SIASA Malawi Yataka Viongozi wa Mitaa Na Claire Ngozo
LILONGWE, Nov 17 (IPS) - Nchini Malawi, uchaguzi wa serikai za mitaa unafanyika mara chache na uko hatarini kupotea kama ilivyo kwa faru mweusi.
Kwa hakika, inaonekana kana kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa uko hatarini zaidi kupotea kuliko wanyama pori– kwasababu angalau faru weusi wanarejeshwa taratibu nchini Malawi. Lakini kwa sasa, inaonekana kana kwamba kuna matumaini machache kwa uchaguzi wa serikali za mitaa kufanyika mara kwa mara.
Hii inakuja baada ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa (EC) kusema haijapanga vizuri shughuli kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, kwasababu serikali haijatoa rasilimali.
Tangu kuanza kwa vyama vingi mwaka 1994, nchi imeshafanya uchaguzi wa serikali za mitaa mara moja, mwaka 2000. Chaguzi hazijafanyika, kama ambavyo zilitakiwa kufanyika mwaka 1995. Na uchaguzi wa serikali za mitaa ulipangwa kufanyika mwaka 2005, wakati madiwani waliochaguliwa mwaka 2000 muda wao ulipomalizika. Tangu wakati huo wananchi wa Malawi wamekuwa wakiishi bila ya kuwa na wawakilishi katika ngazi ya serikali za mitaa.
Na hii imesababisha Mtandao wa Kusaidia Uchaguzi Malawi (MESN), shirika mwamvuli la mashirika ya kiraia 100 kutaka kuangalia mfumo wa uchaguzi, kuanzisha hatua ya kisheria dhidi ya serikali ya Malawi kutokana na kushindwa kwake kufanya uchaguzi.
"Watu na demokrasia wana hasara hapa. Madaraka mikoani, uwazi, ushiriki wa watu katika maendeleo ya mitaa vitaendelea kuumia kwasababu hakuna wawakilishi halali kisheria kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda vizuri," alisema mwenyekiti wa MESN Aloisious Nthenda.
Katiba ya Malawi inasema katika Kifungu cha 147, uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika katika kila wiki ya tatu ya mwezi Mei, katika mwaka unaofuata uchaguzi mkuu. Malawi ilihitaji kuwa na uchaguzi wa kwanza mwaka 1995 baada ya kuanza kwa vyama vingi lakini hili halijafanyika.
Nchi ilifanya uchaguzi wake mkuu Mei mwaka huu, na uchaguzi wa mitaa ulipaswa kufanyika Mei 2010. Lakini hakuna kalenda ya uchaguzi. MESN inatuhumu serikali kukiuka matakwa ya katiba.
Nthenda alisema sheria ndogo hazitekelezwi, na rushwa ilikuwa kubwa katika mikutano ya serikali za mitaa, kwasababu hakukuwa na wawakilishi waliochaguliwa kihalali kuhakikisha kuwa rasilimali kwa maendeleo ya serikali za mitaa zinakwenda mahali zilipokusudiwa.
MESN siyo shirika pekee linaloona mapungufu ya kutokufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa; wanakijiji kutoka Mabuka-Mulanje, wilaya ya kusini mwa Malawi, wametishia kuandamana dhidi ya kushindwa kwa serikali kuwezesha uchaguzi. Maandamano yanatokea mara chache sana katika nchi hii ya amani barani Afrika.
Grace Katoni, mwanajumuiya huko Mabuka, ana wasiwasi umaskini unachochewa kwasababu hakuna wawakilishi katika ngazi za serikali kushinikiza maendeleo katika ngazi za chini.
Hadi asilimia 60 ya wananchi milioni 13.1 nchini Malawi wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa dola moja kwa siku kulingana na Umoja wa Mataifa. Nchini Malawi, dola moja inatosha kununulia tu mkate lakini kaya nyingi zinaona mkate kama anasa. Wengi wangeweza kuamua kutumia dola kununua kibaba cha unga wa mahindi na maharage kidogo au mboga za majani kwa ajili ya mlo mmoja.
"Kutokana na watu kushindwa kushiriki katika maendeleo ya eneo lao, kama ambavyo hatuna wawakilishi wa serikali za mitaa. Wabunge ni mara chache wanawasiliana nasi katika miradi ya maendeleo tunayohitaji," alisema Katoni.
Alielezea kuwa watu kutoka upande mwingine wa kijiji walikuwa na shida ya kufika kwenye kliniki karibu nao, hasa wakati wa msimu wa mvua, kwani inabidi wavuke mto ambao hauna daraja, na mara nyingi haupitiki. Alisema wengine wamekufa kutokana na kushindwa kufika kliniki baada ya kuugua.
"Hakuna mamlaka za mitaa kuwezesha ujenzi wa daraja katika mto huu. Tunaandaa maandamano kushinikiza serikali kufanya uchaguzi huu," alisema Katoni.
MESN inadai kalenda ya uchaguzi itolewe katikati mwa mwezi Novemba, ili mchakato wa uchaguzi uweze kusonga mbele. "Tayari tumeshawasiliana na wanasheria katika kufungulia serikali mashitaka ya kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa," alisema Nthenda.
Lakini kutolewa kwa kalenda hakuonekani kujitokeza hivi karibuni. Waziri wa serikali za mitaa Goodall Gondwe alisema katika mkutano wa wanahabari kuwa uchaguzi usingefanyika Mei kama ilivyotarajiwa, lakini pengine mwishoni mwa mwaka 2010.
"Serikali inapata ushauri kuhusu uchaguzi. Pengine Mei hii ijayo inaweza kuwa ni mapema mno kufanya uchaguzi huu," alisema Gondwe. Serikali ilikuwa ikipata ushauri kutoka kwa jamii mbalimbali juu ya jinsi madiwani wanaweza kufanya kazi.
"Ushauriano huu utawezesha serikali kuandaa sera ambayo itakuwa mwomgozo kwa serikali za mitaa," alisema Gondwe. Tayari serikali ilikuwa imeshatenga dola milioni 15 katika Bajeti yake ya taifa kwa ajili ya uchaguzi.
"Fedha hizi zinaonyesha kuwa serikali ina dhamira ya kufanya uchaguzi wa mitaa."
Kwa kutokufanya uchaguzi tangu mwaka 2005, na kutokuonyesha nia ya kufanya uchaguzi sasa, serikali ya Malawi inajenga rikodi mbaya ya kiutawala, kulingana na Chama cha Wanasheria Malawi, ambacho kinawakilisha na kusaidia wasomi wanasheria, na kufanya kazi ya kulinda umma kisheria.
Msemaji wa Chama cha Sheria Mercy Mulele alisema mapema mwezi huu: "Kutokana na kwamba suala hilo lipo katika Katiba, serikali inapaswa kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mitaa unafanyika." Tangu wakati huo ameahidi kuwa chama cha sheria kitaendelea kushinikiza.
Wakati huo huo EC, chombo cha kikatiba chenye jukumu la kuandaa uchaguzi huru na wa haki, usiokuwa na gharama na wa mara kwa mara, kama inavyotakiwa na Katiba, imesema haijapanga shughuli yoyote ile tayari kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, kwasababu serikali haijatoa rasilimali. (END/2009)
|
|
|