MAENDELEO: Mabadiliko ya Hali ya Hewa Kuongeza Njaa Afrika Julio Godoy
BERLIN, Nov 18 (IPS) - Afrika, bara ambalo tayari limeathirika na njaa na uhaba wa chakula, lina uwezekano wa kushuhudia matatizo yake hayo yakiongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kubadilika kwa mwenendo wa mvua, wanasema wataalam na wanasayansi.
Kulingana na takwimu za Taasisi ya Utafiti wa Hali Hewa ya Ujerumani, tofauti ya mwenendo wa mvua barani Afrika, hasa katika kanda ya Magharibi, umeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu miaka ya1980.
Harald Kunstmann, mkurugenzi wa taasisi hiyo, anasema wakati katika kanda ya Sahel ukame ambao ulianza miaka ya 1970 na 1980 haujabadilika sana, katika delta ya Volga kiasi cha mvua kwa mwaka kinabakia kuwa kilele kile, lakini sasa kinafuata mwenendo wa kukatikakatika.
Kwa upande wa delta ya Volga, "tumeona ongezeko dogo la kiwango cha mvua cha kama asilimia tano," Kunstmann, mtafiti wa mabadiliko ya hali ya hewa na mvua za kimbunga, aliiambia IPS. Wakati huo huo, "kuna kupungua kwa kasi kwa mvua katika mwezi wa Aprili, mwezi ambapo unaonyesha mpaka kati ya msimu wa mvua na wa ukame katika eneo hilo," alisema.
Kupungua huku kuna wakati kunafika hadi asilimia 70 ya mvua.
Jambo jingine linaloonekana katika kanda ya Volta wakati wa miaka 40 iliyopita ni kufupika kwa msimu wa mvua, na kuchelewa kwa kuanza kwa mvua hadi siku 30.
"Ongezeko la joto duniani linabadilisha hali ya maji baridi," Kunstmann aliiambia IPS. Wastani wa joto la juu unasababisha mvuke zaidi katika anga, na hivyo kusababisha mvua kubwa zaidi, lakini pia myeyuko wa haraka na kuganda kwa maji. "Madhara ya mabadiliko haya katika maji safi mara nyingi ni mafuriko ya mara kwa mara na ukame wa muda mrefu zaidi," Kunstmann alisema.
Katika kilimo, hali ya hewa ya aina hiyo ina madhara makubwa. Mafuriko na ukame vinaharibu mbegu na mashamba, hali ya hewa isiyokuwa ya kawaida inalazimisha wakulima kubadili ratiba za kilimo.
Mabadiliko hayo tayari yameshathibitishwa na wakulima wa Afrika, na wataalam katika nchi zenye viwanda vingi duniani.
Namanga Ngongi, mkulima nchini Cameroon, na rais wa Umoja wa Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), aliuambia mkutano wa hivi karibuni wa kilimo na mabadiliko ya hali ya hewa Salzburg, Austria,kuwa "ongezeko la joto duniani tayari linaangamiza kilimo barani Afrika. Kuna ukame wa mara kwa mara zaidi, mafuriko ya mara kwa mara, na pia uharibifu zaidi," alisema.
Uharibifu huu wa kilimo kupitia mabadiliko ya hali ya hewa unazidisha kuongezeka kwa njaa ambayo tayari ipo katika nchi nyingi za Afrika.
Kulingana na Ripoti ya Njaa Duniani, kama inavyopimwa na Taasisi ya Washington ya Kutafiti Sera za Chakula (IFPRI), tangu mwaka 1990 njaa imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika nchi tisa za Afrika: Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, njaa imeongezeka kwa asilimia 67, nchini Swaziland kwa asilimia 32, nchini Guinea Bissau, Zimbabwe, Burundi, na Liberia kwa asilimia 19, 18, 17 na 16.
Katika kipindi hicho, Misri ilikuwa taifa la Kiafrika pekee lililoweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa chakula na njaa. Mataifa mengine yaliyopata mafanikio aidha ni ya Mashariki mwa Asia, Uarabuni au mataifa ya Amerika Kusini.
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Ujerumani la Welthungerhilfe (Msaada wa Njaa Duniani) lilifikia hitimisho kama hilo. Kulingana na Ripoti ya Njaa Duniani mwaka 2009, kwa uchache katika nchi 28, nyingi katika kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, njaa inafikia katika "hali mbaya, na hata mbaya zaidi," inasema ripoti hiyo.
Shirika la Msaada wa Njaa Duniani pia linaiweka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kama nchi yenye matokeo mabaya zaidi katika kupambana na njaa, ikifuatiwa na Burundi, Eritrea, Sierra Leone, Chad, na Ethiopia.
