TANZANIA Mabadiliko ya Hali ya Hewa Yana Sura ya Mwanamke Na Marko Gideon
DAR ES SALAAM, Nov 18 (IPS) - Juliet*, 20, ni mfanyakazi wa ndani katika kata ya Kinyerezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Anaamka saa 10 kabla ya jua kupambazuka, kujiandaa kwa ajili ya kazi itakayomchukua siku nzima. Kazi hiyo siyo nyingine, bali ni kuchota maji kwa ajili ya familia ya watu 8.
Ni saa 11 asubuhi, Juliet ameshapeleka ndoo kumi na mbili katika kisima cha jirani, kama umbali wa mita 500 kutoka nyumbani anakofanyia kazi. Ndoo hizo husubiri katika foleni, wakati yeye akirejea nyumbani kuendelea na kazi nyingine kama vile kusafisha nyumba, kumwandaa mtoto anayesoma shule ya awali, kuandaa kifungua kinywa na shughuli nyingine za jikoni.
Inapofika saa 3 anaamua kwenda kuangalia kama maji ambayo huyalipia shilingi 100 kwa ndoo yameshajazwa. Anakuta ndoo bado hazina maji. Anarudi nyumbani mikono mitupu na kurejea tena kisimani saa 5, hakuna maji, saa 7 mchana, ndoo zipo tupu. Anaamua kurejea saa 11 jioni, anakuta ni ndoo moja tu imejazwa maji.
Hapo Juliet anaamua kutenga maji yaliyopatika kwa ajili ya kupikia. Anakwenda kuchota maji katika kisima kingine kifupi kwenye bonde la karibu na nyumbani, ambacho maji yake yanajulikana kwa wenyeji kuwa siyo salama, yana harufu ya kuoza kwa mimea na wadudu. Haya yangetumika kwa ajili ya kufulia, kuoshea vyombo, kumwaga chooni, kuogea na kusafishia nyumba. Kazi hii anaimaliza saa moja usiku kabla hajaanza kupika.
Hadithi ya Juliet, ambaye alianza kufanya kazi za ndani miaka miwili iliyopita akitokea mkoani Singida ambako alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari akiwa kidato cha pili kutokana na wazazi wake ambao ni maskini kushindwa kuendelea kumlipia ada baada ya kushindwa kufaulu mtihani wa kidato cha pili, inawahusu wanawake na wasichana wengi, siyo tu jijini Dar es Salaam, lakini pia maeneo mengine ya Tanzania – mijini na vijijini. Tatizo la kukosekana kwa maji eneo la Kinyerezi kwa kiasi kikubwa linatokana na kushindwa kunyesha kwa mvua za vuli na masika mwaka jana. Hali hii imesababisha kukauka kwa visima na hivyo kuwepo kwa uhaba mkubwa wa maji kwa wakazi ambao karibu wote wanategemea maji ya visima.
Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 45% tu ya wakazi wa Dar es Salaam wanapata huduma ya maji ya bomba na chini ya robo ya wakazi wake wote katika jiji hilo wameunganishiwa maji ya bomba majumbani mwao.
Wakati watu wengi wanaweza wasijue ni kitu gani kimesababisha mvua kukosekana na kusababisha ukame katika maeneo mengi ya nchi na hususan jijini Dar es Salaam, ambako wananchi wake wengi hutegemea maji ya chini ya ardhi kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku, duniani kote mjadala unaendelea juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake kwa maisha ya kila siku ya jamii. Hizi ni pamoja na upatikanaji wa maji, nishati, usalama wa chakula, uchumi, athari za kijamii na hata haki za binadamu. Katika athari zote hizi, wanawake na wasichana ndiyo waathirika wakuu.
Akizindua Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani 2009, jijini Dar es Salaam leo (Novemba 18), Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk Batilda Burian alisema mabadiliko ya hali ya hewa ni halisi na yana athari kubwa kwa binadamu.
"Tunakutana hapa katika wakati mgumu kwenye historia, wakati ambapo sayari yetu inazidi kuwa na joto hadi kufikia katika kiwango cha hatari kutokana na viwango vya juu vya gesi zinazochafua hewa ambazo zimesababisha kuongezeka kwa joto na mabadiliko ya hali ya hewa," alisema Dk Burian. "Mabadiliko ya hali ya hewa ni halisi. Yanaathiri kila nyanja katika jamii yetu, kuanzia kwenye afya ya uchumi wetu hadi kwenye afya yetu na watoto wetu."
"Mabadiliko ya hali ya hewa yanahusu maji katika visima vyetu na mito, yanahusu chakula na malisho ya mifugo yetu na wanyamapori na yanahusu nishati, haki za binadamu na usalama wa mwanadamu," aliongeza Waziri Burian. "Ni haki ya kibinadamu kutokana na hatari inayosababisha katika afya ya mwanadamu kama vile kuongezeka kwa matukio ya malaria na magonjwa mengine makubwa; kuhama kwa watu kwa wingi; matatizo ya maji na usambazaji wa chakula na kupoteza maisha ya watu na vipato na utamaduni wao."
Akitoa mfano wa nchini Tanzania, waziri alisema madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa ni makubwa na ni ya kiwango cha juu kuwahi kutokea. Alisema haya yanaonekana katika kupanda kwa kina cha maji ya Bahari ambayo yanaathiri kilimo na kumeza visima vya maji katika maeneo ya mwambao pamoja na Zanzibar na hivyo kuongeza changamoto za kimaendeleo kwa jumuiya za mwambao wa pwani ambazo hutegemea zaidi kilimo cha kujikimu kuendesha maisha yao.
