano River Union. "Tumesambaza umeme hali ambayo ilikuwa mbaya mno katika serikali iliyopita, na tunapanga kuboresha hali hiyo. Tumeweka kipaumbele katika kilimo, na kuongeza bajeti ya kilimo kutoka asilimia 1.7 (ambayo tulirithi) hadi 7.7. "Tutaelekeza nguvu katika maendeleo ya binadamu kwa kuboresha huduma za jamii. Kwa hili tutashinikiza kuendeleza sera zetu na kuacha utoaji wa huduma kuwa chini ya halmashauri za serikali za mitaa," alisema Kargbo.
Yote haya yanakwenda sanjari na Agenda ya Mabadiliko nchini, mkakati wa kupunguza umaskini.
"Watu wanatakiwa kuwa wavumilivu, kwasababu maendeleo yanakuja polepole, lakini rais ameahidi kuwa maisha yatakua mazuri kwa wananchi wa Sierra Leone – na tunamaanisha na tutaweza." Hivi karibuni ACC imesema kuwa waziri wa afya nchini humo na amepunguziwa kazi kama waziri wakati akijibu mashitaka yanayomkabili. Kamishina wa ACC, Abdul Tejan Cole, ameambia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu rushwa mjini Doha Novemba 9 kuwa zaidi ya watendaji wa serikali 17,000 ikiwa ni pamoja na rais na mawaziri wote na wabunge wameshatangaza mali zao kwa ACC.
Salamatu Bah, mfanyabiashara mdogo katikati mwa mji, alisema "Serikai inajaribu, na mambo yanazidi kuwa mazuri sasa kuliko hapo kabla. Sikubaliani na wimbo wa Emerson wa "Tiday Betteh Pass Yesterday", lakini hoja haitakiwi kuwa ni serikali gani inafanya vizuri au vibaya. Tumepiga kura kupata mabadiliko na ni mabadiliko ambayo tunayataka." (END/2009)
|
|
|