Mbali ya mabadiliko ya hali ya hewa na vita, kuwa na sera zisizokuwa sahihi ni sababu ya msingi katika kushindwa kukabiliana na njaa, alisema Michael Windfuhr, wa shirika la kanisa la Ujerumani la Brot fuer die Welt (Mkate wa Dunia). "Bajeti za kilimo za taifa katika nchi nyingi za Afrika zimepunguzwa kwa asilimia 50 katika miaka 20 iliyopita," Windfuhr aliiambia IPS. "Lakini pia ushirikiano wa kimataifa na misaada ya maendeleo imeondoka kutoka kusaidia uzalishaji wa chakula wa ndani katika nchi zinazoendelea."
Zaidi ya hapo, sera mbaya za kilimo zimeharibu ardhi katika nchi nyingi za Afrika, na kuzifanya kuwa rahisi zaidi kukabiliwa na mmomonyoko wa udongo, na kupungua mavuno mashambani, Windfuhr aliongeza.
"Katika kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, ruzuku za kilimo barani Ulaya na Amerika Kaskazini na kuongezeka kwa uuzaji wa nje wa bidhaa za kilimo zinazozalishwa kwa ruzuku kubwa kwenda nchi zinazoendelea kumezingira uzalishaji wa ndani," alisema.
Kwa kulinganisha, baadhi ya nchi zinazoendelea kama vile Brazil, zimeonyesha jinsi ya kukabiliana na njaa kwa mafanikio, Windfuhr alisema. Kwa kufadhili familia maskini zinazoendesha kilimo cha kujikimu, Brazil tangu mwaka 2003 imeweza kusaidia baadhi ya watu milionbi 20 kujinasua na umaskini," alisema.
Lakini, kutoka kwenye mabadiliko ya hali ya hewa, Brazil pia inalengwa na kukosolewa kutokana na kuruhusu kumaliza misitu ya kitropiki katika kanda ya Amazon, kwa ajili ya malengo makubwa ya kilimo, hususan kufuga ng’ombe.
Katika ripoti yake ya ‘mabadiliko ya Hali ya hewa: madhara ya Kilimo na Gharama za Kuishi katika Mazingira ya Mabadiliko’, iliyoboreshwa Nov. 6, IFPRI pia inatoa wito kuangaliwa kwa athari zinazoweza kukumba sekta ya kilimo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
"Joto la juu linapunguza mavuno ya mazao yanayotakiwa wakati huo huo linasababisha kuongezeka kwa magugu na wadudu waharibifu wa mazao," Gerald Nelson, mwandishi mkuu wa ripoti aliiambia IPS. "Mabadiliko katika mwenendo wa mvua yanaongeza uwezekano wa kushindwa kukua kwa mimea na hivyo kupunguza uzalishaji."
IFPRI inasema kuwa, "Pamoja na kwamba kutakuwa na mafanikio katika baadhi ya mazao katika baadhi ya kanda duniani, madhara ya jumla ya mabadiliko ya hali ya hewa katika kilimo yanatarajiwa kuwa hasi, na kutishia usalama wa chakula duniani."
Katika ripoti yake, IFPRI inatoa wito wa kuangaliwa mahitaji maalum ya mazao ya ndani ya nchi na uzalishaji wa mifugo, upatikanaji wa masoko, na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa. Inatoa wito kwa mashirika ya maendeleo ya kimataifa na serikali za kitaifa "kuhakikisha kuwa msaada wa kujenga uwezo wa kiufundi, na kifedha unafikia jumuiya za wazawa."
Pendekezo jingine la IFPRI ni kuimarisha na kusambaza takwimu. Uangalizi wa mara kwa mara wa sura ya nchi kupitia vyombo vya kupimia vya kisasa ni muhimu, George Nelson alisema.
"Ufadhili wa programu za takwimnu za kitaifa unatakiwa kuongezwa ili waweze kutimiza kazi ya ufuatiliaji wa mabadiliko ya kimataifa," inasema ripoti hiyo. "Kuelewa uhusiano wa kilimo na mabadiliko ya hali ya hewa kiasi chakutosha kusaidia shughuli za kukabiliana na kuweza kuishi katika mabadiliko kwa kujitikita katika matumizi ya ardhi kunahitaji ukusaji mkubwa wa takwimu, usambazaji, na uchambuzi."
Hili ndilo ambalo Taasisi ya Ujerumani ya Utafiti wa Hali ya Hewa inafanya. Harald Kunstmann na taasisi yake wametengeneza mfano wa kompyuta ya kutabiri hali ya hewa kwa ajili ya Cameroon na nchi jirani ambayo inaangalia mabadiliko ya mwenendo wa mvua katika eneo hilo.
Mifano hii ni msingi wa ratiba mpya ya kukatua mashamba na kupanda, ambayo itafuata hali ya hewa inayobadilika, na kutumia mbinu za jadi za kilimo katika mwenendo wa mvua zinazopungua na zenye joto.
(END/2009)
|
|
|