Alisema zaidi ya asilimia sitini ya ardhi nchini Tanzania inakabiliwa na hali ya jangwa na rasilimali maji zinazidi kupungua kutokana na ukame wa mara kwa mara ambao unaathiri kwa kiasi kikubwa vyanzo vya maji na bayoanuwai nyingine.
"Hii ina madhara makubwa siyo tu katika maisha lakini pia katika uchumi na maendeleo ya kijamii kwani inaathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya nishati," alisema na kuongeza, "hivi karibuni sote tumeshuhudia madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu kwa mfano kunyesha kwa mvua kubwa huko Same, Bagamoyo na Kongwa mkoani Dodoma ambazo zimesababisha kupotea kwa maisha ya watu, mali na miundombinu na pia ukame mkubwa mkoani Arusha na maeneo ya kati mwa nchi yetu ambapo maelfu ya mifugo imekufa na hivyo kuathiri kipato na maisha ya watu katika eneo hilo."
Akizidi kusisitiza madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani nchini Tanzania wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ya Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNPFA), yenye kaulimbiu "Kukabiliana na Mabadiliko ya Dunia: Wanawake, Idadi ya Watu na Hali ya Hewa", waziri aliendelea kusema kuwa ripoti hiyo inakumbusha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni zaidi ya teknolojia, ambapo tunazungumzia kuhusu ufanisi na kuzalisha hewa chache za kaboni, lakini pia yanahusu watu na ubinadamu. "Kutokana na kwamba ni tatizo la ubinadamu linahitaji hatua za kibinadamu kulitatua," alisema.
Akinukuu ripoti hiyo, alisema wakati mwananchi wa Marekani anazalisha gesi chafu ya kaboni mara 200 zaidi kila mwaka ikilinganishwa na mwananchi wa kawaida wa Ethiopia au Tanzania ambaye anatarajiwa kuathirika zaidi na mabadiliko ya joto na hali ya hewa, upatikanaji wa maji, na kuwa na rasilimali chache za kuweza kuishi katika mazingira ya mabadiliko hayo.
Alisema lakini kama ambavyo mabadiliko ya hali ya hewa yanavyoathiri dunia kwa viwango tofauti, yanaathiri pia nchi kwa viwango tofauti. "Maskini kwa ujumla wanaathirika zaidi, wanawake na wasichana ambao ndiyo maskini zaidi duniani wanaathirika zaidi."
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa wanawake mara nyingi wanafariki kwa wingi zaidi wakati wa majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile mawimbi ya joto na mafuriko na vimbunga.
Akitoa mfano wa hivi karibuni wa maporomoko ya udongo yaliyotokana na mvua kubwa wilayani Same, waziri Burian alisema kati ya watu 24 waliofariki dunia, 15 walikuwa wanawake, 8 wanaume na mmoja mtoto mchanga.
"Ni wakati muafaka sasa kulenga katika upande wa kibinadamu wa mabadiliko ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na usawa wa kijinsia," alisema, akiongeza kuwa Mawaziri wa Mazinfira Wanawake wa Afrika wameanzisha mtandao na kwamba wamekuwa wakishawishi na kufanikiwa kuingiza suala la jinsia katika mazungumzo yanayoendelea kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.
Mbadiliko ya hali ya hewa pia, kulingana na Dk Burian, yanarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) nchini Tanzania. Alisema vifo vinavyotokana na uzazi ni 578 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai, wakati vifo vya watoto wachanga ni 58 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa wakiwa hai. "Vifo hivi bado ni vingi mno na vinaathiri zaidi wanawake na watoto na familia zao," alisema. "Jitihada za kuboresha afya ya uzazi, watoto wanaozaliwa na watoto wachanga zitaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa." Hii itatokana zaidi na uhaba wa chakula na majanga ya kiafya ambayo yanazidishwa zaidi na uhaba wa maji, vimbunga na mafuriko.
"Wanawake hasa katika maeneo ya vijijini wataathirika zaidi kuliko wanaume. Wataathirika zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa kwasababu wanachangia kwa kiasi kikubwa katika nguvu kazi ya kilimo na kutokana na kuwa na fursa chache za kujiingizia kipato," alisema.
Katika taarifa yake ya ufunguzi, Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Balozi Charles Mutalemwa alisema miaka 10 yenye joto zaidi duniani imerikodiwa kuwa katika miaka 13 iliyopita tangu mwaka 1880 ambapo nchini Tanzania, tofauti za mvua zinasababisha changamoto halisi katika kilimo na kuleta wasiwasi katika maeneo mengi ya nchi.
"Ni uhalisia ambao sisi sote, kwa pamoja, tunapaswa kuchukua hatua za haraka kuchangia katika jitihada za kimataifa za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu zinazochafua hewa na pia kupunguza shughuli za kibinadamu ambazo zinasababisha uharibifu wa mazingira," alisema Balozi Mutalemwa.
Ripoti ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Dunia: Wanawake, Idadi ya Watu na Hali ya Hewa imezinduliwa huku dunia ikielekeza macho yake katika mkutano wa hali ya hewa duniani mjini Capehagan, Denmark Desemba 7 - 18.
Masuala ambayo yanatarajiwa kujitokeza katika mkutano huo ni pamoja na kuwa na mkataba ambao utaweka wazi jinsi nchi tajiri zitakavyopunguza uzalishaji wa gesi chafu zinazochafua hali ya hewa, ni kwa kiasi gani nchi kubwa zinazoendelea duniani kama China na India zitapunguza ongezeko lake la uzalishaji wa gesi hizo, jinsi gani ya kufadhili nchi zinazoendelea kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na pia kuwa na mikakati ya jinsi ya kuishi katika mazingira ya mabadiliko ya hali ya hewa na jinsi gani fedha hizo zitasimamiwa.
*Siyo jina lake
(END/2009)
|
|
|