Inter Press Service News Agency
Wednesday, April 25, 2018   22:44 GMT    
   Homepage
   World Service
   East Africa
   Southern Africa
   West Africa
   Central Africa
 
   Environment
   Health-HIV/AIDS
   Education
   Rights
   Politics
   Economics
   and Finance
   Development
   Energy
   Population
   Culture
 
   Radio Service
 
   Français
 
   About IPS
 
   ENGLISH
   ESPAÑOL
   FRANÇAIS
   ARABIC
   DEUTSCH
   ITALIANO
   NEDERLANDS
   PORTUGUÊS
   SUOMI
   SVENSKA
   SWAHILI
   TÜRKÇE
PrintSend to a friend
Readers Opinions

TANZANIA
"Kilimo Kwanza", Je Tutafika?
Na Marko Gideon

DAR ES SALAAM, Juni 25 (IPS) - S)-Bajeti ya Tanzania ya mwaka wa fedha 2009/2010 inaongozwa na kaulimbiu ya "Kilimo Kwanza". Akifafanua maana ya kaulimbiu ya mwaka huu, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema "Hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa kilimo kinapatiwa rasilimali zaidi ikiwemo pembejeo na zana za kilimo".

Aliongeza Mkulo "Kwa kuzingatia mikakati tuliyojiwekea, tutazingatia kuwa msukumo unawekwa kwenye kilimo kwanza, na kusisitiza matumizi ya fedha za umma katika maeneo yenye kuleta tija."

Pamoja na sera ya kilimo kwanza kuonekana kama njia sahihi ya kujenga uchumi wa Tanzania, hasa katika kipindi hiki cha mtikisiko wa uchumi duniani, pia inaonekana kama mkombozi wa maisha ya wananchi ambao asilimia 80 ni wakulima wadogo wadogo wanaoishi vijijini.

"Ili kuutoa Uchumi wetu kutoka kwenye Uchumi uliyo nyuma na tegemezi na kuuingiza kwenye Uchumi imara, wa kisasa na endelevu tunahitaji kufanya Mapinduzi katika Sekta ya Kilimo na Viwanda. Mapinduzi haya yataongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza ukuaji wa Uchumi," alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika Hotuba yake ya Juni 22, ya mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge mwaka 2009/20010, na kuongeza kuwa "uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka, mavuno yataongezeka na hivyo ongezeko hilo litawawezesha wakulima kunufaika kupata kipato kutokana na kuuza mazao mengi zaidi nje. Hii pia, inavutia wawekezaji kujenga viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani kutokana na mazao ya kilimo.

"Tukifanya mapinduzi hayo, tutakuwa tumetekeleza ahadi yetu ya Maisha Bora kwa kila Mtanzania", alisema Waziri Mkuu.

Lakini hata hivyo, pamoja na kaulimbiu hiyo, bado bajeti haijaonyesha waziwazi kuwa inatoa kipaumbele cha kwanza katika kilimo.

Kwa kuangalia katika mgawanyo wa mapato, sekta ya elimu bado inaongoza katika kutengewa kiasi kikubwa zaidi cha fedha (shilingi bilioni 1,743.9), ikifuatiwa na sekta ya miundombinu (shilingi bilioni 1,096.6), sekta ya afya (shilingi bilioni 963.0) halafu sekta ya kilimo (shilingi bilioni 666.9).

Kulingana na mgawanyo wa kisekta hapo juu, inaonyesha kuwa kaulimbiu hiyo haijakwenda sambamba na dhamira ya serikali ya kutoa kipaumbele cha kwanza katika kilimo.

Akichangia hoja ya hotuba ya Waziri Mkuu katika kikao cha bunge la bajeti Jumatano, Juni 24, Halima Mdee (Mbunge), alisema kuna fedha chache tu za maendeleo ambazo zimetengwa katika sekta ya kilimo. Alisema kati ya bajeti nzima ya fedha za maendeleo katika sekta hiyo, ni shilingi bilioni 23 tu zitatokana na fedha za ndani. Nyingine zinategemea fedha za wafadhili.

Aliongeza kuwa kati ya shilingi bilioni 65 zilizotengwa kuendeleza kilimo katika mikoa yote nchini– ni shilingi milioni 55 tu zitatokana na makusanyo ya ndani.

Mdee alionyesha wasiwasi kuwa utegemezi huo hautaleta mafanikio katika sera ya kilimo kwanza kwani "Asilimia 70 ya fedha za wafadhili, ama haziji au zinachelewa".

Mbali ya wasiwasi huo, kuna masuala mbalimbali yanayojitokeza ambayo yanaonyesha uwezekano mdogo wa kutekeleza kivitendo sera hiyo. Pamoja na serikali kuhimiza watu walime, bado kuna tatizo la miundombinu ya kupeleka bidhaa za kilimo katika soko kama vile bara bara, bandari nakadhalika.

Vile vile kuna wasiwasi kama msisitizo katika kilimo bila kuwekeza katika umwagiliaji unaweza kuwa na tija kwa taifa.

" Nguvukazi tunayo, lakini maji hatuna. Wazo la umwagiliaji linaweza kuwa msaada mkubwa kwetu," alisema Mbunge Simba Chawene alipokuwa akichangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Kwa kuangalia historia, siyo mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo. Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutangaza waziwazi kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne – watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Tafsiri ya maneno haya ni kwamba nguvukazi na ardhi ni muhimu mno katika maendeleo ya kilimo nchini.

Serikali yake pia ilikwenda mbali zaidi na kuwa na sera ya "siasa ni kilimo". Azimio la Iringa la mwaka 1972 lilihimiza masuala mbalimbali kuhusu kilimo. Kaulimbiu kama "kilimo ni uti wa mgongo" na "nguvu kazi" hazikuishia tu katika nadharia, ila kivitendo na wananchi walihimizwa kuanzisha mashamba ya ushirika vijijini, matumizi ya mbolea na pia kilimo cha kisasa chenye tija.

Hata hivyo, kwa maoni yangu, sera ya sasa imekuja wakati ambapo dunia inakabiliwa na mitikisiko mitatu – mtikisiko wa uchumi, sekta za fedha na kuongezeka kwa bei ya vyakula duniani, na hivyo kudhoofisha jitihada za mataifa mbalimbali yanayoendelea kufikia lengo la kwanza la Maendeleo ya Milenia la kupunguza nusu ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani ifikapo mwaka 2015. Hali hii imetabiriwa kusukumiza wananchi wengi zaidi katika mataifa yanayoendelea, hasa katika bara la Afrika kwenye umaski uliokithiri.

Kulingana na Jukwaa la Uchumi Duniani, kuna haja ya kuweka msisitizo katika kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ili kukabiliana na hali ya sasa.

"Jitihada za kutokomeza umaskini na njaa na kukuza uchumi wa Afrika zitakuwa hazina matunda kama mahitaji ya wakulima wadogo wadogo katika kanda yanapuuzwa" kulingana na Msimamo wa Jukwaa la Uchumi Duniani kwa Afrika ambalo lilihitimishwa mjini Cape Town, Afrika Kusini, Alhamisi Juni 12.

‘‘Kuongeza uzalishaji wa wakulima hawa kunawezekana na ni jambo la msingi kwa usalama wa chakula kwa Afrika na ukuaji wa uchumi kwa ujumla,’’ alisema Florence Wambugu, mtaalam wa zamani wa teknolojia ya mimea katika kampuni ya Monsanto.

Kofi Annan, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa aliliambia jukwaa hilo kuwa wakulima wadogo katika Afrika wanaogelea peke yao. ‘‘Mwanamke huyu hana bima dhidi ya hali ya hewa isiyokuwa na uhakika, hapati ruzuku na hapati mkopo. Nasema ‘mwanamke’ kwasababu wengi wa wakulima wadogo katika Afrika ni wanawake.’’

Kauli ya Annan inaungwa mkono na Mbunge Chawene.

"Wakulima ni watoto na wanawake ambao ni wazee, huwezi kuona kijana katika kilimo," alisema Chawene huku akipendekeza serikali kutumia sera kama vile nguvukazi, kwani nguvukazi kubwa imehamia mijini.

"Hatuwezi kuleta mapinduzi namna hii, mapinduzi yoyote yale ni vita".

Jambo jingine linalotia shaka katika bajeti ya mwaka huu ni kama kweli serikali ina dhamira ya kweli ya kuweka msisitizo katika sekta ya kilimo kama ilivyokubaliwa na wakuu wa mataifa ya Afrika.

Mwaka 2003, katika Azimio la Maputo, viongozi wa Afrika waliahidi kutenga asilimia 10 ya bajeti za mataifa yao katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2008 kama sehemu ya jitihada zao za kufikia lengo la kwanza la Maendeleo ya Milenia – kupambana na umaskini na njaa.

Hata hivyo, hadi sasa ni mataifa machache tu ambayo yamefikia lengo hilo huku Tanzania ikiwa siyo miongoni mwa mataifa hayo. Mataifa yaliyofikia shabaha hiyo ni pamoja na Burkina Faso, Cape Verde, Chad, Ethipia, Mali, Malawi, Niger na Rwanda.

Pamoja na Tanzania kusisitiza katika kilimo kwanza, takwimu zinaonyesha kuwa kilimo kimetengewa asilimia saba tu ya bajeti ya mwaka huu kama ilivyokuwa kwa bajeti ya mwaka jana, na hivyo kuendelea kuwa chini ya lengo la asilimia kumi lililokubaliwa na Umoja wa Afrika.

‘‘Kilimo ni kichochea muhimu cha maendeleo ya uchumi, hususan katika Afrika ambapo watu wengi wanategemea kilimo,’’ rais wa Rwanda Paul Kagame alisema katika Jukwaa la Uchumi.

Maneno ya Kagame yanapaswa pia kuungwa mkono kwa vitendo na wanasiasa na viongozi wa Tanzania kwani kulingana na Mbunge Zitto Kabwe, "Miongoni mwa asilimia 33.5% ya watu maskini zaidi nchini Tanzania, asilimia 74% wanaishi vijijini" ambako wanategemea kilimo. (END/2009)

 

 
 Latest News from Africa
News in RSS
XML error: The element 'html' is used but not declared in the DTD/Schema.
  Dernières Nouvelles
News in RSS
DEVELOPPEMENT: Nous devons penser autrement à la "sécurité"
AUSTRALIE: Le port de Newcastle bloqué par les Guerriers du changement climatique
IRAN: L’examen d’un document clé à l’AIEA suggère un coup d’Israël
PAKISTAN: Les Ahmadis confrontés à la mort ou à l’exil
ETATS-UNIS: Le budget de la défense peut accroître alors que le public est fatigué de la guerre
A lire également>>